Tanzania kutoshiriki Miss World, sababu zatajwa

Thursday December 02 2021
miss world pic
By Nasra Abdallah

Wakati zikiwa zimebaki siku kumi kufanyika kwa mashindano ya Miss World, mwakilishi wa Tanzania Juliana Rugamisa hatoweza kwenda sababu zikitajwa ni kukwama kwa viza.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Desemba 2, 2021 na uongozi wa kamati wa Miss Tanzania kupitia taarifa yake kwa umma waliyoitoa kwenye ukarasa wao wa Instagram.

Mashindano ya Miss World ambayo mwaka huu yanatarajiwa kufanyika nchini Puerto Rico Desemba 12, mpaka sasa tayari wawakilishi kutoka nchi nyingine wameshawasili lakini mwakilishi wa Tanzania ameshindwa kufanya hivyo huku sababu ikitajwa kuwa ni kuchelewa kukosa viza.

Katika taarifa yao Miss Tanzania imesema “Kesho Desemba 3, 2021 ndio mwisho wa kuingia kambi ya Miss World baada ya nchi nyingi kupata changamoto ya kuchelewa kupata Viza ya Marekani kwa wakati, Miss World wakaongeza muda na kuruhusu hadi ikifika hiyo kesho iwe mwisho.

“Mashindano ya urembo ya Dunia mwaka huu yanafanyika nchini Puerto Rico, na Puerto Rico ni 'territory ' ya Marekani hivyo utahitaji viza ya Puerto Rico moja kwa moja ama utahitaji kuwa na Viza ya Marekani hata kama hutaingia Marekani ili kuweza kuingia Puerto Rico haswa kwa nchi za Afrika, maana hamna ubalozi wala consulate hata moja barani Africa,” imesema taarifa hiyo.


Advertisement

Hata hivyo kamati hiyo imefafanua kwamba janga la Uviko-19 nalo limebadilisha namna nzima ya upatikanaji wa Viza ya Marekani licha ya Serikali ya Puerto Rico kujitahidi kuandika barua kwa ajili ya washiriki wote akiwemo Miss Tanzania Juliana Rugumisa ya kuwawezesha kuipata kabla ya Januari.

Lakini ndio hivyo haijajulikana mpaka sasa itapatikana lini ambapo hati ya kusafiria ya mrembo huyo bado ipo ubalozini kusubiri Visa

“Hii ndio kusema kwa mwaka huu haitawezekana tena. Hata hivyo mwisho wa mashindano ndio mwanzo wa mashindano yajayo. Tunashukuru sana wadau wetu Miss World kwa jitihada kubwa na kuhakikisha hadi tunapata appointment mapema badala ya Januari, Serikali ya Puerto Rico ambao ndio wenyeji wa mashindano, umoja wetu wa 'country coordinators' dunia nzima imetufanya tumekua kitu kimoja badala ya kua washindani.

“Mwaka huu tulikua na mwakilishi bora sana Juliana_Rugumisa aliyetikisa dunia huu ni mwanzo na sio mwisho. Kwa mapenzi ya Mungu Miss World family tutakutana 2022. Kwa mashabiki zetu msikate tamaa kwetu iwe muendelezo wa maandalizi kwa ajili 2022,” imesema taarifa hiyo.

Advertisement