Licha ya changamoto Paris Jackson , anasimamia imara urithi wa baba yake
Muktasari:
- Tangu alivyozaliwa Aprili 3, 1998 amekulia katika maisha ya kistaa kutokana na umaarufu mkubwa wa baba yake, Michael ambaye alifariki dunia mwaka 2009.
MMOJA wa watoto wa marehemu mfalme wa muziki wa pop, Michael Jackson aitwaye Paris Jackson maisha yake yamevutia wengi na amekuwa akifuatiliwa zaidi.
Tangu alivyozaliwa Aprili 3, 1998 amekulia katika maisha ya kistaa kutokana na umaarufu mkubwa wa baba yake, Michael ambaye alifariki dunia mwaka 2009.
Baada ya kifo cha baba yake, Paris pamoja na ndugu zake walilelewa na bibi yao, Katherine Jackson na hapa Mwanaspoti linakuchambulia maisha, kazi za sanaa na kashfa mbalimbli zikiwamo za kutumia dawa za kulevya zinazomhusu binti huyo.
KWENYE MUZIKI YUKO HIVI
Tofauti na matarajio ya watu, huenda angerithi mikoba ya baba yake, mambo ni tofauti na Paris ameamua kupita njia yake akichagua mtindo wa Indie na Rock tofauti na MJ ambaye alikuwa mfalme wa Pop.
Aliingia katika muziki mwaka 2010, ana albamu moja 'Wilted' iliyotoka mwaka 2020 chini ya lebo ya Republic, huku pia akiwa na Extended Playlist (EP) mbili tu 'The Lost EP' ya mwaka 2022 na 'The Soundflowers' ya 2020 chini ya lebo ya Self Released.
Licha ya kutoa kazi hizo, wengi wanaamini anapitia tu upepo wa baba yake na hana kipaji halisi kama ilivyokuwa kwa familia yao iliyoanza kutamba miaka ya 1980 na kundi la Jackson 5.
URITHI
Licha ya kujenga maisha yake binafsi, Paris bado anaonyesha heshima kubwa kwa baba yake katika kurithi kipaji cha muziki na mara nyingi amekuwa akishiriki katika matukio ya kumbukumbu ya Michael na kueleza jinsi alivyomsaidia kumfikisha hapo alipo.
Kwa jumla, Paris ameendelea kuonyesha licha ya kubeba jina kubwa la familia ya Jackson, ana uwezo wa kujenga brandi yake kama msanii kutokana na vipaji vingi alivyonavyo.
VIPAJI VINGINE
Mbali na muziki Paris ana vipaji vingi ikiwamo uigizaji na huku ndiyo wengi wanaona panamfaa na siyo kuimba.
Amewahi kuigiza kwenye filamu mbalimbali za Marekani zikiwamo Gringo ya mwaka 2018 akicheza kama Nelly, The Space Between, Habit, Sex Appeal na One Spoon of Chocolate.
Pia Paris ni mwanamitindo maarufu nchini humo akifanya kazi na Kampuni ya IMG Models inayowasimamia walimbwende wakubwa Marekani.
UHUSIANO WAKE
Amekuwa katika uhusiano na wasanii mbalimbali akiwamo mwanamuziki Gabriel Glenn aliyewahi kufanya naye kazi katika bendi yao ya The Soundflowers.
Uhusiano huo ambao ulikuwa unavutia zaidi mashabiki ulivunjika mwaka 2020, kabla ya kuanza kuhusishwa na mwanamitindo na mwigizaji wa Uingereza, Cara Delevingne, ingawa hawajawahi kuthibitisha uhusiano huulicha ya ukaribu wao ulikuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
UMAARUFU CHANGAMOTO
Paris aliwahi kusema moja ya changamoto kubwa aliyokumbana nayo katika maisha yake ni kuishi katika familia ya watu maarufu ingawa baadaye alizoea hali hiyo.
"Kuna muda unahitaji usiri au kuwa faragha na familia yako au hata marafiki, hata hivyo, ukitoka tu mara ushapigwa picha kesho umesambaa magazetini unakuwa hauna uhuru wa kutoka," anasema Paris
Anasema mbali na changamoto hiyo aliwahi kupata msongo wa mawazo kutokana na presha kubwa na matarajio makubwa kutoka kwenye vyombo vya habari.
MIGOGORO YA FAMILIA
Baada ya kifo cha Michael, familia ya Jackson imekuwa katika migogoro ya mara kwa mara hasa kutokana na urithi na usimamizi wa mali.
Baadhi ya migogoro hiyo ni ya familia na wasimamizi wa kazi za baba yake na inadaiwa waliwahi kujaribu kuwadhulumu watoto wa MJ.
Moja ya migogoro hiyo ni kuhusu kazi za baba yake na hasa kutokana na mapato ya wimbo wa 'Thriller' na Paris aliwasilisha ombi mahakamani kupinga kampuni za sheria zinazosimamia mali za MJ kutaka kumdhulumu.
Katika kesi hiyo, inaelezwa Paris alishinda na kupokea kiasi cha takribani Dola 65 milioni kutoka kwenye mali hiyo kama faida.
Pia mwishoni mwa mwaka 2025, Paris alipinga namna mali za baba yake zinavyosimamiwa na kuna usimamizi mbovu uliofanywa na wasimamizi wa mali hizo na kuhoji zilipo zaidi ya Dola 625 milioni zilizolipwa kwa kampuni za sheria kama kile kinachoitwa malipo ya ziada.
Hata hivyo, licha ya kupokea kiasi hicho cha pesa, anadai zaidi ya Dola 300 milioni bado zimewekezwa vibaya na kuwashutumu wasimamizi hao kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi kwa kujipa fidia inayokadiriwa kufikia Dola 100 milioni.
Paris pia hivi karibuni aliwasilisha pingamizi jipya mahakamani dhidi ya mali ya baba yake (ikiwamo jumba la kifahari), hatua inayoongeza mvutano katika mgogoro wa kisheria unaoendelea kuhusu gharama za mawakili na namna mali hiyo inavyosimamiwa.
Hata hivyo,, baadhi ya migogoro amekuwa akijaribu kujitenga nayo na kuendelea na mambo yake.
DAWA ZA KULEVYA, UNYANYASAJI
Mwanadada huyo amewahi kuhusishwa na matumizi ya dawa za kulevya katika baadhi ya ripoti za vyombo vya habari, hasa alipokuwa akipitia changamoto za kisaikolojia baada ya kifo cha baba yake.
Mwenyewe amewahi kukiri katika mahojiano kadhaa kuwa aliwahi kupitia kipindi kigumu akiwa kijana na alijaribu kutumia baadhi ya vitu kama pombe kupita kiasi na dawa za kulevya. Hata hivyo, anaeleza hali hiyo ilitokana na msongo wa mawazo, upweke na presha ya maisha ya umaarufu.
Anasema hata hivyo vitu hivyo havikumsaidia kuwa sawa na mara kadhaa amewahi kuzungumzia kuhusu changamoto alizopitia ili kuhamasisha vijana kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na kutunza afya ya akili.
“Kuacha matumizi ya dawa za kulevya hakumaanishi moja kwa moja maisha yanakuwa makamilifu. Baada ya miaka michache, mambo yakawa magumu sana, kwa muda ambao ulionekana kama hauna mwisho. Wakati huo sikuwa tena na mbinu zile zile za kujinusuru nilizokuwa nimezoea kutumia kukabiliana na hali ngumu. Ilinibidi nijifunze kuishi maisha kama yalivyo.”
Paris pia amewahi kuzungumzia suala la ubakaji ikiwamo kuwahi kubakwa akiwa bado mdogo na mzee ambaye hakuwahi kumtaja.
Anasema tukio hilo lilikuwa moja ya mambo yaliyomletea maumivu makubwa ya kihisia na kuchangia changamoto za afya ya akili alizopitia wakati wa ujana wake.
Paris anasema kwa muda mrefu alibeba maumivu hayo kimya kimya kabla ya kuamua kuzungumza hadharani ili kusaidia wengine wanaopitia hali kama hiyo.