Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huu ni wakati wa kufufua nyimbo za komedi

Muktasari:

  • Hizi hazikuwa ngoma za wewe kusikiliza ili ujisikie hisia unazosikia ukisiliza ngoma za Amini wa THT - hapana. Hizi zilikuwa ni ngoma ambazo lengo lake kubwa lilikuwa ni kukufanya ufurahi na ucheke. Zilikuwa ni ngoma za komedi. Nasikitika kwamba kwa sasa muziki huu umepotea.

ZAMANI wakati kina Diamond wanaimba Kamwambie, kina Alikiba wanahitI na Cinderela na Barnaba na THT wanatoa ngoma zenye haki ya kuitwa muziki, Kingwendu alikuwa anatesa mtaani na ngoma yake ya Demu Mapepe, huku Masanja alikuwa na kawimbo maarufu kanaitwa Ninakataa Ugali wakati Bambo alikuwa ana goma linaloitwa Kitambi Noma.

Hizi hazikuwa ngoma za wewe kusikiliza ili ujisikie hisia unazosikia ukisiliza ngoma za Amini wa THT - hapana. Hizi zilikuwa ni ngoma ambazo lengo lake kubwa lilikuwa ni kukufanya ufurahi na ucheke. Zilikuwa ni ngoma za komedi. Nasikitika kwamba kwa sasa muziki huu umepotea.

Muziki wa komedi ulikuwa mkubwa Tanzania kiasi kwamba mpaka wasanii wakubwa walijaribu kuachia ngoma za aina hiyo. Alikiba alikuwa na wimbo wa kuitwa Usiniseme na humo ndani alikuwa anaimba kama jamaa anayependa sana kula. Jamaa anatembea na ndizi na pilipili mfukoni ili akikuta sherehe popote akae, ale. Mbaya zaidi yakipita na mayai ya kuchemsha anaagiza na kula na kuanza kuachia ushuzi. We' unadhani kama hujawahi kusikia hii ngoma nikikwambia kwamba Alikiba unayemjua wewe amewahi kuimba wimbo wa aina hiyo utakubali?

Muziki wa komedi ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ulimpa Godzila hiti ya 'La Kuchumpa'. Ndani ya La Kuchumpa hayati King wa Salasala alikuwa anaimba kama mshkaji anayemiliki bonge la buti na mistari yake ilikuwa inasema vitu kama vile "watu wanadhani buti nimelinunua Ulaya kumbe nimenunua buku jero Karume kwenye mitumba". Sehemu nyingine anasema "eti, usiku wanakuja wachawi kuniroga, lakini wanashindwa kuniroga wanadata wanapoona buti langu la kuchumpa". Ni wimbo wa ajabu, lakini umeimbwa vizuri na niamini mimi ilikuwa ukiusikiliza unafurahi na ulikuwa unashika namba moja kwenye TOP TEN za redio za Bongo.

Wasanii wa komedi waliokuwa wanafanya muziki walikuwa ni wengi sana ukiachana na Bambo, Kingwendu na Masanja ambao nimeshawataja hapo juu, pia Joti amewahi kuimba muziki wa komedi. Mzee Pembe amewahi kuimba muziki wa komedi, Sharo Milionea, Kitale na listi inaendelea na kuendelea.

Nashangaa kuona muziki huo umekufa kwa sababu binafsi. Naamini enzi hizi ndizo zilitakiwa kuwa enzi za muziki huo. Kwanza, enzi hizo ni enzi za teknolojia. Kurekodi muziki sio gharama tena na kila mtu mwenye laptop na kinasa sauti anaweza kurekodi kwa ubora mzuri. Na ukizingatia kwamba muziki huu ni wa komedi, pengine wala hauhitaji kurekodiwa kwenye studio kubwa kwa gharama za kujiumiza.

Pili, hizi ni enzi za 'content'. Video za vituko na vichekesho zimejaa Tiktok na Instagram kupita maelezo. Nyimbo kama hizi zingepata makazi kwenye hiyo mitandao na kutrendi kuliko kawaida. Mfano mzuri, Bambo na Kingwendu waliachia wimbo wa komedi majuzi kati ambao ulikimbiza sana kwenye mitandao. Wimbo unaitwa Nani Kajamba.

Nitafurahi kuona wasanii hususani wa komedi wanarudi kujaribu aina hii ya muziki kwa sababu uzuri wake ni kwamba, muziki huu unatupa mbadala wa nyimbo za kusikiliza tunapochoka kusikiliza amapiano za Wasafi na Konde Gang ambazo kutwa kucha zinatamba.