MASTORI YA OSCAR: Ali Kiba na Messi, Diamondi na Ronaldo

Monday May 09 2022
Oscar PIC
By Oscar Oscar

UBISHI wa nani mchezaji bora kati ya Pele na Maradona, walibishana sana wazazi wetu na mwishowe waliuacha bila kupata jibu sahihi. Sio vibaya kuwajadili na sio vibaya kupishana mtazamo. Wapo wanaomtaja Pele. Wapo wanaomtaja Maradona. Ubishi kati ya bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma na Sikinde, walibishana sana wazazi wetu na mwisho waliuacha bila kupata majibu. Wapo wanaoitaja Msondo kuwa bora zaidi.

Wapo wanaoiona Sikinde ndio baba lao. Sio vibaya kujadili ubora wa bendi hizi. Sio vibaya pia tukipishana mawazo. Wakati mwingine mnapotofautiana kwa hoja ndio raha yenyewe. Ukiona pande mbili zinalinganishwa kila siku na watu wanagawanyika, ujue zimekuwa bora zama zake.

Wapo watu wengi wanafanikiwa duniani kwa sababu ya kuzaliwa na vipaji au vipawa, lakini wengine wanafanikiwa zaidi kwa kujifunza na kuweka bidii kwenye jambo ambalo pengine si vipaji asili.

Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wamelinganishwa kwenye soka katika miaka karibu 15 hivi karibuni. Kuna vitu vingi wanafanana, lakini vipo vitu vingine wanatofautiana. Mitazamo ni mingi, lakini watu hawajawahi kukubaliana. Ni vigumu kusema nani ni bora kuliko mwingine. Wote wanafunga. Wote wanaburudisha.

Wote ni washindi. katika muziki wa Bongofleva Tanzania kwa sasa, Ali Kiba na Diamond Platinumz ni kama Messi na Ronaldo. Kama Pele na Maradona. Ni kama Msondo na Sikinde. Wamefanya kazi nzuri miaka 10 ya hivi karibuni. Kila mtu ana kijiji chake. Kila mmoja ana mashabiki wake.

Tanzania bado hatuamini kutengeneza mastaa wengi kwenye tasnia moja. Tunaishi kwenye tamaduni za mfalme mmoja kwa kila utawala. Kwenye kikapu nchi imewahi kujivunia Hasheem Thabeet hadi alipoanza kuporomoka kiwango. Zama hizi kwenye soka watu tunajivunia Mbwana Samatta hadi anapoanza kuporomoka kiwango. Hakuna mastaa wengine kwenye levo ya Hasheem. Hakuna mastaa wengine kwenye levo ya Samatta. Sio lazima Diamond Platinumz ashuke ndio tumpandishe mwingine.

Advertisement

Wote wanaweza kuwa juu kwa wakati mmoja na maisha yanaendelea. Mara nyingi ubishi na uchambuzi wa nani bora kati ya Ali Kiba na Diamond umejikita kumpandisha mmoja na kumshusha mwingine badala ya kutaka wote wawe juu na kuongeza wengine wenye levo hiyo. Aslay alipaswa kufika levo ya Diamond na Ali Kiba kwa sasa.

Marioo anapaswa kufika levo ya Kiba na Diamond kwa sasa. Harmonize yupo juu anafanya kazi nzuri. Tunahitaji mastaa kwenye levo ya Kiba na Mondi hata 20 nchini. Hakuna ubaya wowote. Wazazi wetu waliowatazama Pele na Maradona waliburudika sana. Sisi tuliowaona Messi na Cristiano tuna bahati. Sio vibaya kuwalinganisha.

Sio vibaya kila mtu kuchagua upande, lakini utofauti kimtazamo usiwe na lengo la kumshusha mmoja ili kumpandisha mwingine. Wote wanaweza kuwa juu. Wote wanaweza kuwa wasanii wakubwa. Waliowaona Msondo na Sikinde wakiwa kwenye ubora wao walikuwa na bahati kubwa kama ambavyo mimi na wewe tunawaona Diamond na Kiba kwenye zama hizi.

Ali Kiba amekuwa kwenye gemu karibu miaka 20. Sio jambo dogo. Hakuna kitu kigumu kama kubaki juu. Kuna safari ndefu kwenda juu ya kitu chochote, lakini kuna safari ndefu zaidi kubaki juu. Watu wengi hasa kwenye sanaa na vipaji hawatoboi zaidi ya miaka 10. Kukaa juu miaka zaidi ya 10 sio jambo dogo. Diamond alikuja baadaye, lakini ni ‘role model’ wa vijana wengi hata kama hawasemi.

Ndiye msanii aliyetengeneza pesa nyingi kupitia muziki. Ndiye msanii mwenye ushawishi zaidi kwenye mitandao kuliko mtu mwingine yeyote. Hii kitu haiji kwa bahati mbaya.

Platinumz amebadilisha kabisa mwelekeo wa video zake. Kutazama video zake siku hizi ni kama unaangalia muvi. Yuko kwenye dunia yake kabisa. Hawa watu sio vibaya kuwalinganisha. Sio vibaya mtu kuchukua upande, lakini mwingi lazima uwe kwenye kujenga zaidi. Ni aina ya vijana ambao wameukuza na kuungezea thamani muziki wetu na hasa zama hizi.

Ni kweli wapo wakongwe kama kina Lady Jaydee, Mr II a.k.a Sugu, Mwana FA, Prof Jay na wengine ambao walitoka na muziki huu mbali, lakini zama hizi Diamond na Kiba wameugeuza muziki kuwa pesa. Thamani imepanda ya muziki. Heshima ya Bongo fleva imeongezeka.

Kuna muda tumekuwa tukitumia nguvu kuwakuza watu, lakini baada ya kuwakuza tunatumia tena nguvu kubwa kuwashusha. Muziki wetu hauwezi kuendelea kwa kuwashusha chini wasanii wakubwa. Tunaweza kuwakuza wengi tu kila siku. Muziki ni ajira kubwa kwa nchi kama yetu ambayo sehemu kubwa ya watu wake ni vijana.

Kama unamkubali Ally Kiba usisite kuniandikia moja kati ya vitu unavyofurahia kutoka kwake kupitia namba ya simu hapo juu. Na kwa wewe ambaye umekuwa shabiki mkubwa wa Diamond Platinumz nieleze kupitia namba ya simu hapo juu chochote unachofurahia kutoka kwa Diamond Platnumz. Kiba ni kama Lionel Messi, ilhali Diamond Platinumz ni kama Cristiano Ronaldo.

Advertisement