Kwa hakika Usher kapata mke aisee

SIKU chache kabla ya Usher kutumbuiza katika onyesho lake la Super Bowl hapo Februari 8, 2024, staa huyo na mpenzi wake, Jennifer ‘Jenn’ Goicoechea walipata cheti cha ndoa huko Las Vegas, Marekani. 

Siku nne baadaye, vyanzo vingi vilithibitisha kwamba wawili hao waliokuwa pamoja tangu mwaka 2019 walifunga ndoa wikiendi hiyo wakiwa tayari wamejaliwa watoto wawili, Sovereign Bo (2020) na Sire Castrello (2021).

Hata hivyo, mshindi huyo wa Grammy ambaye jina lake halisi ni Usher Raymond IV, kabla ya kumuoa Goicoechea, alikuwa katika ndoa na Tameka Foster na kupata watoto wawili, Usher V na Naviyd Ely.

“Nina mpenzi mzuri, tuna nguvu ya ajabu. Nina furaha sana, nina bahati sana kuwa na rafiki kama yeye, si tu mpenzi, bali yeye ni rafiki yangu mkubwa na ninampenda sana,” alisema Usher akiongea na People katika mahojiano ya Novemba 2023.

Katika mahojiano mengine siku chache kabla ya wawili hao kufunga pingu za maisha, Usher alifunguka zaidi kuhusu kujitolea kwa Goicoechea na kusema unapopata mtu ambaye unajua ni mwaminifu, bila shaka ni heshima na furaha kuwa naye.

“Ni wazi tumejitolea kuishi maisha ya pamoja kwa sababu ya watoto wetu, haitakuwa jambo la ajabu kwetu kuoana. Tayari tumefanya jambo hapa. Unajua ninachosema? Kiukweli najisikia vizuri kuwa naye, na hiyo ni heshima,” alisema Usher.

Je, huyu anayezungumziwa na Usher ni nani hasa? Goicoechea ambaye alizaliwa na mama wa Kiitaliano na baba wa Puerto Rico, alikulia Miami. Kwa mujibu wa LinkedIn yake, alisomea sanaa katika Chuo Kikuu cha Full Sail huko Winter Park, Florida, kuanzia 2003.

Aliingia katika tasnia ya burudani akimsaidia mama yake, Barbara Goicoechea ambaye alikuwa Mkurugenzi wa ACT Productions tangu 1988. Kufanya kazi na mama yake kukampa Goicoechea nafasi ya kufanya kazi kama msaidizi wa mwimbaji Ciara.

Baadaye alifanya kazi ya kusimamia wasanii mbalimbali chini ya Boogs’N’Effect Management, kisha Januari 2014 akawa Mkurugenzi wa Rhythm & Soul, shirika lisilo la faida linalowasaidia watunzi wa nyimbo na wachapishaji kupata mirabaha ya kazi zao.

Akiwa amefanya kazi katika tasnia ya muziki kwa miaka mingi, Goicoechea alikutana na Usher mara kadhaa katika hafla mbalimbali kabla ya kuwa na uhusiano rasmi.

Tetesi za wawili hao kuwa pamoja zilianza pindi walipohudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Thomas huko Atlanta Juni 2019, kisha walikuja kuonekana wakibusiana nyuma ya jukwaa kwenye tamasha la Hollywood Bowl Oktoba 2019.

Desemba 2019, Usher na Goicoechea walijumuika kwenye sherehe ya miaka 50 ya kuzaliwa kwa Sean ‘Diddy’ Combs huko Los Angeles. Kwa mujibu wa The Atlanta Journal-Constitution, Usher pia alitumbuiza katika hafla hiyo iliyojaa mastaa kibao.

Septemba 4, 2020 Usher akiongea na Good Morning America, alithibitisha kuwa yeye na Goicoechea wanatajia mtoto wao wa kwanza. Wiki mbili baadaye wakajaliwa binti yao, Sovereign Bo, huku Usher akitoa taarifa hiyo Instagram siku chache baadaye.

“Tunajisikia kubarikiwa sana na kujawa na upendo kwa kuzaliwa kwa mtoto wetu msichana mzuri, Sovereign Bo Raymond,” aliandika katika Instagram mwimbaji huyo wa kibao maarufu, Yeah! (2004).

Wakati wa hafla ya tuzo za muziki za iHeartRadio mnamo Mei 2021 ambazo Usher alikuwa mshereheshaji, Goicoechea akiwa amevalia gauni jeusi, alimuonyesha mtoto wao na kutangaza kuwa wanatarajia mtoto mwingine siku sio nyingi.

Mtoto wao wa kiume, Sire Castrello alizaliwa Septemba 29, 2021, Usher alitangaza kuzaliwa kwake mwezi uliofuata, huku Goicoechea akieleza sababu ya kumpa mwanae jina la Castrello.

Goicoechea alisema Castrello alikuwa ni babu yake ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 105. Alifariki muda mfupi kabla ya kujifungua kwake, ndipo akaona sio vibaya kumpa mtoto wake jina hilo.

“Champ alikuwa mtu hodari zaidi, shujaa, mcheshi, mkarimu na kielelezo cha familia, ndivyo nilivyomjua. Nisingeweza kuuliza mfano bora wa jinsi mwanaume anapaswa kuwa! Alikuwa mfano bora, hivyo ni sawa tu kuendelea kuweka jina lake hai,” alisema Goicoechea.

Mei 13, 2023, Chuo cha Muziki cha Berklee huko Boston kilimkabidhi Usher shahada ya heshima ya udaktari. Goicoechea alikuwa miongoni mwa waliohudhuria na kumpongeza kwa mafanikio hayo makubwa.

Wengine waliohudhuria ni mama yake Usher, Jonetta Patton, rafiki yake wa muda mrefu, Jermaine Dupri, kaka yake, J.Lack na watoto wake wawili wakubwa, Usher V na Naviyd Ely.