Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lamata akabidhiwa mashindano ya Miss Tanzania

Aliyekuwa mmiliki wa Miss Tanzania, Basilla Mwanukuzi (kulia) akibadilishana mkataba na Mkurugenzi wa kampuni ya Lamata Village,Lamata Leah,jijini Dar es Salaam leo,katikati ni mwakilishi wa BASATA,Abel Ndaga.Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Mwanukuzi kupitia kampuni ya The Look, wamekabidhi rasmi mashindano ya Miss Tanzania kwa kampuni ya Lamata Village chini ya mtayarishaji wa filamu, Lamata Leah, katika hafla uliyofanyika leo Aprili 14, 2026 ndani ya ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Korogwe na msimamizi wa Mashindano ya Miss Tanzania, Basilla Mwanukuzi, amesema wamefanya uamuzi sahihi wa kumkabidhi shindano la kutafuta warembo, Miss Tanzania, Lamata Leah.

Mwanukuzi kupitia kampuni ya The Look, wamekabidhi rasmi mashindano ya Miss Tanzania kwa kampuni ya Lamata Village chini ya mtayarishaji wa filamu, Lamata Leah, katika hafla uliyofanyika leo Aprili 14, 2026 ndani ya ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sanaa, urembo na burudani, ikiwemo warembo wa zamani wa Miss Tanzania, wasanii wa filamu na viongozi wa taasisi za Serikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwanukuzi aliyewahi kuwa Miss Tanzania mwaka 1998, amesema mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza vipaji vya mabinti na kuitangaza Tanzania kimataifa.

“Urembo ni heshima, na kupitia Miss Tanzania tumeweza kutoa warembo waliotuwakilisha vyema nje ya nchi,” amesema Mwanukuzi, akiwataja baadhi ya wanamitindo waliotikisa kimataifa akiwemo Miriam Odemba, Genevive Mpangala, Diana Vev na Elizabeth Makune.

Ameongeza kuwa, tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo na marehemu Hashim Lundenga mwaka 1994, yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwawezesha mabinti.

Mwanukuzi amesisitiza kuwa, jukumu la kuendesha mashindano hayo sasa linaachwa mikononi mwa wamiliki wapya ambao ni Lamata Village, huku akibainisha kwamba kulikuwa na uchambuzi wa kabla ya kufikia hatua ya kukabidhi.

“Tulihitaji kujiridhisha nani anaweza kuibeba dhamana hii. Miss Tanzania ni jukwaa la taifa, linahitaji sapoti ya kila mmoja,” amesema Mwanukuzi.

Akizungumza kwa niaba ya Lamata Village, Grace Mgaya amesema wanatambua uzito wa jukumu walilokabidhiwa na kuahidi kushirikiana na wadau kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa viwango vya juu.

“Huwezi kulitaja jina la Lamata bila kutaja ubora. Tuna hamu kubwa ya kuona Miss Tanzania inarejea kwa nguvu na heshima yake,” amesema Mgaya.

Mtayarishaji wa filamu ya Jua Kali, Leah Lamata, amesema: “Mimi sio mzungumzaji sana lakini nitayathamini, nitayaongoza na kuhakikisha mashindano ya Miss Tanzania yanatoa kilicho bora zaidi.”

Kwa upande wa miss Tanzania mwaka 2019, Elizabeth Makune amesema urembo si sura pekee bali ni sauti na ushawishi.

“Miss Tanzania sio tu sura, bali unafanya nini kwa jamii, tuna imani na Lamata Village kuwa wanaweza kufanya zaidi, nasi tutatoa ushirikiano kuhakikisha jukwaa hili linaendelea kuwajenga mabinti,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Abel Ndaga, amesema mashindano ya Miss Tanzania yamekuwa zaidi ya jukwaa la urembo, yakichangia kuibua viongozi na mabalozi wa taifa.

“Sisi kama baraza tuko bega kwa bega kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa, shindano hili hatuliangalii kwenye dhana ya urembo pekee bali pia umuhimu wake kwa jamii,” amesema Ndaga.


ILIVYOKUWA

Kama unavyojua hekaheka za Lamata na kundi lake, waigizaji wengi walihudhuria makabidhiano hayo. Kwenye suala la kuvaa sasa waigizaji wa kiume wote walivalia mavazi ya rangi nyeusi, wengi walivaa suti baadhi walivaa kawaida lakini wakiwa kwenye 'code' ile ile.

Kwa upande wa wanawake, kila mmoja alipendeza kivyake kwa magauni ya kupendeza lakini Dorah pekee alivaa mavazi ya kiutamaduni.

Hafla hiyo pia ilipambwa na matukio ya burudani, hasa walipojitokeza baadhi ya watu maarufu akiwemo muigizaji Jackline Wolper kupanda jukwaani na kutembea kwa stepu kama mamodo.

Mwingine ni mchekeshaji Gladness Kifaluka aliyewavutia wengi kwa ubunifu wake wa mavazi, akivalia gauni lililotengenezwa kwa mifuko meusi.

Kifaluka alipigiwa shangwe baada ya kuingia ukumbini kutokana na utofauti aliouonesha.

Tukio lililozua gumzo zaidi lilikuwa la Miriam Odemba ambaye awali alisita kupanda jukwaani alipoitwa na MC, akieleza kuwa kama mtaalamu wa uanamitindo (pro model) haruhusiwi kufanya catwalk wakati kundi la watu wapo kwenye jukwaa hilo. Hata hivyo, baadaye alipanda jukwaani akiwa peke yake.