R Kelly akutwa na hatia ya kuongoza genge la ukatili wa kingono

Muktasari:
- Nyota wa muziki wa R&B, R. Kelly jana (Jumatatu) alipatikana na hatia ya kuongoza mradi wa uhalifu wa ngono kwa takriban miaka 30, huku mahakama ikimtia hatiani katika mashtaka yote tisa, likiwemo kubwa la utapeli (racketeering) linalojumuisha matendo 14 yakiwemo ya usafirishaji binadamu kwa ajili ya ngono, rushwa, utekajina kutumikisha kinguvu.
New York, Marekani (AFP). Nyota wa muziki wa R&B, R Kelly jana (Jumatatu) alipatikana na hatia ya kuongoza mradi wa uhalifu wa ngono kwa takriban miaka 30, huku mahakama ikimtia hatiani katika mashtaka yote tisa, likiwemo kubwa la utapeli (racketeering) linalojumuisha matendo 14 yakiwemo ya usafirishaji binadamu kwa ajili ya ngono, rushwa, utekaji na kutumikisha kinguvu.
Baada ya wiki sita za ushahidi mkali, mahakama ilijadili kwa saa tisa tu kabla ya kumtia hatiani nyota huyo wa muziki mwenye miaka 54 kwa makosa ya kuajiri wanawake na watoto kwa ajili ya ngono, kabla ya kufanya nao mapenzi na kuwafanyia ukatili.
Kesi hiyo, iliyosimama kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona, inaonekana na wengi kuwa ni mafanikio makubwa kwa kundi la wanaharakati la #MeToo: ni kesi ya kwanza kubwa inayohusu uhalifu wa kingono ambao wanaotuhumu wengi ni wanawake weusi.
Akiwa amevalia tai ya bluu bahari, suti ya mistari na barakoa nyeupe, Kelly alikuwa ametulia, ameinamisha kichwa chini na kwa nyakati fulani akifumba macho yake yaliyokuwa nyuma ya miwani ya jua ya rangi nyeusi.
Anakabiliwa na adhabu inayoweza kuwa ya kifungo cha maisha jela, ikiwa ni anguko la ghafla la mwimbaji huyo wa kibao cha "I Believe I Can Fly" ambaye alisifika kama mfalme wa R&B.
Hukumu yake itatangazwa Mei 4.
"Tunatumaini kuwa uamuzi wa leo utaleta kiasi fulani cha faraja kwa waathirika," alisema mwanasheria wa serikali wa Wilaya ya Mashariki, Jacquelyn Kasulis.
Deveraux Cannick, ambaye ni wakili wa Kelly ambaye wakati wa utetezi alimuelezea nyota huyo wa muziki kuwa "mpenda mapenzi" na "alama ya ngono" na ambaye alivutia wengi, alisema timu yake "haijafurahishwa na uamuzi huo".
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa "wanafikiria" kukata rufaa.
Serikali ilikuwa na jukumu la kuthibitisha kosa la utapeli, ambalo ni nyeti na linahusiana na umafia na linalomuonyesha Kelly kuwa kiongozi wa genge ambalo lilifanikisha makosa yake. Matendo yanayounda kosa hilo ni pamoja na usafirishaji binadamu kwa jili ya ngono, utekaji, kutumikisha kinguvu na rushwa.
Wakiwa wameita mashahidi 45, wanasheria wa serikali walijumuisha mlolongo wa tuhuma za makosa kuonyesha kuwa Robert Sylvester Kelly alifanya bila ya kuchukuliwa hatua, akitumia umaarufu wake kukandamiza wanyonge.
Soma zaidi:Ushahidi wamuweka pabaya R Kelly
Kumtia hatiani kwa kosa la utapeli, mahakama ilitakiwa imkute na angalau makosa mawili kati ya 14 yanayounda uhalifu huo.
Ushuhuda uliolenga kuthibitisha matendo hayo ulihusisha ubakaji, kulewesha kwa kutumia dawa, kuwashikilia watu kinyume cha sheria na picha za ngono kwa watoto.
Jopo la majaji watano wanawake na wanaume saba lilibaini kuwa makosa mawili kati ya hayo yalithibitishwa.
Kelly alipatikana na makosa nane ya kuvunja sheria ya Mann Act, ambayo inazuia kusafirisha watu kwa ajili ya ngono.