Nelly, Kelly Rowland dakika za jioooni!
Muktasari:
- Wawili hao walikutana kwenye tamasha la Baby2Baby Gala 2024 huko Los Angeles, Marekani na mpenzi wa Nelly, Ashanti naye alihudhuriwa ikiwa ni takribani miezi minne tangu kujifungua mtoto wao wa kwanza Kareem.
Hivi karibuni Nelly, 50, na Kelly Rowland, 43, walijumuika pamoja jukwaani na kutumbuiza wimbo wao, Dilemma (2002) wenye miaka zaidi ya 20 tangu kuachiwa na kuiteka mitaa huku rapa huyo akizidi kujipatia ushawishi wa mitindo kwa vijana wengi.
Wawili hao walikutana kwenye tamasha la Baby2Baby Gala 2024 huko Los Angeles, Marekani na mpenzi wa Nelly, Ashanti naye alihudhuriwa ikiwa ni takribani miezi minne tangu kujifungua mtoto wao wa kwanza Kareem.
“Kwa hiyo, kwa kuwa nina malaika hapa, kwa kuwa nina mwakilishi wa Baby2Baby, nadhani ni sawa kufanya hivi kwa vile nilipata ombi hili kutoka kwa kila mtu..., tufanye unyama mwingi hapa,” alisema Nelly kisha kumuita jukwaani Kelly Rowland.
Basi Nelly na Kelly Rowland, mwimbaji wa zamani wa kundi la Destiny’s Child wakatuimbuiza wimbo huo ulioshika namba moja chati ya Billboard Hot 100 kwa wiki tisa mfululizo na hadi sasa ukiwa wimbo pekee kwa wawili hao kufikia rekodi hiyo.
Hata hivyo, kuna mengi nyuma pazia kuhusu kurekodiwa, kutoka na kubamba kwa wimbo huo, unajua nini?, ni kama goli la dakika za jioooni ambalo halikutarajiwa katika mechi ambayo timu zote mbili tayari zilishakuwa na mtazamo wa kutoka bila bila.
Nelly alishakamilisha albamu yake ya pili, Nellyville (2002) na yupo tayari kuitoa ila Mtayarishaji Muziki, Macon akampa mdundo mmoja matata uliotengenezwa na Bowser aliyeusampo kutoka katika wimbo wa Patti LaBelle, Love, Need and Want You (1983).
Alipousikia mdundo huo akaona anaweza kufanya jambo, mara moja akachukua kalamu na karatasi na kuanza kuandika mistari, kisha akazama chumba cha sindano, yaani Booth na kurekodi ila baadaye akaona sauti ya mtoto wa kike inahitajika.
Mwimbaji wa kwanza wa kike kumjia kichwani alikuwa ni Kelly Rowland ambaye walikutana katika ziara ya Total Request Live (TRL), kipindi cha MTV mwaka 2001, basi akampigia simu na kumueleza kuhusu kolabo hiyo na Kelly hakuwa na pingamizi.
Kelly akaibuka studio na kurekodi huku rapa huyo akirudia baadhi ya sehemu na kuongeza vionjo, ulipokamilika Nelly akaujumuisha katika albamu yake ‘Nellyville’ iliyotoka Juni 25, 2002.
Albamu ilipotoka DJ’s wa viwanja na watangazaji wa redio wakaanza kuucheza wimbo wa Dilemma wakati Nelly alishatoa wimbo wa kwanza na kwa ajili ya kuitambulisha albamu hiyo sokoni, Hot in Herre.
Ikumbukwe ngoma ya Hot in Herre nayo ilipata mapokezi mazuri ikishika namba moja Billboard Hot 100 ukiwa ni wimbo wa kwanza wa Nelly kufanya hivyo ila Dilemma ilikuja kwa kasi sana kiasi cha kuvuruga ratiba.
Kutokana na mapokezi makubwa ya ghafla, Nelly alilazimika kuiachia Dilemma kama wimbo wa pili kutoka katika albamu hiyo kinyume na mpango wa awali na punde tu nao ulishika namba moja katika chati.
Nyimbo hizo zilichochea albamu yake kufanya vizuri ikishika namba moja Billboard 200 huku akiuza nakala 715,000 katika wiki ya kwanza sokoni na haikuchukua muda kufikia hadhi ya Platnum, yaani mauzo ya nakala milioni 1.
Kwa mujibu wa Chama cha Rekodi za Muziki Marekani (RIAA), hadi Machi 2011, albamu ya Nellyville ilikuwa imegonga Platnum mara sita ikiuza nakala zaidi ya milioni 6.4 nchini humo ikiwa ni albamu ya 14 ya rap kuuza zaidi Marekani kwa muda wote.
Hadi sasa video ya Dilemma iliyowekwa YouTube Oktoba 6, 2009, imeshatazamwa (views) zaidi ya mara Bilioni 1.4 ikiwa video ya tatu ya Hip Hop duniani kufanya hivyo baada ya ‘In da Club’ ya 50 Cent na ‘Without Me’ ya Eminem.
Hivyo nyuma ya mafanikio ya albamu ‘Nellyville’ kuna Dilemma, na wimbo huu sio tu ulimtikisa Nelly, bali hata wasanii wa Destiny’s Child akiwemo Kelly Rowland na Beyonce ambao walilazimika kufanya mabadiliko ya tarahe za kutoa albamu zao. Beyonce alipanga kutoa albamu yake ‘Dangerously in Love’ Oktoba 2002 ila akasogeza hadi Juni 2003 na kumpisha Kelly Rowland kutembelea upepo wa Dilemma na kutoa albamu yake ‘Simply Deep’ hapo Oktoba 2002 wakati awali ilipangwa kutoka 2003.
Unaambiwa kurekodiwa kwa albamu hiyo ya Kelly Rowland kuliharakishwa sana na uongozi wa Destiny’s Child, ndani ya wiki tatu tu ilikamilika ili kwenda sambamba na mafanikio ya Dilemma.
Pia Dilemma ilijumuishwa katika albamu hiyo ya Kelly ukiwa kama wimbo wa kwanza kutoka na ulichangia pakubwa katika mauzo ya albamu yake hiyo, Simply Deep (2002).
Kwa kifupi Kelly Rowland, mwanamuziki aliyedumu na Destiny’s Child tangu mwaka 1990 hadi 2006, naye aliokota dodo chini ya mnazi dakika za jioooni kabisa kama magoli ya Italia dhidi ya mwenyeji Ujerumani katika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2006.