Mdogo wa Mandojo asimulia dakika za mwisho za kaka yake

Mdogo wa marehemu Joseph Francis (Mandojo) akizungumza na wanahabari nyumbani kwake Mnada Mpya jijini Dodoma. Pocha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Wakati mdogo wa Joseph Francis (Mandojo) akisimulia dakika za mwisho za mdogo wake duniani, ndugu wamemkana mtu aliyejitambulisha mtandaoni kama ndugu yao.
Dodoma. Mdogo wa mwanamuziki na mfanyabiashara, Joseph Francis maarufu kama Mandojo, aliyefariki dunia jana Jumapili Agosti 11, 2024, amesimulia dakika za mwisho alivyokutana na kaka yake kabla ya umauti.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake Mnada Mpya, jijini Dodoma leo Jumatatu Agosti 12, 2024, Yohana Chacha amesema kaka yake ni mkazi wa jijini Dar es Salaam na alikwenda Dodoma kwa mkewe.
“Ana siku kama tano tangu aje, alikuwa anakwenda Babati (mkoani Manyara) kwenye shoo, ndio akapita hapa kumsalimia mke wake,”amesema Chacha.
Amesema jana alipigiwa simu na mkewe (Mandojo) kuwa tangu alipotoka nyumbani juzi hajarudi mpaka jana.
“Nikawapigia simu baadhi ya rafiki zake, akiwemo Amani (ofisa magereza) waliosoma naye kuanzia kidato cha kwanza, aliniambia hajamuona,” amesimulia Chacha.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa nyumbani kwa Mdogo wake na marehemu Joseph Francis (Mandojo) Mnada mpya jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Hivyo, alimwambia Ivyo, a mke wa Mandojo kuwa wagawane kwenda kuripoti vituo vya polisi ambapo mke wa marehemu alikwenda kituo cha polisi Nzuguni.
Amesema baada ya kwenda huko aliambiwa kituo kimehamia Nanenane, jambo lililomfanya yeye kwenda kuripoti kituo cha kati cha Polisi.
Amesema alipofika kituo cha polisi cha kati, alimkuta Mandojo ambaye alipozungumza naye alimwambia ampeleke hospitali.
“Wakati huo (anamwambia ampeleke hospitali) polisi walikuwa wameshampeleka hospitali na akapata matibabu, lakini aliona bado anajisikia vibaya, hivyo tumpeleke hospitali,”amesema.
Kuhusu Mandojo kufika polisi na hali aliyokuwa nayo, Chacha amesema suala hilo waulizwe polisi.
Mwananchi ilipomtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma ameisema yupo kikaoni na akimaliza atamrudia mwandishi.
“Sisi kama familia tunalizungumzia lile lililo ndani ya uwezo wetu. Wakati tunampeleka hospitali hakuwa katika hali ya kuongea. Polisi waliniruhusu kumpeleka hospitali na walikuwa tayari kunipa gari, lakini bahati nzuri mkewe alikuwa amefika na gari,” amesema.
Amesema alipatiwa matibabu katika idara ya magonjwa wa dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, lakini baada ya nusu saa walipewa taarifa kuwa ndugu yao amefariki dunia.
Chacha amesema mtu aliyejitokeza katika mitandao ya jamii anayejiita kuwa ni Msafiri hawamfahamu, na si mwanafamilia na wala si rafiki yake.
“Nataka nikanushe taarifa alizozitoa jana si za kweli, taarifa za familia ni hizi na za upande wa polisi mtapewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma,”amesema.
Kuhusu atazikwa lini, amesema kaka yao mkubwa Christian yuko safarini akitokea mkoani Mtwara, hivyo akifika watakaa kama familia na kupanga watazika lini na wapi.
Amesema msiba upo jijini Dodoma na Wilaya ya Manyoni mkoani Singida ambapo marehemu wazazi wao walizikiwa.
Amewaomba polisi kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.