Ndoa ya Wastara kiboko yake

Wastara Juma akiwa amefunga ndoa na Sadifa Juma Hamis mwenyekiti wa UVCCM
Muktasari:
Wastara alifunga ndoa hiyo usiku wa Alhamisi na Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis
USILOLIJUA ni kama usiku wa kiza. Wiki iliyopita wakati wananchi wakiwa wametekwa na shughuli ya bomoabomoa ya nyumba za waliojengwa mabondeni, walishtukizwa na taarifa za nyota wa filamu, mwanadada Wastara Juma akiwa amefunga ndoa na kigogo mmoja wa UV-CCM kutoka Zanzibar.
Wastara alifunga ndoa hiyo usiku wa Alhamisi na Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis ikiwa ni ndoa ya kushtukiza kwani hakuna hata msanii mmoja aliyekuwa anafahamu lolote kuhusu shughuli hiyo.
“Kila jambo linapotokea tunapaswa kushukuru, yote ninayapokea kuna wakati wa furaha, kuna wakati wa majonzi, changamoto zinapotokea pia ni kumuomba Mungu nashukuru Mungu kanipa mume halali maisha yanaendelea,” alifunguka Wastara baada ya ndoa yake hiyo ya ghafla.
Tukio hilo la aina yake lilifanyika nyumbani kwa msanii huyo Tabata Barakuda jijini Dar es Salaam, huku wengi wa marafiki na watu wake wa karibu walikuwa wakidhani angeolewa na mpenzi wake wa siku nyingi Bond bin Sinan. Kabla ya ndoa hii Wastara alikuwa mke wa marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’.