Nahreel awatolea uvivu wazushi wote

Muktasari:
- Katikati ya wiki iliyopita, kuna picha ya Nahreel ilitupiwa mtandaoni akiwa katika sherehe ya harusi ya Jux & Priscilla, ambayo iliwaibuka wasiopitwa na mambo walioanza kuijadili na kusema afya yake imekuwa mgogoro na wengine wakajiuliza amepatwa na nini.
MTAYARISHAJI na mwimbaji wa kundi la Navy Kenzo, Nahreel, amewatolea uvivu wazushi wote wanaomnanga kwamba muonekane alionao kwa sasa umechangiwa na kuwa na afya mgogoro.
Katikati ya wiki iliyopita, kuna picha ya Nahreel ilitupiwa mtandaoni akiwa katika sherehe ya harusi ya Jux & Priscilla, ambayo iliwaibuka wasiopitwa na mambo walioanza kuijadili na kusema afya yake imekuwa mgogoro na wengine wakajiuliza amepatwa na nini.
Hata hivyo, Nahreel ameliambia Mwanaspoti, angekuwa na afya mgogoro asingeweza kuendelea na harakati zake kumuingizia kipato.
“Acha watu waseme, sasa mimi lini niliwahi kuwa mnene? Nimeona sana ninavyojadiliwa. Nimeambiwa eti nimekuwa na afya mgogoro na kila mmoja anaongea lake, hivi mwenye afya mgogoro angeweza kutembea sehemu mbalimbali au kujitafutia pesa? Tatizo watu hawabadiliki wanapenda kuishi na historia ya mambo ya zamani, halafu kingine watu inabidi wajue kuna kukua sio kila siku utabakia palepale na sura ile ile,” amesema Nahreel.
Mkali huyo aliongeza kwa kuhoji kuwa mzee ni dhambi? “Sijitetei ila kama picha niliyopigwa imetoka na muonekano ule je, uzee dhambi? Watu wana maneno sana.”
Aidha, Nahreel amezungumzia madai ya watu kuwa huwa hawa hawahudhurii kwenye matukio ya kijamii ya wasanii wenzao ambapo amesema wakialikwa wataalikika na sio kwenda sehemu kama hawajaalikwa.
“Hiyo ishu pia huwa tunaiona mitandaoni kuwa hatushiriki kwenye sherehe za watu, leo tupo wapi hapa? Tupo katika sherehe ya Jux, hivyo sisi tunatokeaga sherehe ambayo tunatakiwa uwepo wetu na ni muhimu na sio kujipeleka mbele hata kama hatujaalikwa,” alisema Nahreel.