Nandy aachia video yake ya kwanza ya Gospel

Monday April 05 2021
Nandy pc
By Nasra Abdallah

Msanii wa muziki wa Bongofleva,Faustina Charles, maarufu Nandy ameachia kwa mara ya kwanza video ya wimbo wake wa Injili.


Wimbo huo unaoitwa ‘Wanibariki’, ameuachia leo Jumatatu Aprili 5,2021,  katika youtube yake, ambapo mpaka sasa umeshatazamwa na watu zaidi ya 100,000.


Machi mwaka huu, msanii huyo aliyefikisha watazamaji milioni moja kwenye mtandao wa Youtube, alitekeleza ahadi yake ya kuachia EP ya nyimbo za Injili, kama ambavyo aliwahi kuwaahidi  mashabiki zake huko nyuma.


EP hiyo ina jumla ya nyimbo tano,ukiachilia mbali Wanibariki, Ipo Umenifaa,Nipo Naye, Asante na Noel ya Kwanza.
Wanibariki ndio utakuwa wimbo wa kwanza kuachiwa video yake katika EP hiyo.


Nandy aliyeanza kuvuma miaka minne iliyopita na kibao chake cha Nagusagusa, amekuwa moto wa kuotea mbali na kuwa moja ya wasanii wa kike wanaofanya vizuri kwa sasa.


Vibao kama Kivuruge, Ninogeshe,Wasikudanganye, Na Nusu vilizidi kumuweka kwenye ramani nzuri ya soko la muziki na kujikuta akipata tuzo mbalimbali za nje ya nchi na kufanya kazi na wasanii wakubwa akiwemo Koffi Olomide wa DRC Congo, Joe Boy wa nchini Nigeria, Saut Soul na Willy Paul wa Kenya.

Advertisement
Advertisement