MZEE WA UPUPU: Diamond, Zuchu picha lilianzia kwa dada mtangazaji

DIAMOND Platinumz na Zuchu wameudhihirishia ulimwengu wa mashabiki wao na muziki kwa ujumla kwamba wanaishi kwenye sayari ya ndoto zao, sayari mapenzi!

Hii ni baada ya tetesi nyingi na za muda mrefu ambazo zilianza kama ‘kiki’, lakini kwa mujibu wa video walizozisambaza hivi karibuni ni rasmi kwamba LITAWACHOMA, CHECHE NA MTASUBIRI SANA ulikuwa ujumbe rasmi kwa wenye chuki dhidi yao.

Maisha yanaenda kasi sana. Zuchu alitambulishwa kwenye lebo ya Wasafi mwaka 2017, sasa yeye ndiyo anashilikilia funguo ya lebo... Yaani kutoka kuwa mpangaji hadi kuwa mwenye nyumba ndani ya miaka mitano tu...kasi sana!


ILIKOANZIA

Ni rahisi mtu kudhani au kuamini kwamba ilikuwa ghafla bin vu tu, wawili hawa wakaaingia mapenzini...lakini kuna stori kubwa sana nyuma ya hili...kubwa sana!

Diamond alikuwa na uhusiano na mmoja wa watangazaji wa Wasafi Media, kisirisiri sana. Wakati Diamond yupo na wanawake wengine kama Zari, Hamisa na hata Tanasha, yule mtangazaji alikuwa na uhusiano wa siri.

Baada ya wanamama hawa kuachana na Diamond, ikaonekana sasa zamu ya dada mtangazaji kujiachia imefika...na kweli mambo yalishaanza taratibu.

Watu wa karibu na familia ya Wasafi walikuwa wameshagundua na hata mtangazaji mmoja mwanaume wa kipindi cha michezo aliingia mgogoro na Diamond kwa ajili ya huyo dada.

Siyo kwamba mtangazaji huyo alikuwa na uhusiano na dada, hapana. Walikuwa tu na ukaribu wa kishkaji tangu Diamond akificha uhusiano wake na dada mtangazaji.

Sasa alipoanza kujiachia na kuongeza muda wa kuwa naye, ndiyo akagundua kwamba kumbe dada mtangazaji yupo karibu na kaka mtangazaji...akakonda moyo.

Kaka mtangazaji tangu ajiunge na Wasafi Media, alikuwa karibu sana na bosi, na hata taarifa ya maendeleo ya kipindi cha michezo aliziulizia kwake, siyo kwa mkuu wa idara ya michezo.

Lakini alipogundua ukaribu wake na dada mtangazaji, akamfungia vioo jumla. Siku moja Diamond akiwa na dada mtangazaji alikuwa ‘location’ wakirekodi kitu na wasanii wake, lakini Zuchu hakutokea.

Hii ilimkera sana Diamond na kuona Zuchu ameanza kudharau kazi. Inadaiwa alisema maneno mengi. Kumbe dada mtangazaji na Zuchu walikuwa marafiki wakubwa sana, na marafiki wa Kiswahili hawanyimani umbea. Dada mtangazaji akamfikishia salamu zote Zuchu, kwamba umesemwa sana leo.

Zuchu akaumia sana moyoni, kwanini bosi aniseme huko badala ya kunitafuta ajue nini kimenikuta. Alipokutana naye akamlalamikia sana. Diamond akashangaa, amejuaje kama tulimjadili kule. Zuchu akasema ameambiwa na dada mtangazaji.

Diamond akamrudia dada mtangazaji na kumkemea kwa umbea wa kuchukua maneno ya jandoni na kuyapeleka uraiani. Akamuuliza unadhani yeye atakwambia mambo yako akiyasikia? Dada akiamini kwamba Zuchu ni ‘bestie’ yake, akajibu ‘kwanini asiniambie’?

Hii haikumfurahisha Diamond. Kwa hiyo akapanga kumtafuta Zuchu na kutoka naye angalau mara moja ili aone kama dada mtangazaji atapata taarifa. Siku zikapita na Diamond akaenda Uturuki kikazi na Zuchu akaenda Afrika Kusini kikazi.

Diamond aliporudi akabadilisha nguo na begi tu, akaunga Afrika Kusini. Hukohuko ndiko mambo yalikoanzia. Waliporudi nyumbani, Diamond akasubiri kama atasikia lolote kutoka kwa dada mtangazaji...kimya.

Akaanza yeye kuuliza, ‘Zuchu amekwambia tulifanya nini Afrika Kusini?’ Dada mtangazaji ‘akalowa’. Diamond hakupanga kuweka kambi kwa Zuchu, lakini akajikuta anarudia na kurudia na matokeo yake ni hizi video za hivi karibuni.

Dada mtangazaji alidhani Zuchu ni ‘bestie’ yake wa kumpelekea umbea, kumbe kampelekea penzi. Lakini hata hivyo, menejimenti ya Diamond hailioni penzi hili kama lina afya kwa kazi yao. Mapenzi ni mazuri bahari inapokuwa shwari, lakini ikitokea dhoruba chombo husambaratika na kufupisha safari. Ndicho wanachokiogopa.

Lady Jaydee na Garnder Habash walikuwa mfano wa vijana mashuhuri kwenye uhusiano. Lakini anguko la penzi lao likasababisha anguko kubwa la kazi zao. Hadi kurudi kusimama upya, jasho la mgongoni liliwatoka.

Hiki ndicho menejimenti inachokiogopa, lakini ndiyo hivyo tena. Diamond kwa Zuchu hasikii na Zuchu kwa Diamond haoni. Yote yalianzia kwenye umbea wa dada mtangazaji.