Sri Lanka yamkamata 'Mke Mrembo Duniani' kwa kushambulia

Thursday April 08 2021
MREMBOPIC

Colombo, Sri Lanka (AFP).Polisi wa Colombo leo Alhamisi wamemkamata "Mrs World (Mke Mrembo Duniani)" kwa tuhuma za kushambulia katika fujo zilizotokea jukwaani ambako mama huyo alimvua mshindi mpya wa shindano la "Mrs Sri Lanka".

Caroline Jurie aliliondoa taji kutoka kichwani mwa Pushpika de Silva dakika chache baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa "Mrs Sri Lanka 2020" Jumapili katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Nelum Pokuna jijini Colombo.

Jurie ndiye aliyekuwa akishikilia taji hilo baada ya kulitwaa mwaka jana na akaenda mbele kutwaa taji la "Mrs World" ambalo huandaliwa na kampuni moja ya California ya Marekani.

Pushpika de Silva alipelekwa hospitali kutibiwa baada ya tukio hilo, lililoshuhudiwa na mashabiki waliojazana ukumbini na pia kurushwa moja kwa moja na mitandao ya kijamii.

"Tumemkamata Jurie na (mshirika wake) Chula Manamendra kutokana na shtaka la kushambulia na kusababisha  uharibifu katika ukumbi wa Nelum Pokuna," ofisa mwandamizi wa polisi, Ajith Rohana alisema.

De Silva aliwaambia waandishi nje ya kituo cha polisi cha Cinnamon Gardens jijini Colombo leo kuwa alikuwa tayari kufuta mashtaka kama Jurie angeomba radhi hadharani, lakini amekataa.

Advertisement

"Nilijaribu kulimaliza hili nje ya mahakama, lakini amekataa," de Silva alisema. "Naweza kusamehe na si kusahau."

Jurie hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

Vyanzo vya habari kutoka polisi vinasema kesi hiyo inaweza kusikilizwa wiki ijayo na kwamba mshirika wake anaweza kuachiwa kwa dhamana leo.

Jurie alikuwa anadai kuwa Silva aliachika na hivyo hakustahili kushinda taji hilo.

Ili kuwa na sifa ya kutwaa taji hilo, washiriki wanatakiwa wawe wameolewa. De Silva aliachika kwa mumewe, lakini kisheria bado ni wanandoa.

Waandaaji walisema wanadai fidia kutoka kwa Jurie kutokana na kusababisha hasara jukwaani na katika vyumba vya kubadilishia nguo ambako vioo kadhaa vilivunjwa.

Jurie pia amekuwa akituhumiwa na waandaaji kuwa analishushia hadhi shindano hilo.

Advertisement