BSS yapata Top 10, fainali Julai 11
Muktasari:
- Akizungumza jana, Mkuu wa Channel ya Sinema Zetu wa Azam TV, Sophia Mgaza alisema maandalizi ya fainali yamekamilika na kila kitu kimewekwa sawa kuhakikisha mashabiki wanapata burudani ya kiwango cha juu.
WAANDAAJI wa shindano la BSS kwa kushirikiana na Azam Media wametangaza kuwa fainali kubwa ya shindano hilo itafanyika Julai 11, 2026, huku wakiwatambulisha rasmi washiriki 10 bora watakaowania taji hilo.
Akizungumza jana, Mkuu wa Channel ya Sinema Zetu wa Azam TV, Sophia Mgaza alisema maandalizi ya fainali yamekamilika na kila kitu kimewekwa sawa kuhakikisha mashabiki wanapata burudani ya kiwango cha juu.
“Azam imejipanga kuhakikisha inafanya tukio hilo kwa ukubwa ili kuwapa watazamaji na mashabiki wa sanaa pamoja na Azam TV burudani ya hali ya juu,” alisema Sophia.
Alieleza kuwa ingawa ukumbi wa fainali una uwezo wa kupokea watu takribani 2,000 pekee, waandaaji wameweka maandalizi yatakayowezesha mashabiki wengi zaidi kushuhudia tukio hilo kupitia matangazo ya mubashara.
“Ukumbi ni mdogo unaweza kupokea watu 2,000 pekee. Hata hivyo, mashabiki wataweza kufuatilia tukio hilo mubashara kupitia Sinema Zetu kwa kuwa tumeweka vifaa vyenye uwezo mkubwa wa kurusha matangazo,” aliongeza.
Mbali na kutangaza tarehe ya fainali, waandaaji pia waliwatambulisha rasmi washiriki wa BSS Top 10, huku wakiwapa nafasi ya kuzungumza na vyombo vya habari na kuwaomba Watanzania kuendelea kuwaunga mkono kwa kuwapa kura.
Vilevile wadau na washirika wa shindano hilo walitambulishwa sambamba na kutolewa kwa taarifa mbalimbali kuhusu maandalizi ya usiku wa fainali, ambao unatarajiwa kuwa kilele cha msimu wa mwaka huu wa BSS.