MZEE WA UPUPU: Mondi hakuona alichokiona Puffy Daddy

VIDEO ya wimbo wa Mtasubiri sana wa Diamond Platinumz na Zuchu imesimamishwa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuchezwa kwenye vyombo vya utangazaji kutokana na maudhui yake kuleta tafsiri yenye ukakasi kidini.

Kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, TCRA imechukua hatua hiyo kulinda maadili ya kidini hasa kutokana na kipande kinachomuonyesha Zuchu akiwa kanisani akiimba kwaya kisha kupokea simu kutoka kwa mpenzi wake na kuondoka kwenda kudumisha penzi.

Kanisani ni sehemu takatifu, kuonyesha mtu anaacha shughuli za kanisani na kufuata mapenzi ni kudhalilisha utukufu wa kiroho kwa ajili ya mambo ya kidunia...siyo sawa hata kidogo.

Na ilipaswa Diamond Platinumz mwenyewe alitambue hilo hata kabla video haijatoka. Hata kama muongozaji wa video hiyo alikuwa na sababu ya msingi kuweka kipande kile.

Mkasa kama huu ulitokea Marekani mwaka 1999 wakati wa uzinduzi wa video ya wimbo wa Hate Me Now wa Nastradamas Escobar maarufu kama Nas alioshirikiana na Puffy Daddy, kabla haya P. Diddy.

Wimbo huo ambao ulikuwa jiwe kwa wakosoaji wake na vyombo vya habari ulikuwa na kipande kikimuonyesha Nas mwenyewe na mshikaji wake Puffy Daddy wakisubuliwa msalabani kama Yesu Kristo.

Video hiyo ilizinduliwa Aprili 15, 1999, kupitia kipindi cha Total Request Live cha kituo cha luninga cha MTV.

Ikiwa ndani ya albamu ya I Am, video ya Hate Me Now iliongozwa na mwongozaji mashuhuri wa wakati huo, Hype Williams.

Baada ya kuzinduliwa ikachochea ukosoaji kutoka kwa wachambuzi wa muziki na vyombo vya habari kuliko hata ilivyokuwa kabla.

Japo serikali ya Marekani haikuupiga marufuku wimbo huu, lakini jamii ilipaza sauti kubwa kuukosoa.

Baadaye ikabainika kwamba kumbe hata kabla video haijatoka Puffy Daddy alipata wazo la kuondoa kile kipande cha msalaba na akawaambia watengenezaji wakiondoe kabla ya kuitoa video hiyo.

Lakini wao hawakuondoa na baada ya kuzinduliwa kwenye TRL ikiwa na kile kipande cha msalabani Puffy Daddy alimfuata mkurugenzi wa kampuni iliyotengeneza video hiyo, Steve Stoute, na kumshambulia vibaya.

Akiwa na mabaunsa wake, Daddy alikwenda ofisini kwa Stoute na kumlalamikia kwanini alipuuza maombi yao kuondoa kile kipande, maneno yakapandiliana na ndipo Stoute akachezea kichapo kikali kupitiliza.

Maelezo haya alikuja kuyatoa Steve Stoute mwenyewe akihojiwa na MTV, akasema yeye ndiye alikosea kwenye utata wa video ile kwani Puffy Daddy aliwaomba wakiondoe kile kipande na walikubali lakini baadaye waliamua kukiacha wakiamini hakikuwa na tatizo.

Akasema Puffy Daddy alikasirika kiasi cha kutaka kumuua kwa kupuuza maombi yao.

Nas alitunga wimbo ule kuwalaumu wakosoaji wake ambao hawakuwa wakiona hata jema moja alilokuwa anafanya.

Kwa mawazo ya mwongozaji, walichokuwa wanafanya wakosoaji ni sawa na kumsulubu Nas, hivyo akajenga picha ya Yesu msalabani.

Lakini baadaye Puffy Daddy akaona kwamba hiyo itawapa wakosoaji cha kusema zaidi, hivyo akaomba kitolewe, ila watengenezaji hawakutoa...ndiyo kisa cha ule ugomvi.

Hii ndiyo akili ambayo Diamond alipaswa kuya nayo.

Baada ya kuwa amehusika kwenye matukio mengi yenye utata ikiwemo kufungiwa nyimbo zake nyingi, Diamond Platinumz alipaswa kubaini mapema utata ambao ungeweza kuletwa na video yake hiyo hata kama mwongozaji wake alikuwa na picha anataka kuitengeneza.

Lakini Diamond Platinumz siyo Puffy Daddy, hakuona hadi TCRA walipomsaidia.