MASTORY YA OSCAR OSCAR: Unataka kutuachaje?

Muktasari:
- Tuache chuki, tuache wivu, tujifunze kwa waliofanikiwa
KAMA kuja jambo ambalo kila mwanadamu ana uhakika nalo basi ni kifo. Ni suala la muda tu. Itakuwa asubuhi, mchana, jioni au usiku. Ni suala la muda tu. Hatupaswi kuwa na hofu. Hatupaswi kuwa na wasiwasi, lakini unatuachaje? Hilo ndilo swali ambalo tunatakiwa kulipatia majibu tungali hai. Bruce Lee ni moja kati ya waingizaji wa muvi maarufu sana ambao hawakuishi muda mrefu. Alizaliwa 1940 na kufariki dunia 1973. Ukifanya hesabu utagundua kuwa nguli huyu wa martial arts aliishi miaka 33 tu. Ni muda mfupi sana, lakini bado dunia inamuimba. Bado vizazi na vizazi vinaendelea kujifunza kupitia kazi zake. Bado jina lake linaendelea kutajwa kila kukicha. Tunaweza kuwa tunaogopa kifo, lakini hilo ndilo jambo pekee ambalo tuna uhakika kila mmoja wetu atalipitia. Haijalishi umeishi miaka mingapi. Haijalishi utakuwa umeacha alama ngani kwenye maisha ya watu. Unadhani leo au kesho ukiondoka jina lako litatajwa kwa miaka mingapi? Usinipe jibu. Unadhani leo au kesho ukiondoka ni watoto wangapi mtaani watakulilia? Usinipe jibu. Huu ni wakati sahihi wa kuendelea kukumbushana umuhimu wa kuwekeza kwenye maisha ya watu. Haijalishi umeishi kwa miaka mingapi, ni muda wetu wa kuendelea kugusa maisha ya watu.
Tuko kwenye dunia ambayo hatima ya kila mtu iko mikononi mwake. Bob Marley ni msanii maarufu wa muziki wa reggae. Alizaliwa 1945 na kufariki dunia 1981. Ukifanya hesabu utagundua kuwa aliishi miaka 36. Bado alikuwa kijana. Bado alikuwa na mengi ya kuifanyia dunia. Leo ni zaidi ya miaka 40 tangu afariki, lakini bado watu wanamuimba. Sio lazima uishi miaka 100. Unaweza kuishi muda mfupi, lakini unaendelea kugusa maisha ya watu. Tunazo changamoto za uchumi. Tunazo changamoto za kiutamaduni, lakini bado haituzuii kuendelea kugusa maisha ya watu. Wapo watu wameishi miaka 100 na hakuna anayewakumbuka. Wapo watu wameishi miaka 80 majina yao hayatambuliki. Kupanga ni kuchangua. Umepanga watu wakukumbuke kwa lipi? Nipe maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Kila mmoja wetu ana nafasi ya kuacha alama kwenye jamii. Sio lazima uwe tajiri. Sio lazima uwe maarufu. Sio lazima uwe na madaraka makubwa serikalini. Unataka kutuachaje? Usinipe jibu. Hatuna uhakika wa maisha tunayoishi, lakini tuna uhakika kuwa siku moja tutaondoka duniani. Hakuna jambo zuri kama maisha yako kugusa wengine. Hakuna jambo nzuri kama kuwashika mkono wasio na uwezo. Tuna mtihani wa kuacha alama njema kwenye maisha ya watu. Hakuna aijuaye kesho. Kila nikitazama Bongo Movie huwa namkumbuka Steven Kanumba. Pumzika kwa amani kaka. Alizaliwa 1984 na kufariki dunia 2012. Ukifanya hesabu utagundua kuwa aliishi kwa miaka 28. Alifariki akiwa kijana mdogo lakini bado anaishi kwenye Bongo Movie. Kuna watu wengi wameibuka na wanafanya vizuri, lakini bado Kanumba anaendelea kuheshimika. Haijalishi umeishi miaka mingi kiasi gani lengo ni kugusa maisha ya watu. Kanumba alikuwa miongoni mwa watu ambao waliongeza thamani ya filamu za nyumbani. Aliboresha uzalishaji, alisaidia kutanua soko la filamu nje ya Tanzania. Kifupi Kanumba aliacha alama kwenye filamu za Kitanzania ambayo
itaishi milele. Hakuishi muda mrefu, lakini maono yake bado yanaishi. Tuendelee kufanya kazi kwa bidii. Tuendelee kugusa maisha ya watu. Bila kujali mimi na wewe tutaishi muda gani tuna wajibu wa kuendelea kugusa maisha ya watu kila siku . Bila kujali changamoto mbalimbali za kimaisha ni lazima tuache alama kwenye jamii yetu. Unadhani ukiondoka leo watu watakukumbuka kwa lipi? Usinipe jibu.
Maisha tunayoishi ndugu zangu ni kwa neema tu. Wapo watu wameondoka duniani miaka 30 iliyopita lakini bado barabara mpya zikijengwa wanawakumbuka. Wapo walioondoka miaka 20 iliyopita, lakini watu wakijenga shule mpya wanawakumbuka. Wema haufi. Ukigusa maisha ya watu utaishi milele. Tujitahidi kuacha alama kwenye maisha ya wapendwa wetu.