Mondi na Kiba wajao

Muktasari:

DIAMOND na Alikiba ni moja wa upinzani uliodumu kwa muda mrefu zaidi katika tasnia ya muziki nchini. Vuguvugu la upinzani wao lilianza zaidi ya miaka 10 iliyopita na mpaka kufikia sasa limebadilika kuwa ‘bifu’ lisilokuwa na dalili ya kuisha hivi karibuni.

DIAMOND na Alikiba ni moja wa upinzani uliodumu kwa muda mrefu zaidi katika tasnia ya muziki nchini. Vuguvugu la upinzani wao lilianza zaidi ya miaka 10 iliyopita na mpaka kufikia sasa limebadilika kuwa ‘bifu’ lisilokuwa na dalili ya kuisha hivi karibuni.

Hata hivyo, siku za hivi karibuni wameibuka wasanii wengine wanaoonyesha kuwa na upinzani unaoelekea kuwa bifu kiasi kwamba kama mambo yataendelea hivi hivi wasanii hao wanaweza kuwa ndiyo Diamond na Alikiba upande wa upinzani na bifu kwa miaka kadhaa ijayo.


ZUCHU vs NANDY

Upinzani wao upo lakini unalazimishwa zaidi na mashabiki kuliko wao wenyewe. Upinzani huu ulikuja baada ya Nandy kutawala gemu kwa muda mrefu kama msanii wa kike nambari moja Tanzania, lakini ilipofika Aprili mwaka jana taji hilo lilianza kukosa nguvu taratibu baada Zuchu kuingia mjini.

Zuchu alivunja rekodi nyingi za Nandy ndani ya muda mfupi sana ikiwemo kumzidi wafuasi kwenye mitandao ya kijamii kama vile Youtube pamoja na kupata nafasi kwenye majukwaa ya kimataifa kama vile tuzo na matamasha na hata mtaani sasa imekuwa sio Nandy pekee anayezungumziwa, bali ni Nandy na Zuchu.

Sasa kwa sababu wote ni wakali na wana dalili zote za kudumu kwenye gemu kwa muda mrefu zaidi huku kukiwa hakuna ukaribu baina yao kama ilivyo kwa Nandy na wasanii wengine wa kike, huenda baada ya miaka kadhaa ijayo wakawa ndiyo Diamond na Alikiba wa kike.


YOUNG LUNYA vs CONBOI

Washikaji walikuwa memba wa kundi moja la Hip Hop linaloitwa OMG, kundi lililokuwa likiundwa na wasanii watatu, Young Lunya, Salmin Swaggz na Conboi na walitamba na ngoma kama vile Umbea waliyomshirikisha Baraka The Prince.

Mwaka 2019 waliamua kuachana na habari za kundi na kila mmoja akaanza kufanya muziki kivyake huku wakiahidi mashabiki zao kwamba wataendelea kushirikana kwani hawakuvunja kundi kwa ubaya bali walitaka kukua kisanaa; lakini matokeo yake utengano wao ukazalisha vuguvugu la kwamba Young Lunya na Salmin Swaggz wanamtenga Conboi na kufanya mambo yao kimya kimya.

Hata hivyo kwa mujibu wa Young Lunya ambaye anahit na wimbo wake mpya wa Mbuzi anasema Conboi ndiye anayejitenga nao huku Conboi ambaye mkwaju wake maarufu zaidi unaitwa Till I Die akigoma kabisa kuongelea sakata hilo.

Kwa walipofikia sasa bifu lao limekuwa zito kiasi kwamba kila wimbo wa kujitamba anaotoa mmoja wao mashabiki wanatafsiri kama ni dongo kwa mwingine.

Sasa kwa sababu wote ni wakali wa kunata na biti na uandishi na pia wana vigezo vyote vya kudumu kwenye gemu kwa muda mrefu, huenda miaka kadhaa ijayo tukaona upinzani na bifu lao limewageuza kuwa Diamond na Alikiba na Hip Hop.


HARMONIZE vs RAYVANNY

Timbwili lao lilianza majuzi yalipotokea mambo ya Paula wa Kajala, ni stori ambayo wote tunaifahamu au sio?

Mpaka sekeseke linazimika kila kitu kilikuwa wazi kwamba wawili hao walikuwa na vinyongo ikiwa ni pamoja na kutupiana vijembe kupitia nyimbo pamoja kuitana majina yasiyopendeza kama vile panya na kibonge pia kutupiana tuhuma za kusambaziana picha za utupu tuhuma ambazo zilisababisha mpaka wakapelekana polisi na kufunguliana kesi za kudhalilishana.

Hii inatoa ishara kwamba kama Harmonize na Rayvanny wataendelea kuwepo kwenye gemu kwa miaka kadhaa mbele uadui wao utabadilika kuwa bifu kisha upinzani mzito ambao labda utapelekea wawe Diamond na Alikiba toleo la pili.


H BABA vs BABA LEVO

Ni wanamuziki ambao wako kitambo kwenye gemu na labda hakuna aliyefikiria kama labda siku moja watakuwa wapinzani kutokana na utofauti wa muziki waliokuwa wakiimba zamani. Hata hivyo kwa sasa wamejikuta wamekuwa wapinzani kwenye sekta ya uchawa, huku Baba Levo akiwa ni chawa nguli wa Diamond wakati H Baba akiwa chawa mkuu wa Harmonize.

Sasa kwa sababu wawili hawa wote ni wanamuziki kuna uwezekano mkubwa wa ushindani wao ukahamia kwenye kutupiana madongo kwa njia ya nyimbo na kupata kiki ambayo itawarudisha mjini na kuwafanya kuwa sio chawa tu, bali wapinzani kama mabosi zao.