Mdundiko: Filamu ya Bongo iliyoonyesha njia

Jackson Kabigiri akiongoza fIlmau ya Mdundiko
Muktasari:
- Filamu ya Mdundiko inaweza kuwa ndiyo mkombozi wa filamu za Kitanzania endapo watayarishaji wake watatumia njia ambazo watayarishaji wa filamu ya Mdundiko wametumia kufika huko.
TASNIA ya filamu nchini inazidi kukua kuliko nchi zote za Afrika ya Mashariki, lakini inakumbana na changamoto kadhaa, kubwa ni jinsi ambavyo itaweza kufikia medani za kimataifa.
Hivi karibuni, filamu ya Mdundiko iliyotengenezwa Tanzania imevuka mipaka kwa kuchaguliwa katika tuzo kubwa na kushiriki matamasha makubwa, tuzo ya kwanza ni African Film Academy Awards (ZAFAA) katika kipengele cha filamu ya kiasili (Best Indigenous Movies). Katika kipengele hiki, filamu ya Mdundiko ndiyo pekee iliyoingia kutoka Afrika Mashariki, huu ni ushindi kwa tasnia ya filamu Tanzania. Tuzo hizo zinatarajia kufanyika Uingereza mwaka huu na jambo la kujivunia ni kwamba katika kipengele hiki, Mdundiko imekuwa filamu pekee kutoka Afrika Mashariki. Nyingine zote zilizoingia kinyang’anyiro cha sinema za asili zimetoka Afrika Magharibi, yaani Ghana na Nigeria.
Filamu ya Mdundiko inaweza kuwa ndiyo mkombozi wa filamu za Kitanzania endapo watayarishaji wake watatumia njia ambazo watayarishaji wa filamu ya Mdundiko wametumia kufika huko. Hiyo ndiyo njia ya kuitangaza Tanzania kiutalii na utamaduni kutokana na mfumo wa utayarishaji wa filamu ambayo imerekodiwa kiasili.
Tuzo za pili ni tuzo kubwa ulimwenguni yaani Oscars ambazo msanii au mtayarishaji yeyote anapopata nafasi ya kushiriki au kuchaguliwa kuwemo katika tuzo hizo huona fahari kubwa pamoja na kuwa na tuzo nyingine duniani kote bado hakuna ambazo hadi leo zimefikia hadhi ya tuzo za Oscars.
Mdundiko inaweza kuitoa kimasomaso Tanzania kwa kuchaguliwa katika tuzo hizo kwa mwaka 2013/14.
Imeingia kwenye tuzo za Oscars kati ya filamu lukuki za Afrika, kati ya hizo ni 26 tu ndizo zimeingia kugombea tuzo ya filamu iliyotengenezwa kiasili na kutumia lugha ya asili.
Si hivyo tu, filamu ya Mdundiko, Oktoba 13, 2013 itashiriki tamasha kubwa la filamu la Silicon Valley African Film Festival (SVAFF 2013) ambako itaonyeshwa kwenye Jumba la sinema la San Antonio Circle Mountain View, Chuo cha Muziki na Sanaa cha California, Marekani. Hiyo itakuwa Jumapili, saa 4:45 asubuhi hadi saa 6:45 mchana kwa saa za Amerika.
Walikotoka waigizaji wa Mdundiko
Walioshiriki filamu ya Mdundiko, si wageni kutoka nje, hao na wengine ambao ni watayarishaji kwa muda mrefu hawajafanikiwa kupeleka filamu katika matamasha ya ndani. Kinara wa filamu hiyo, Richard Mshanga ‘Masinde’, akisaidiwa na Lumole Matovolwa ‘Biggie’. Wengine ni, Hisani Muya ‘Tino’, Simon Mwapagata ‘Rado’, Fatuma Makongoro ‘Bi. Mwenda’, Ummy Wencelaus ‘Dokii’, Adam Melele ‘Swebe Santana’ Julieth Samson ‘Kemmy’ Mohamed Fungafunga ‘Jengua’ pamoja na Yusuf Embe na wengineo. Hao ni kati ya majina makubwa katika tasnia ya filamu nchini, wengi wao walikosa njia ya kujitangaza kimataifa, lakini kupitia Mdundiko majina yao yameandikwa katika historia ya filamu, haitakuwa ajabu kusikia Masinde anashiriki filamu za Hollywood akiigiza na kina Angelina Jolie na wengineo.
Mwongozaji wao, Jackson Kabigiri ‘Jack’ ambaye hana uzoefu mkubwa, ameonyesha uwezo, fikra zake za kubadilisha tasnia ya filamu na kwenda katika medani za kimataifa. Mtayarishaji na aliyepiga picha za filamu hiyo Timoth Conrard ‘Tico’ hajatayarisha filamu nyingi, ameonyesha inawezekana kufikia medani za kimataifa.
Tico pia ndiye mtunzi wa hadithi ya filamu hiyo inayoburudisha na kuelimisha. Kwa Mdundiko kuchaguliwa katika matamasha hayo, Tico na Jack wataweza kwenda Uingereza na Marekani na kukutana na watayarishaji wakubwa wa filamu duniani.
Filamu yenyewe imebeba taswira halisi ya maisha ya Mtanzania kwa kuongelea baadhi ya mila na tamaduni za jamii zetu, changamoto bado kubwa kwani hata filamu hiyo imefanikiwa kutokana na ufadhili wa Media Fund Development International (MFDI).
Matarajio ni kuwa baada ya Mdundiko kufungua njia, wengine watumie mwanya huo kutangaza kazi zao kimataifa na kutangaza utamaduni wa Mtanzania.