Kuna cha kujifunza simulizi ya MC Pilipili
Muktasari:
- Ila shida kubwa ni kwetu binadamu ambao tumeumbwa kusahau imekuwa kama tabia kwamba tunapofikwa na matatizo huwa tunaumia na kujiambia mioyoni, tutabadilika ila baada ya muda mfupi tunaishi maisha yaleyale.
KWELI kesho ni fumbo, kulala na kuamka mambo yanaweza kubadilika. Kifo kinapotokea basi hakina taarifa, lakini huacha funzo kwa wale wanaosalia.
Ila shida kubwa ni kwetu binadamu ambao tumeumbwa kusahau imekuwa kama tabia kwamba tunapofikwa na matatizo huwa tunaumia na kujiambia mioyoni, tutabadilika ila baada ya muda mfupi tunaishi maisha yaleyale.
Kwangu najifunza kuthamini upendo, muda na kutoa pongezi na moyo wa shukrani kwa yule anaenitendea mema, kwani kadri siku zinavyozidi kwenda nimegundua kifo hakina taarifa na anayekufa huwa haagi ni lini ataondoka.
Kwa pamoja tuchukue funzo la MC Pilipili. Muda na wakati kama huu alikuwa mzima na aliposti katika mitandao yake ya kijamii kama mimi na wewe tunavyofanya au tulivyofanya, lakini dakika tano zilikuwa nyingi pumzi yake kuendelea.
NINAVYOMFAHAMU
Ukiachilia mbali kuwa ‘MC wa taifa’ kama wengi wanavyomfahamu kwangu ni kaka na kati ya watu imara nikikumbuka 2020 nilimtia machoni kwa mara ya kwanza.
Akiwa mmoja kati ya kaka na kijana mchangamfu hakuonyesha umaarufu aliokuwa nao kwangu alinifanya nimuone mtu wa kawaida ili tuongee lugha moja.
Ilikuwa ni saa 7 mchana nikiwa nimetoka chuoni, Ilala Bungoni, Dar alifika zilipokuwa ofisi za Basata. Nje ya ofisi hizo kulikuwa na duka moja. Nikiwa kwenye hekaheka za mambo ya chuo aliniomba nimsaidie kusoma moja kati ya chapisho lake kama liko sawa.
Tukajikuta tunaanza kuzungumza kama watu ambao tunafahamiana kwa miaka kadhaa. Alikuwa ni mtu mnyenyekevu, mstaarabu na huwezi kuacha kumsikiliza kwa utulivu aliokuwa nao.
Hapo niligundua maisha ya mitandaoni ni tofauti na uhalisia kwani hakuwa kama mchekeshaji kama wengi walivyomfahamu.
Heshima aliyokuwa nayo kwa wanawake inakupa picha ya maisha yake halisi kwamba alikuwa mtu ambaye hana tamaa za ajabu ajabu.
Hakuchukua zaidi ya dakika 20 dukani hapo aliondoka na kuniacha mimi na waliokuwepo pale na furaha kutokana na ucheshi wake.
Mawasiliano yetu mpaka umauti unamfika yalikuwa ya kutiana moyo katika magumu ya kazi. Pia hakuacha kuniambia ‘pambana dogo maisha ni wewe’, na kunikumbusha kwamba ndoto kubwa inatimizwa na mambo madogo ambayo yakiunganishwa yanatimiza jambo kubwa.
Bila kusahau alinikumbusha kuishi na watu vizuri. Sitasahau wakati tunaongelea jambo fulani kuhusu mahusiano na watu akanisihi ‘usirudie kosa mara mbili’.
Alinifundisha kupambana na kuwa imara, lakini nisilie mbele za watu ninapoumia.
Kwangu atabaki kuwa kaka imara, mwenye hofu ya Mungu asiyewaza kuhusu watu wanaongea nini ila furaha na malengo yake kwanza pamoja na ibada.
Atabaki kuwa mfano mzuri wa kutokata tamaa. Kama utakumbuka alipotea kipindi flani lakini nilipomuuliza alisema ‘dogo najipanga nikirudi utafurahi, kwa sababu nikitoka zamu hii ndio sirudi tena kwenye ukimya’. Nikikaa naye au kuongea naye hata kwa muda mfupi tu lazima aniulize kuhusu hali ya wazazi. “Vick wazazi ndio wana baraka zako umewapigia leo, usikute una mawazo kwa sababu wao wamehuzunika hujawapigia leo”. Huo ulikuwa ni mfano mzuri wa mtoto mwenye upendo halisi kwa wazazi licha ya kwamba alimpoteza mama yake, lakini hakuacha kumtaja kwenye kila mahojiano kuwa anamkumbuka.
HISTORIA YAKE
MC Pilipili mwenye uso wa ucheshi kama kazi yake ilivyokuwa alizaliwa Mtaa wa Airport, Dodoma mjini Oktoba Mosi, 1985 akiwa mtoto wa pili wa Mathias Matebe na Bi Mariam Matebe.
Emmanuel alianza elimu ya msingi katika Shule ya Uwanja wa Ndege ambapo alisoma hadi darasa la nne na kuhamia Ipagala ambako alimalizia 2000.
Akiwa shule ya msingi alijihusisha na masuala ya u-ch-o-raji, uimbaji na hata ku-cheza muziki ingawa alikuwa na ndoto za kuwa mwandishi wa habari.
Baaada ya kumaliza darasa la saba alijiunga na Sekondari ya Dodoma 2001 ambapo ndoto za uandishi wa habari zilianza kufunikwa taratibu.
Akiwa sekondari kama ilivyo kawaida huwa kuna masomo ya kuchagua kutokana na tabia yake, mwalimu Kilela ambaye sasa ni marehemu alimshauri achukue somo la Sanaa za Jukwaani ambalo alilipenda na kufaulu kuliko mengine.
UCHEKESHAJI, USHEREHESHAJI
Alipendelea masuala ya sanaa hali iliyokifanya kipaji chake cha uchekeshaji kukua na hata kuanza kuwa ushereheshaji (MC) katika matukio mbalimbali wakati akiwa shuleni.
Aliendelea na kazi ya ushereheshaji hata alipoanza masomo ya kidato cha tano na sita katika Sekondari ya Jubilee mkoani Dodoma.
Pilipili amefanya kazi ya uchekeshaji na ushereheshaji katika nchi mbalimbali kama Kenya, Rwanda, Uganda na Afrika Kusini hali iliyomsaidia kujitangaza ndani na nje ya nchi kwani mashirika na kampuni mbalimbali zilikuwa zikimwita sana kuongoza sherehe na matukio.
SAFARI YAKE
Mwaka 2020 kurudi nyuma nyota yake iliangaza katika shughuli mbalimbali, japo makali yake yalipungua kwa muda mfupi kabla hajarejea tena hivi karibuni akionekana kujinoa upya katika tasnia yake.
Mwaka 2019 alifunga ndoa na Philomena Thadey Emmanuel na kubarikiwa mtoto wa kike aitwaye Elphina. Kupitia baadhi vyombo vya habari, MC Pilipili aliwahi kueleza kuwa na watoto watatu wote wa kike akiwataja kwa majina ya Mariam, Brianna na Elphina ambao alidai kuwapenda na kuwajali sana.
Mwaka 2020 alipata pigo kwa kumpoteza mama yake mzazi na maumivu hayo yalionekana wazi kupitia machungu aliyokuwa akiyashiriki katika mitandao ya kijamii. MC Pilipili alifariki dunia akiwa Dodoma ambako alikuwa katika maandalizi ya shughuli aliyotarajiwa kuisherehesha.
SIASA KIDOGO
Emmanuel Mathias maarufu MC Pilipili sio mchekeshaji tu ila alikuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alichokitumia katika kinyang’anyiro cha kuwania udiwani kwa kuchukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea Kata ya Tambukareli, Jimbo la Mtumba mkoani Dodoma, lakini hakufanikiwa kupita.
Mwaka huu haukuwa wa kwanza kwake kwani 2020 aliwahi kugombea ubunge, lakini pia hakufanikiwa kupita katika kinyang’anyiro hicho.
UCHUNGAJI
Miaka ya hivi karibuni MC Pilipili alifungua kanisa lililoitwa Love Church, lakini halikuweza kudumu.
Alipata elimu ya Biblia na uongozin wa kanisa, lakini muda mfupi alitangaza kuwa atakuwa anahudumu kupitia mitandao yake ya kijamii kwani kanisa limemshinda.
SHABIKI WA YANGA
MC Pilipili hakuwahi kuficha mapenzi yake na soka, huku akiwa shabiki mkubwa wa Yanga na muda mwingi aliishabikia, na hata kununua jezi za timu hiyo.
Aliwahi kubadili rangi ya nywele kama mmoja kati ya viungo wa Yanga, Pacome Zouzoua kuonyesha mapenzi yake kwa mchezaji huyo.
MTANGAZAJI
Mchekeshaji huyo pia aliwahi kuwa mtangazaji wa vipindi vya dini akiwa anatoa maudhui kuhusu neno la Mungu na kuwaombea watu.
Lakini miaka ya nyuma aliwahi kuwa na kipindi cha uchekeshaji ambacho kilipendwa kutokana na maudhui yake.