Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Imbeju Sauti Moja kunogesha CRDB Bank International Marathon 2026

Muktasari:

  • Mashindano hayo yatapambwa na  uzinduzi wa tamasha jipya la kimataifa la burudani lijulikanalo kama IMBEJU Sauti Moja.

BENKI ya CRDB kupitia kampuni tanzu yake ya CRDB Bank Foundation, imezindua rasmi msimu wa saba wa CRDB Bank International Marathon 2026, utakaofanyika Agosti 2026 katika viwanja vya TTCL Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yatapambwa na  uzinduzi wa tamasha jipya la kimataifa la burudani lijulikanalo kama IMBEJU Sauti Moja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Mussa Nsekela, alisema ubunifu huu unaendana na mkakati wa benki wa kuunganisha mafanikio ya biashara na ustawi wa jamii.

Dk Nsekela alisema kupitia marathon na sasa IMBEJU Sauti Moja, wanaendelea kujenga jukwaa linalounganisha watu wa kada zote kutumia michezo, sanaa na rasilimali zao kubadili maisha ya Watanzania.

“Huu ni uwekezaji wa kimkakati kwa vijana na mustakabali wa taifa,”, alisema Dk Nsekela.

Aliongeza kuwa, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020, CRDB Bank Marathon imekuwa chombo muhimu cha kusaidia mamia ya watoto wenye matatizo ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na wanawake wenye ujauzito hatarishi wanaohudumiwa kwenye Hospitali ya CCBRT pamoja na kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia Programu ya IMBEJU inayotekelezwa na taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya CRDB.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alisema msimu huu unakuja na ubunifu mkubwa kwa kuunganisha michezo, burudani na maendeleo ya jamii katika jukwaa moja.

“Marathon hii si mbio pekee bali ni jitihada za kusambaza tabasamu, kuboresha maisha ya watoto, wanawake na vijana. Mwaka huu tunaongeza nguvu ya muziki kupitia tamasha la IMBEJU Sauti Moja ili kupanua zaidi wigo wa ushiriki na kuleta msukumo zaidi wa maendeleo kwa jamii,” alisema Tully.

Kwa mara ya kwanza, CRDB Bank International Marathon itageuka kuwa wikiendi kamili ya burudani na uwekezaji kwa jamii, kuanzia Agosti 1 hadi 14, litakapofanyika tamasha la IMBEJU Sauti Moja na kufuatiwa kuu ambalo ni mbio hizi za hisani.

Tamasha hilo linatarajiwa kupambwa na wasanii maarufu wa kimataifa akiwemo Trey Songz kutoka Marekani na wasanii wengine wakubwa Afrika na duniani watakaosindikizwa na wasanii mahiri wa Tanzania, hatua inayolenga kulifanya kuwa mojawapo ya matukio makubwa ya burudani barani Afrika.

IMBEJU Sauti Moja inalenga kuwa jukwaa la kukuza vipaji, ubunifu na fursa za kiuchumi kwa vijana huku ikichangia moja kwa moja katika mfuko uwezeshaji wa vijana, wanawake na makundi maalumu kupitia taasisi ya CRDB Bank Foundation.

Ili kushiriki katika msimu huu wa saba wa CRDB Bank Marathon, kila mmoja anatakiwa kujisajili kupitia tovuti ya: www.crdbbankfoundation.co.tz kwa gharama ya Sh50,000 kwa mtu mmoja na Sh45,000 kwa kila mmoja kwa kikundi cha watu wasiopungua 30.

Alisema kwa wanaopenda burudani itakayoshushwa kupitia Tamasha la IMBEJU Sauti Moja, kutakuwa na viingilio vya aina tofauti.

Tully alisema tiketi ya kawaida itapatikana kwa Sh60,000 lakini kwa watakaolipia mapema watapata punguzo la Sh10,000 hivyo kulipia Sh50,000 tu.

Pia tiketi ya VIP inayogharimu Sh150,000 kwa watakaolipa mapema watatoa Sh130,000 na ile ya meza maalumu yaani VVIP itapatikana kwa gharama ya kuanzia Sh5 milioni hadi Sh20 milioni.

“Baada ya uzinduzi huo, CRDB Bank Foundation inawaalika Watanzania, taasisi, kampuni na wadau mbalimbali kushiriki kwa wingi katika matukio yote mawili yanayounda CRDB Bank International Marathon kwa kuwa kila tiketi na usajili ni mchango wa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya jamii.

“Kila anayeshiriki anakuwa sehemu ya safari ya kusambaza tabasamu. Karibuni tushiriki kwa pamoja IMBEJU Sauti Moja na CRDB Bank Marathon 2026,” alisisitiza Tully.

Akieleza manufaa mengine yatakayopatikana katika mbio za mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, alisema: “Washiriki wote wataruhusiwa kufanya vipimo vya moyo bure katika kituo chochote cha JKCI.”

Msimu huu wa saba unatarajiwa kuwa mkubwa zaidi ukishirikisha wakimbiaji zaidi ya 16,000 hivyo kuendelea kuimarisha nafasi ya CRDB Bank Marathon kama moja ya matukio yanayokua kwa kasi duniani, huku ukichangia ustawi wa jamii, kukuza utalii na kujenga uchumi jumuishi.