Mbona fresh, Ronaldo ndiye Pedeshee wa Diamond

Friday January 01 2021
mond pic

JINA Pedeshee lilikuwa maarufu sana kwenye muziki wa dansi tofauti na hata upande wa Bongofleva. Hata hivyo jina hilo taratibu linaenda likipotea au lipo ila linatumika kwa mtindo mwingine tofauti na ilivyokuwa imezoeleka.

Mara nyingi pedeshee ni mtu aliyekuwa anatajwa na msanii katika wimbo wake kwa lengo kumshawishi kumtunza fedha jukwaani au tayari alishatoa mchango wa aina yoyote kufanikisha kazi za msanii husika.

Utamaduni huo ulikuzwa zaidi na wasanii kutoka DR Congo lengo likiwa ni kuwasifu baadhi ya watu hasa wahisani na wafadhili wao kwa ajili ya kuendelea kutengeza mazingira mazuri ya kuendeleza uhusiano baina yao.

Mwimbaji wa Bongofleva, Diamond Platnumz kwa namna anavyomrusha mshambuliaji Cristiano Ronaldo ‘CR7’ katika nyimbo zake waweza kusema ndiye pedeshee wake. Twende taratibu.

mond pic 2

Katika wimbo wake mpya ‘Waaah’ aliomshirikisha mkali wa soukous kutokea DR Congo, Koffi Olomide, Diamond anasikika akimtaja mchezaji huyo ghali uliwenguni na mshindani wake Lionel Messi.

Advertisement

Sio mara ya kwanza kwa Diamond kumtaja Ronaldo katika nyimbo zake, alifanya hivyo 2015 katika wimbo wake uitwao Nana aliomshirikisha Mr Flavour kutoka Nigeria.

Ikumbukwe hivi karibuni Ronaldo anayeichezea timu ya taifa ya Ureno na Juventus inayoshiriki Ligi Kuu Italia (Serie A) alishinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Karne (2001-2020) katika tuzo za Globe Soccer zilizofanyika Dubai na kuzidi kumuongezea thamani.

Licha ya Diamond kutajwa kama msanii mwenye mafanikio makubwa kimuziki na kifedha hapa nchini, sio vibaya kumfanya Ronaldo kuwa pedeshee wake kwani CR Mnyama anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani milioni 500 kwa mujibu wa mtandao wa Celebrity Net Worth.

mond pic 1

Hivyo, Ronaldo ana fedha nyingi tu za kutosha kumpatia Diamond endapo naye atakuwa na roho ya utoaji kama pedeshee pale atakaposikia jina lake limetajwa katika wimbo na msanii fulani maarufu, pengine ndiye Chibu.

Je, ni lini hasa Ronaldo atasikia nyimbo hizo alizotajwa na Diamond na hata kumtunza fedha au chochote kitu?

Septemba mwaka huu, mchekeshaji Elsa Majimbo mwenye umri wa miaka 19 kutoka nchini Kenya alitangazwa kuingia mkataba na kampuni ya mitindo ya msanii mkubwa duniani kutoka Marekani, Rihanna iitwayo Fenty.

Majimbo alipata dili hilo baada ya kujipatia umaarufu kutokana na video zake katika mitandao ya Twitter na Instagram tangu kuanza kwa mlipuko wa virusi vya corona na kumfikia Rihanna, na baadaye zilimfikia mchekeshaji mkubwa duniani, Steve Harvey.

Hivyo katika ulimwengu huu wa digitali kazi za sanaa zinasafiri na kufika mbali zaidi na kuwafikia watu ambao msanii husika hakutarajia kuwafikia, hivyo suala la Ronaldo kusikia nyimbo za Diamond ni muda tu ndio utaamua.

Licha ya hilo, Ronaldo na Diamond ni mapacha wanaofanana kwa kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo linasababisha kuvuna mamilioni ya fedha kutokana na dili za ubalozi wanazopata.

Ronaldo ndiye binadamu mwenye wafuasi (followers) wengi zaidi duniani kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram akiwa nao milioni 249, pia ndiye anaongoza upande wa Facebook akiwa na watu milioni 124.

Lakini Diamond ndiye msanii anayeongoza Tanzania kufuatiliwa na watu wengi zaidi kwenye mitandao ya Instagram, Facebook na YouTube. Katika mitandao hiyo, Chibu anafuatiliwa na watu milioni 11.3 Instagram, ilhali huko Facebook ana wafuasi milioni tatu na YouTube wako milioni 4.6. Idadi hiyo ya wafuasi ni mtaji tosha kwa Ronaldo na Diamond kufikisha ujumbe wao kwa watumiaji mitandao.


Imeandikwa na Peter Akalo

Advertisement