Harmonize, RockStar Africa kuna jambo!
Muktasari:
- Harmonize, mwanzilishi wa Konde Music Worldwide, ndani ya miaka mitatu tayari ameshirikiana na wasanii watatu kati ya wanne wa Bongofleva ambao wapo chini ya RockStar Africa kwa sasa.
NDIVYO unavyoweza kusema kwa jinsi ambavyo Harmonize ameendelea kushirikiana na wasanii ambao wapo chini ya lebo ya RockStar Africa, hatua ambayo inaonyesha uhusiano mzuri uliyopo kati yao.
Harmonize, mwanzilishi wa Konde Music Worldwide, ndani ya miaka mitatu tayari ameshirikiana na wasanii watatu kati ya wanne wa Bongofleva ambao wapo chini ya RockStar Africa kwa sasa.
Ikumbukwe RockStar Africa inawasimamia Ommy Dimpoz, Abigail Chams, Young Lunya na Aslay, mwanachama wa zamani wa kundi la Yamoto Band chini ya Mkubwa Na Wanawe.
Vilevile wasanii wote wa lebo hiyo, pia wanafanya kazi na Sony Music Entertainment Africa, dili ambalo lilitangazwa mwaka 2022, kwa wanamuziki hao wa watatu wa mwisho.
Ushirikiano kati ya wasanii hao watatu wa Rockstar Africa na Harmonize, umezalisha jumla ya nyimbo sita ambazo kwa asilimia kubwa zimefanyaje vizuri na kuongoza chati mbalimbali za digital streaming.
1. Aslay vs Harmonize
Muda mfupi baada ya Aslay kutambulishwa RockStar Africa aliachia wimbo wake wa kwanza, Follow Me (2022) ambao alimshirikisha Harmonize, huku ukiwa umetayarishwa na John Hamis Misana.
Huu ndio ulikuwa mradi wa kwanza kati ya RockStar Africa na Konde Music Worldwide, lebo yake Harmonize ambayo ilianza kufanya kazi rasmi mnamo Oktoba 10, 2019 ikiwa ni kipindi kifupi baada ya kujitoa WCB Wasafi.
Kolabo hiyo ilifanya vizuri kwa sababu mashabiki wengi walikuwa na kiu ya kumsikiliza Aslay baada ya ukimya wa muda uliotokana na mchakato wa kuhamisha haki ya kazi zake katika menejimenti mpya, yaani RockStar Africa na Sony Music.
Ikiwa ni zaidi ya miaka mitatu tangu kolabo hiyo imetoka, hadi sasa huo ndio wimbo wa Aslay chini ya lebo hiyo uliofanyika vizuri zaidi YouTube ambapo video yake imeshatazamwa (views) zaidi ya mara milioni 3.6.
Utakumbuka ni hivi karibuni tu Aslay ameachia albamu yake ya pili, My Way (2026), ikiwa na jumla ya nyimbo 14 huku akiwashirikisha wasanii wawili ambao ni Chino Kidd na Kontawa, mshindi wa TMA 2023.
2. Abigail vs Harmonize
Hadi sasa Abigail Chams ndiye msanii wa RockStar Africa ambaye ameshirikiana zaidi na Harmonize, na kwa ujumla Abigail ni kati ya wasanii wa wawili wa kike wa Bongofleva ambao wapiga kolabo nyingi na Konde Boy.
Abigail Chams amemshirikisha Harmonize katika ngoma zake mbili, Closer (2022) na Me Too (2025), ambao video yake imeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 38 ukiwa ni wimbo wake wa kwanza kufanya hivyo.
Miezi michache baada ya kuachia kolabo yao ya tatu (Me Too), ndipo Abigail Chams aliteuliwa kuwania tuzo za BET nchini Marekani akiwa ni msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kupata nafasi hiyo.
Naye Harmonize amemshirikisha Abigail Chams katika nyimbo zake mbili pia ambazo ni Leave Me Alone (2022) na Lala (2025), huku Abigail akionekana katika video ya wimbo wa Harmonize, Furaha (2025).
Utakumbuka Abigail Chams ni mwanamuziki wa pili wa kike Tanzania kusainiwa na Sony Music, wa kwanza alikuwa staa wa muziki wa Injili, Rose Muhando aliyetangazwa kuchukua dili hilo hapo Februari 2012, kisha kutoa kibao chake, Wololo (2013).
3. Lunya vs Harmonize
Siku chache zilizopo Young Lunya ameachia ngoma yake mpya, Mkuu wa Majeshi (2026) akishirikiana na Harmonize, na tayari ngoma hiyo imeanza kufanya vizuri kutokana na nguvu yao ya ushawishi.
Young Lunya ambaye ni mshindi mara nne wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), wiki moja kabla ya wimbo huo kutoka alitajwa na Harmonize kama msanii bora wa Hip Hop Bongo kwa sasa.
Huo unakuwa ni wimbo wa pili kwa wawili hao kushirikiana baada ya awali Young Lunya kusikika katika ngoma ya Harmonize, Bedroom Remix (2020) ambayo ilikutanisha rapa wengi wakali. Mbali na Young Lunya, wengine waliosikika ni Country Wizzy, Moni Centrozone, Billnass, Rosa Ree, Baghdad na Salmin Swaggz, ambaye anaunda kundi la OMG na Lunya pamoja na Conboi.
Ikumbukwe chini ya RockStar Africa, moja ya ngoma za Young Lunya zilizofanya vizuri ni Stupid (2023) akishirikiana na Khaligraph Jones kutokea Kenya. Ngoma hiyo ilishinda tuzo mbili za TMA 2023 kama Wimbo Bora wa Hip Hop na Msanii Bora wa Hip Hop.