MC ZIPOMPAPOMPA KUZIKWA IJUMAA

Wednesday November 11 2020
zipo 2 pic

Mwili wa aliyekuwa muigizaji wa Bongomovie, Gladness Chiduo ‘Mc Zipompapompa’ unatarajiwa kupumzishwa kwenye nyumba ya milele Ijumaa ya Novemba 13.

Akizungumza na Mwanaspoti, binti mlezi wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Lona amesema baada ya kikao cha familia wameafikiana kuwa maziko yafanyike Ijumaa.

“Kwa sasa mwili wa mama uko mochwari Lugalo hospitali, tutazika Ijumaa. Tunategemea kuzika katika makaburi ya Kinondoni lakini hilo bado halijathibitishwa kwa sababu bado hatujapata kibali.” ameeleza Lona, ambaye alikuwa akiishi na Mc Zipompapompa siku zote nyumbani kwao Mbweni, Dar es Salaam.

Akisimulia namna mauti yalivyomkuta mama yao, Lona amesema mara ya kwanza Mc Zipompapompa alikuwa akihisi kuumwa, wakaenda hospitali ambapo aligundulika kuwa presha yake imepanda mpaka 160mm, akapitiwa matibabu na iliposhuka wakarejea nyumbani.

“Lakini tukaa siku chache ikarudi tena, tukaenda tena hospitali, akatibiwa, ikashuka, tukarudi nyumbani ambapo tukaa kama siku mbili tu hali ile ile ikamrudia. Tukamkimbiza hospitali ambapo akalazwa, lakini ilipofika saa9 usiku akapoteza maisha. Hiyo ilikuwa ni Jumapili.” amesimulia.

Kuhusu familia, Mc Zipompapompa ameacha watoto watatu wakubwa, wawili wa kiume na wa kike mmoja, lakini pia ameacha wajukuu watatu.

Taarifa zaidi, endelea kuwa karibu na tovuti ya Mwanaspoti na mitandao yetu ya kijamii

Advertisement