MUSIC FACTS: Sauti ya Nandy ndani ya Wasafi Records!

AMETOA albamu moja, The African Princess (2018), EP tatu, Wanibariki (2021), Taste (2021) na Maturity (2022), amefungua rekodi lebo yake, The African Princess, amefanya kazi na Epic Records, Coke Studio Africa na ameshinda tuzo nyingi za ndani na kimataifa.
Takribani miaka saba tangu atoke kimuziki, Nandy amekuwa kwenye kilele cha mafaniko ya kazi yake na miongoni mwa wasanii wa kike wenye ushawishi katika muziki, mitindo, biashara na familia. Huyu ndiye Nandy;.
1. Msanii wa Hip Hop Bongo, Baghdad ndiye alikuwa Meneja wa Nandy hadi anaenda Nigeria kwenye shindano la karaoke Afrika, Tecno Own The Stage ambapo aliibuka mshindi wa pili na kupata nafasi ya kunolewa na lebo ya Chocolate City.
2. Nandy ndiye msanii pekee wa kike Bongo mwenye cheti kutoka kwa waandaji wa tuzo za Grammy, Recording Academy baada ya albamu 'Pamoja' yake Etana kutoka Jamaica kushinda Grammy 2021 kama Albamu Bora ya Reggae, Nandy alishirikishwa kwenye wimbo, Melanin.
Tuzo za Grammy zilianza kutolewa Mei 4, 1959, wakati huo zikifahamika kama Gramophone Awards, huku lengo lake kuu ni kutambua mafanikio katika tasnia ya muziki.
3. Nandy na mumewe, Billnass ambaye wametoa ngoma nne pamoja (Bugana, Do Me, Party na Bye) kwa mara ya kwanza walikutana Chuo cha Biashara (CBE) Dar es Salaam ambapo alikuwa wanasoma. Hata hivyo, uhusiano wao ulianza rasmi katika tamasha la Fiesta mkoani Mbeya.
4. Dully Sykes ndiye alimshawishi Inspector Haroun kumshirikisha Nandy katika wimbo wake 'Sharubu za Babu', wakati huo Nandy alikuwa anafanya kazi studio kwa Dully na huo ukawa mwanzo wa mafanikio yake kimuziki.
Utakumbuka Nandy ameshinda tuzo zaidi ya 10, ametoa albamu moja, EP tatu, ana tamasha lake, Nandy Festival na ni msanii wa pili wa kike Afrika Mashariki aliyetazamwa zaidi YouTube kwa muda wote.
5. Zawadi ya kwanza kubwa ya kwanza ambayo Nandy amewahi kupewa na mumewe, Billnass kwenye Birthday yake ni cheni na hereni ambazo zina thamani ya Sh8. 2 milioni, huku Nandy akimpatia Billnass zawadi ya gari aina ya Range Rover.
6. Tuzo ya kwanza Nandy kushinda katika muziki ni kutoka All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki, na kwa ujumla ameshinda tuzo zaidi ya tano za kimataifa, na tuzo tano za ndani ambazo ni Tanzania Music Awards (TMA) na The Orange Awards.
7. Hadi kukamilika kolabo ya Nandy na Koffi Olomide kutokea DR Congo ilimgharimu zaidi ya Sh40 milioni, na Billnass ndiye alienda kwa Rais wa Yanga SC, Injinia Hersi Said kuazima gari lenye hadhi ya Koffi kwa ajili ya kumchukua kutoka Airport.
8. Katika wimbo wa Christian Bella, Ollah akimshirikisha Khalighraph Jones kutokea nchini Kenya, kuna sauti za Nandy na Ruby mwishoni ambazo walizirekodi kwa nyakati tofauti, walikuja kugundua wamewekwa pamoja baada ya wimbo huo kutoka.
9. Nandy ndiye alifanya 'Jingle' ya Wasafi Records, yaani kile kisauti cha kike kinachosikika mwanzoni mwa nyimbo zinazotoka chini ya Wasafi Records, ni cha Nandy. Alirekodi 'Jingle' hiyo kipindi bado hajatoka kimuziki wala hajaanza kufanya kazi chini ya Tanzania House of Talent (THT).
10. Siku ya kwanza Nandy na Marioo kukutana ili kumwandika wimbo ilikuwa ni studio, alikuwepo Prodyuza Lollipop (Goodluck Gozbert) ambaye ameandika nyimbo kibao zilizofanya vizuri kama Moyo Mashine ya Ben Pol, Basi Nenda na Mo Music n.k.
Uwepo wa Lollipop studio uliondoka ujasiri wa Marioo kunadika, hivyo aliomba kupewa mdundo aende nao nyumbani kuandika, alipomaliza kesho yake na kumtumia Nandy alikubali uwezo wake. Utakumbuka Marioo ndiye ameandika wimbo wa Nandy, Wasikunganye.