MUSIC FACTS - Baba Levo: Mgambo aliyekimbia jeshi kisa muziki

UKIACHANA na muziki wake, wengi wanampenda kutokana na ucheshi wake. Kila alipo lazima genge lichangamke ili raia waongeze siku za kuishi. Chapa yake imejengeka katika eneo hilo na ndipo anapata dili nyingi.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kuwa hapo alipo sasa. Kuna milima na mabonde mafupi na marefu, furaha na huzuni ambavyo vimemfanya kuwa Baba Levo huyu wa leo. Je yeye ni nani na ametoka wapi? Bongo Music Facts inakuza.


1. Baba Levo alianza muziki mwaka 2001 Dodoma alipojiunga na kundi la Original Black Dangerous (OBD), lakini kilichompeleka mkoani humo sio muziki, bali kujiunga na Jeshi.


2. Aliporudi Kigoma aliendelea kujiita OBD ila akiwa na maana ya Original Black Disease. Siku moja akiwa kanisani mchungaji wake alimuuliza nini maana ya jina lake, jibu lake lilikuwa ni Okoka Bila Dukuduku (OBD).


3. Mwaka 2002 Baba Levo alianzisha kundi la K Town People lenye wasanii wawili na kurekodi wimbo wao wa kwanza kwa Prodyuza Kid Bwoy mkoani Mwanza na baadaye Bongo Records kwa P Funk Majani.


4. Baada ya kupata mtoto wake wa kwanza mwaka 2005, Revocatus, ndipo alianza kujiita Baba Levo na kuachana na jina la OBD. jina “Levo” limetoholewa kutoka Revocatus ambalo ni jina la baba yake mzazi.


5. Mwaka 2003 ndipo Baba Levo alirekodi wimbo wake wa kwanza nje ya kundi (solo artist) ambao unaitwa “Clara” ni kwa Prodyuza Enrico Figueiro toka Sound Crafters. Mwaka 2004 akarekodi wimbo wa pili “Mapadri na Mashekhe” kwenye studio ya Mr. Ebbo mkoani Tanga, Motika Records.


6. Mwaka 2007 Baba Levo ndipo alipojiunga na kundi la TMK Wanaume Halisi ambalo lilikuwa linaongozwa na Juma Nature, lengo lilikuwa ni kupambana na TMK Wanaume Family lililokuwa chini ya Chege kwa wakati huo.


7. Prodyuza P Funk Majani ndiye aliyemkabidhi Baba Levo kwa Juma Nature, ni wakati wanaelekea kwenye shoo ya ‘Mkali Nani’ kati ya TMK Wanaume Halisi na TMK Wanaume Family ambao walikuwa wanafanya vizuri na wimbo wao - Dar Mpaka Moro.


8. Wakati kundi la K Town People limekuja Dar es Salaam kurekodi wimbo wao wa pili kwa P Funk, Baba Levo ndipo alikutana na Diamond Platnumz kwa mara ya kwanza na kumueleza naye ni wa Kigoma. Kipindi hicho Chibu bado kijana mdogo sana ila sasa Chibu ndiye bosi wa Baba Levo.


9. Baba Levo anaamini Alikiba na Diamond ndio chanzo cha kuvunjika kundi la Kigoma All Stars lililotamba na ngoma kama Leka Dutigite - ni baada ya kuona wao ndio wanawabeba wasanii wengine zaidi.


10. Mwaka 2000 alitaka kujiunga na Jeshi kutokana elimu yake ni darasa la saba akatakiwa kuanzia Mgambo kisha JKT na kuendelea mbele. Basi akaingia Mgambo miezi mitatu, alipomaliza akaonekana bado hajaiva kuingia JKT hivyo akarudia Mgambo tena miezi mitatu. Raundi hii alifu zu kuing- ia JKT ila hakuenda baada ya kuona ni shughuli yake sio ya kitoto ndipo akazamia kwenye muziki.