Tamasha la Sauti za Busara 2022 kupaza sauti za wanawake

Zimebakia wiki tano kabla ya kuanza kwa Tamasha la 19 la Sauti za Busara, huku mashabiki duniani kote wakisubiri kukutana katika eneo moja la aina yake, ambapo muziki wa Kiafrika unakuwa ukikonga nyoyo za watu kutokea Mji Mkongwe (Stone Town), Zanzibar.

Kama ilivyo kawaida, tamasha hili huutambulisha muziki kutoka sehemu mbalimbali za bara la Afrika unaopigwa mubashara, likijumuisha wanamuziki wadogo na wanaochipukia, huku likitoa msisitizo kwa wanamuziki wa kike kutoka Tanzania, Uganda, Afrika Kusini, Congo na Zambia.

Miongoni mwa wanamuziki watakaotumbuiza katika tamasha la mwaka huu ni Sampa The Great, ambaye uchanganyaji wake wa muziki wa mahadhi ya kufoka (hip hop) katika miondoko ya Kiafrika ni safari ya kujitafuta kwake, ni sehemu ya kujifunza mambo mapya yanayochagizwa na uzoefu wake wa kuishi Australia na mwongozo mzuri wa kiimani, kimwili na kiutamaduni alioupata kwao Zambia.

Sampa the Great ametumbuiza katika matamasha mengi makubwa ya kimataifa, akijizolea idadi kubwa ya mashabiki kwa aina ya burudani ya nguvu na ya kuvutia anayoitoa.

“Hatuchagui wasanii kwa misingi ya uanamke wao,” anaeleza Yusuf Mahmoud, Mkurugenzi wa tamasha.

“Wasanii wote wa Sauti za Busara wanatumbuiza muziki wa hali ya juu wenye asili, ubunifu na wa nguvu, kama itakavyodhihirika wakati Sampa The Great (Zambia), Siti & The Band (Zanzibar), Msaki na Nomfusi (Afrika Kusini), Suzan Kerunen (Uganda), Fanie Fayar (Congo) na Upendo Manase (Tanzania) watakapotumbuiza mwezi ujao chini ya bango la Paza Sauti: Kukuza Muziki wa Wanawake,” anasema Mahmoud.

Wasanii wengine watakaotamba katika tamasha hili ni pamoja na Sjava (Afrika Kusini), Sholo Mwamba na Bendi ya Wamwiduka (Tanzania), Maallem Abdelkebir Merchane (Morocco), Dendri Stambeli Movement (Tunisia), Sylent Nqo na Evans Mapfumo (Zimbabwe), Zan Ubuntu na Nadi Ikhwan Safaa (Zanzibar) na wengine wengi.

Kwa takriban miongo miwili, tamasha la Sauti za Busara limekuwa nguzo muhimu katika muziki wa Afrika ambalo faida zake zinakwenda mbali zaidi kwa kutoa ajira, biashara, fursa ya wasanii kujitambulisha, ushirikiano, kufahamiana, mafunzo na ukuzaji ujuzi, kuimarisha mshikamano wa kijamii, umoja na nje ya mipaka ya kikanda.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi hivi karibuni alilipongeza tamasha hilo kwa kuleta manufaa mengi visiwani humo.

Akizungumza na wadhamini muhimu wa tamasha hilo, alisema: “Naipongeza timu ya Sauti za Busara kwa kujitolea na mafanikio makubwa ya kuliweka tamasha hili hai, na shukrani za pekee kwa wafadhili na wadhamini wote waliofanikisha.

Pia ninawapongeza na kuwashukuru wanamuziki wengi ambao wamefanya tukio hili kuwa maarufu duniani ambalo huvutia wageni wengi zaidi kila mwaka.”

Kiingilio cha kushuhudia tamasha hilo kwa Watanzania watakaohudhuria ni Sh 6,000 kila siku au Sh16,000 kwa siku zote tatu za tamasha hilo.