MKOJANI#2 : Ustaa umenibeba, ila sina mkwanja

KATIKA toleo lililopita tuliona maisha ya Mkojani kabla hajawa maarufu. Ambapo alifuchua alikuwa ni mchekeshaji wa mtaani wa kuweka tumbo kubwa na kujipaka masizi usoni. Pia alielezea kuwa alikuwa kwenye Ze Komedi ya kwanza ya kina Joti na Mpoki kabla hawajamtoa kwenye kundi hilo bila kumpatia sababu za msingi.

Leo anaongelea maisha yake ya umaarufu yalipoanza.


KILICHOMPA

USUPASTAA

Mkojani anakwambia licha ya kwamba alianza kuigiza muda mrefu, tangu mwaka 2008 alipotoa filamu yake ya kuitwa Kigodoro, lakini umaarufu aliupata miaka ya hivi karibuni baada ya kuigiza kama Mkojani.

“Nilikuwa naigiza kwa jina la Kipupwe, lakini watu wengi walikuwa wananichukulia ni msanii wa kawaida tu. Nakwambia nilikuwa hata nikipanda daladala watu wala hawana taimu na mimi,” anasema na kuongeza.

“Lakini sasa hivi nikipita kwenye shule ujue masomo lazima yasimame, watu wananijua, wananipenda na wananikimbilia kila ninapopita. Ni ngumu hata kupanda daladala kwa sasa.”


ETI YEYE NI MASKINI

Kutokana na umaarufu wake, ukipita kwenye soko la kuuza DVD za filamu za Kitanzania pale Kariakoo utakuta mabango makubwa ya filamu zinazofanya vizuri ni zenye sura ya Mkojani. Pia runinga ndani ya mabasi ya mikoani hayaachi kucheza filamu zake na ndizo zinazotawala, bila kusahahu kwa sasa yeye ni kati ya wasanii wachache wa vichekesho wanaotrend kwenye mitandao ya kijamii, Youtube, Instagram na hata kwenye status za Whatsapp vituko vyake vimezagaa.

Kwa sababu hiyo unaweza ukadhani Mkojani anaingiza mkwanja mrefu kinoma kupitia kazi zake hizo, lakini kumbe mambo ni tofauti, na hapa Mkojani anaweka wazi kuwa yeye ni msanii masikini.

“Mimi ni msanii maarufu sana lakini maskini, si mnaona hata hapa mlipokuja kunihoji, kibarazani, ningekuwa tajiri mngenikuta kwenye ofisi yangu nzuri tukafanya intavyuu huku tunakula kiyoyozi.” anasema na kuongeza.

“Sikufuru, nashukuru Mungu sana kwa hiki nilichonacho, lakini ninachomaanisha ni kwamba wasanii wa Tanzania hatupati haki zetu inavyotakiwa. Kwa mfano, hizo kazi zinachezwa kwenye mabasi mimi siingizi hata senti 10 zaidi ya umaafuru tu. Na sina pa kwenda kudai, naanzia wapi?” Anaweka nukta.


SANAA IMEMPA NINI

Swali la umaarufu wake kupitia sanaa umempa nini anachoweza kujivunia mbele za watu lilikuwa ni la muhimu sana, na Mkojani hakulikwepa.

Anajibu kuwa kupitia sanaa yake anaendesha maisha yake vizuri tofauti na ilivyokuwa mwanzo lakini zaidi anaeleza kuwa kwa sasa yeye ndiye tegemezi kwenye familia yao nzima.

“Kwa sasa mimi ndiyo tegemezi, naheshimika kwenye familia na ni kwa sababu ya ninachokipata kupitia sanaa yangu. Siku hizi hata ukitokea msiba watu wanaweza wasizike mpaka mimi niwepo. Maana yake familia zetu hizi kama huna hela mkiwa kwenye kikao watu wanaulizwa unakunywa nini, lakini wewe kapuku unapewa soda yoyote tu.” anasema.


NJE YA KAMERA

Licha ya kwamba akiwa mbele ya kamera anajisifu kuwa ni mpenda mademu na ndiyo mada zinazomfanya atrend kwenye kazi zake, lakini hali ni tofauti sana nyuma ya pazia na hiyo ni moja ya vitu ambavyo anadai kuwa anajivunia sana.

Mkojani anaeleza kuwa nyuma ya kamera yeye ni mtu mwenye mapenzi makubwa sana kwa mchumba wake ambaye anayeitwa Joyce ambaye pia wanatarajia kuwa mke na mume hivi karibuni na ndiyo maana hata amekuwa huru kumposti kwenye mitandao ya kijamii.

“Mimi ni msanii tu, ninavyoigiza kuwa napenda wanawake sio kwa sababu napenda wanawake bali ni kwa sababu watu wa aina hiyo wako wengi mtaani kwahiyo ndiyo tunaonyesha jamii kwa namna ya kufundisha namna kupenda wanawake kunavyoweza kusababisha matatizo,” anasema.

Pia anadai kuwa hata watazamaji wanapenda zaidi kutazama mada hizo kwenye filamu ndiyo maana nao wanazitengeneza sana.

“Kwa utafiti wetu inaonyesha ninapoigiza vichekesho vya kupenda wanawake watu wanapenda zaidi kuliko ninapoigiza vingine, ndiyo maana unaona tufanya sana hivyo kwa sababu sisi ni wafanyabiashara, tunawapa watu kitu wanapenda kutazama.”


INBOX YAKE IMEJAA MADEMU

Kutokana na ustaa wake Mkojani anafichua kuwa DM yake ya Instagram imejaa meseji za wanawake wakimtongoza.

“Natongozwa sana, natakwa sana, naambiwa mambo mazito mazito huko inbox na wanawake lakini kwa sababu najiheshimu na nina mpenzi ambaye nampenda wala sizitazamani mara mbili.” anasema.

Na alipoulizwa hali anayokuwa nayo mpenzi wake akiziona hizo meseji kutoka kwa mashabiki wanaomtaka kimapenzi Mkojani anapasuka kuwa yeye na mke wake hawana kawaida ya kushikiana simu.

“Mke wangu ataziona wapi hizo meseji? Mimi na mke wangu tumewekeana utaratibu wa hakuna kushika simu ya mwenzake. Kwahiyo hata wewe kama una mtumia DM mke wangu wala sitaziona.” anasema.

Hivi ni kweli ana ugomvi na Tin White na anazungumziaje tuhuma za kusafisha nyota kwa Kalumanzira? Usikonde!


Itaendelea kesho