Kupata huduma ya mastaa hawa, uwe na mkwanja mnene...

Sunday July 31 2022
huduma pic
By Peter Akaro

Hakuna ubishi kuwa muziki wa Bongofleva umepiga hatua kubwa upande wa mauzo, wasanii wamekuwa wakitengeneza kiwango fulani cha fedha cha kuridhisha ila bado ni mapema kusema wanavuna zaidi. Hawa ni miongoni mwao;


1. Diamond Platnumz - Sh162 milioni

Hadi kufikia mwaka 2017 Diamond Platnumz alitangaza kutoza Sh100 milioni kwa shoo kiasi cha kutofanya shoo nyingi za ndani ya nchi, huku mapromota wa ndani wakimlalamikia kuwa anatoza fedha nyingi. Kufika Julai 2021 Meneja wa Diamond na WCB Wasafi kwa ujumla, Sallam SK alitangaza kuwa Diamond anatoza Dola70,000, wastani wa Sh162.5 milioni kwa shoo za nje ambazo ndizo hasa msanii huyo amekuwa akizifanya ukilinganisha na za ndani.


2. Harmonize - Sh58 milioni

Advertisement

Akiwa na takribani miaka saba tangu atoke kimuziki, mwimbaji huyo wa Konde Music Worldwide thamani yake katika soko kwa shoo za ndani ni Sh57 milioni, huku akiwa na rekodi ya kuandaa zake binafsi nyingi zaidi. Harmonize alibainisha hilo Desemba 2020 akiwa kwenye jukwaa la shoo ‘Life is Breeze’ Dar es Salaam ambapo alisema malipo yake kwa shoo moja si chini ya Dola25,000, wastani wa Sh58.0 milioni, alisisitiza kila sehemu utakayomuona akitumbuiza jua kalipwa kiasi hicho.


3. Zuchu - Sh46 milioni

Baada ya miezi minne ndani ya Bongofleva tangu atoke kimuziki, WCB Wasafi aliweka wazi kuwa Zuchu anatoza Sh20 milioni kwa shoo, ni kipindi ambacho alikuwa bado hajaachia nyimbo zake kali kama ‘Cheche’, ‘Litawachoma’, ‘Sukari’ na ‘Nyumba Ndogo’. Mwaka mmoja baadaye, Sallam Sk akasema thamani ya Zuchu katika soko imepanda, hivyo anatoza Dola20,000, wastani wa Sh46.4 milioni kwa shoo za nje, na za ndani ikiwa ni Dola15,000, wastani wa Sh34.8 milioni.


4. Barnaba - Sh23 milioni

Mkali huyo wa kuimba na Live Band ameweka wazi anachukua kati ya Dola10,000 hadi Dola20,000, wastani wa Sh23.3 milioni na Sh46.6 milioni ila bei itategemea na mteja wake atampa nini cha zaida nje ya fedha. “Inaweza kubadilika, inategemea ni kitu gani ninafaidika nacho kwako, unaweza kunipa fedha ndogo lakini fursa ua uwanja unaonipa ni mkubwa kuliko hiyo fedha unayonilipa,” alisema Barnaba.


5. Marioo - Sh20 milioni

Mara baada ya kumaliza kutumbuiza kwenye tamasha la Simba Day, Septemba 2021 na kufanya vizuri, Marioo alisema kuwa anatoza Sh20 milioni kwa shoo na hawezi kuchukua chini ya hapo.

6. Saraphina - Sh10 milioni

Huyu ni mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2018, kwa kipindi cha miaka miwili sasa amekuwa akifanya vizuri, ni miongoni mwa wasanii wachache wa Bongofleva waliopata nafasi ya kutumbuiza kwenye maonyesho ya Dubai Expo 2020, Falme za Kiarabu (UAE).

Meneja wake, D-Fighter, Machi 2022 alikaririwa akisema msanii huyo anatoza Sh10 milioni kwa shoo kwa sababu hawezi kutumbuiza bila kuwa na wachezaji ambao anatakiwa kuwalipa na gharama za maandalizi.


7. Mabantu - Sh10 milioni

Kundi hili linaloundwa na wasanii wawili wao wamesema chini ya Sh10 milioni hawapandi jukwaani kabisa kutokana na ukubwa muziki wao kwa sasa katika soko, ila itategemea na aina ya shoo. Mbali na hiyo ikiwa ni shoo ya mkoani, yaani nje ya Dar es Salaam, basi waandaaji wanapaswa kuwakatia tiketi tano za ndege ambazo mbili za kwao, tatu za meneja, mpiga picha na mlinzi au prodyuza wao.


8. Kusah - Sh5 milioni

Mwimbaji huyu hajataja kiwango rasmi cha malipo yake ila chini ya Sh5 milioni huwezi kupata huduma yake kama msanii kutokana na ngoma zake kufanya vizuri zaidi hivi karibuni.

Advertisement