Siku 16 tangu Wema ajifungue, Lulu Diva bado kimya
Muktasari:
- Lulu Diva, ambaye kwa miaka mingi alionekana kuwa mmoja wa marafiki wa karibu wa Wema, hajatoa pongezi hadharani katika mitandao ya kijamii wala kuonekana akimtembelea, jambo lililoibua maswali kuhusu uhusiano wao.
TAKRIBAN siku 16 zimepita tangu Wema Sepetu ajifungue mtoto wake mwezi Juni 2026, lakini ukimya wa Lulu Diva umeendelea kuzua mjadala kwa mashabiki.
Lulu Diva, ambaye kwa miaka mingi alionekana kuwa mmoja wa marafiki wa karibu wa Wema, hajatoa pongezi hadharani katika mitandao ya kijamii wala kuonekana akimtembelea, jambo lililoibua maswali kuhusu uhusiano wao.
Kwa miezi kadhaa kumekuwa na taarifa zisizo rasmi zikidai urafiki wao ulidorora, huku baadhi ya madai yakihusishwa na jina la msanii Whozu. Hata hivyo, hakuna upande uliowahi kuthibitisha chanzo halisi cha tofauti hizo.
Katika mahojiano ya awali, Lulu Diva aliwahi kusema hataki kuendeleza malumbano ya mitandaoni na pia aliwahi kuwataka watu kuacha kumbana Wema kwa maswali kuhusu kupata mtoto.
Baada ya Wema kujifungua, mashabiki wameendelea kuuliza kuhusu ukimya wa Lulu Diva kupitia machapisho mbalimbali ya Wema, wakitaka kujua iwapo bado kuna tofauti kati yao.
Mapema mwaka huu, Lulu Diva aliandika ujumbe uliotafsiriwa na wengi unahusu urafiki wao, akisema urafiki unaweza kufa bila kuanzisha uadui, ingawa hakumtaja Wema moja kwa moja.
Mwanaspoti lilimtafuta Lulu Diva kupata ufafanuzi. Amesema alikuwa na wateja dukani na kuomba atafutwe baadaye.
"Kipenzi sorry, nimtafute baadaye. Niko na wateja dukani," amesema.
Baada ya hapo simu yake iliita bila kupokelewa.
Hadi sasa hajatoa tamko rasmi kuhusu kujifungua kwa Wema au sababu ya ukimya wake. Kutokana na historia ya ukaribu wao, mashabiki wanaendelea kusubiri iwapo atatoa pongezi au kueleza msimamo wake kuhusu suala hilo.