Mke wa Fella afafanua alichokiandika mumewe kutelekezwa
Muktasari:
- Sweet Fella amezungumza na Mwanaspoti na kusema aliamua kuandika kwenye akaunti yake ya Instagram kuhusu Mkubwa Fella kutengwa na watu wake wa karibu kwa kushindwa kumjulia kwa sababu kuna baadhi ya watu wanajua anasaidiwa pesa na msanii Diamond ndio maana watu wengine wanashindwa kuja kumuona, kumbe haipo hivyo anapambana mwenyewe.
WAKATI meneja wa msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul 'Diamond Platnumz', Said Fella 'Mkubwa Fella' akiendelea kupambania afya yake kitandani, mke wa meneja huyo, Sweet Fella ametoa ufafanuzi kuhusu alichokiandika mtandaoni.
Sweet Fella amezungumza na Mwanaspoti na kusema aliamua kuandika kwenye akaunti yake ya Instagram kuhusu Mkubwa Fella kutengwa na watu wake wa karibu kwa kushindwa kumjulia kwa sababu kuna baadhi ya watu wanajua anasaidiwa pesa na msanii Diamond ndio maana watu wengine wanashindwa kuja kumuona, kumbe haipo hivyo anapambana mwenyewe.
"Mimi sijaandika kwenye akaunti yangu ya Instagram ili nipate kulipwa wema wa mume wangu kwa yale mazuri aliyowasaidia au kuwafanyia watu, hii hapana. Mimi nimetoa dukuduku langu watu wajue napambana mwenyewe ili mume wangu apone, maana kipindi yuko mzima kuna simu kibao za watu waliokuwa wananipigia pigia usiku wa manane hadi alfajiri nimuamshe mume wangu wana ishu naye, yaani ilikuwa wakimkosa, mimi ndio nilikuwa napata shida walikuwa wananiambia nimuamshe Mkubwa kuna ishu naye, sasa hivi hizo simu sizioni tena."
Vipi kuhusu Diamond kutoa sapoti?
"Kuhusu Diamond Platnumz kutomsaidia Fella, yaani huwezi kumlazimisha mtu kwamba kwanini husaidii? Kwani yeye mwenyewe hajui kama Fella anaumwa? Si anajua bosi wake meneja wake anaumwa, hata kama ndio alitusaidia tukaenda India tukarudi, lakini asingeishia njiani na kukaa kimya, sasa mimi kama nimetoa dukuduku langu sisaidiwi na mtu maana watu wanaweza kusema napata msaada kwa Diamind ambaye ni tajiri."
Hali ya Fella ikoje kwa sasa?
"Hali ya mume wangu kwasasa hajambo, anaendelea vizuri na mazoezi, maana kwa mwezi anatumia Sh1.2 milioni kwa ajili ya mazoezi na tangu ameanza kuumwa hadi sasa anatimiza mwaka mmoja, mbali na hayo mazoezi kuna kwenda kliniki na kuna dawa za kununua kila wakati ili atumie, na ndio maana nasema napambana mwenyewe, hapa kuna familia inanitegemea yaani kila kitu kinaniangalia mimi, nazidi kumuomba Mungu ampe afya njema mume wangu arudi kama zamani".
Awashukuru Mbosso, Said Kessy, Muddy K
"Kiukweli Kuna watu ambao sitaacha kuwashukuru ambao wamebaki na Mkubwa Fella hadi sasa, na wanatoa sapoti kubwa sana kwake ni shemeji zangu Meneja Said Kessy na Muddy K. Hawa wananisaidia sana na hata juzi wamemletea baiskeli ya kutembelea Mkubwa Fella, sababu bado hajaanza kuchanganya kutembea vizuri. Mbosso amekuwa msaada mkubwa pia."
Alichoandika Instagram
Januari 4, 2026 Sweet Fella, alishusha ujumbe mzito kupitia akaunti yake ya Instagram akielezea masikitiko yake kuhusu mumewe anavyopuuzwa na watu aliowahi kuwasaidia, wakati huu akiwa anaumwa. Aliandika:
"Mume wangu kuugua ni ibada, mimi mke wako nipo pamoja na wewe mpaka dakika za mwisho, ulipo mimi nipo. Leo hii hakuna mtu yeyote anayekuuliza hali, lakini najua mambo yote uliyowafanyia na wanajua ila wanajizima data wote uliowasaidia."
"Pia wanaonisapoti nawatambua, inshallah Mungu atawalipa kwa hicho mnachojitolea Mungu awasaidie. Namuombea mume wangu apone, atakuja kuongea mwenyewe yote."
Mkubwa Fella ni miongoni mwa watu waliowahi kusimamia wasanii wakubwa nchini Tanzania na mchango wake kwenye muziki wa Bongo Fleva ni mkubwa.
Amefanya kazi na kundi la TMK Wanaume lililoundwa na kina Juma Nature, Mheshimiwa Temba, Chegge Chigunda na pia kuasisi kundi la Yamoto Band lililoundwa na Aslay, Mbosso, Beka Flavor na Enock Bella kutoka katika akademi yake ya vipaji vya muziki ya Mkubwa na Wanawe na pia kufanya kazi kama meneja wa Diamond Platnumz hadi sasa.
Mashabiki na wadau sasa wanahimizwa kumkumbuka katika sala na kumtakia nafuu.
TUJIKUMBUSHE
Mwaka jana Machi 4, 2025 Mwanaspoti iliripoti hali ya kiafya ya Fella aliyekuwa akisumbuliwa na presha na kupooza miguu. Wakati huo, Fella amesema afya yake imezidi kuimarika baada ya kutoka kupata matibabu India, ambako huko gharama zote aligharamia Diamond Platnumz.
Ilipofika Mei, 2025 Fella amesema kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa matatizo hayo, alikata tamaa ya kupona, lakini hadi wakati huo amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani anaendelea vizuri.
“Nina furaha kwani kwa sasa naendelea vizuri, hali yangu inaimarika kila siku na nimeanza kufanya mazoezi ya kutembea kila ifikapo jioni.
"Ukweli mimi nimeumwa sana yaani nimeumwa kweli hadi nikawa nimekata tamaa ya kupona, ila namshukuru Mungu sana hadi sasa naweza kuongea na wewe hivi na kutembea vizuri kwa kufanya mzoezi, ilikuwa balaa,” amesema Fella.
Taarifa za kuumwa kwa Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii Januari 2025 kuwa amepoza miguu huku wengi wakituhumu kuwa Diamond alimtelekeza.
Hata hivyo, baada ya kupata taarifa hizo Mwananchi ilimtafuata nyumbani kwake Mbagala kata ya Kilungule, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na baadhi ya ndugu zake ambao walidai hali yake haikuwa nzuri hata kuzungumza na mtu kwa muda mrefu alikuwa anashindwa.
Fella, mbali na mchango wake mkubwa katika muziki pia alikuwa Diwani wa Kata ya Kilungule.