KOMEDI KICHEKO: Ommy Dimpoz awamwagia mamilioni tuzo uchekeshaji

Muktasari:
- Hafla ya uzinduzi huo ilifanyika juzi Jumatano kwenye Ukumbi wa Johari Rotana, Posta, Dar es Salaam na kuhudhuriuwa na wasanii mbalimbali wa vichekesho kutoka tasnia ya Bongo Movie.
NI kicheko kwa wasanii wa tasnia ya uchekeshaji baada ya kuzinduliwa kwa Tuzo za Ucheshi Tanzania (Tanzania Comedy Awards 2024/2025) zenye lengo la kutambua, kuenzi michango ya wasanii wa vichekesho nchini na zitatolewa Februari 14, 2025.
Hafla ya uzinduzi huo ilifanyika juzi Jumatano kwenye Ukumbi wa Johari Rotana, Posta, Dar es Salaam na kuhudhuriuwa na wasanii mbalimbali wa vichekesho kutoka tasnia ya Bongo Movie.
Tuzo hizo zinazotarajiwa kujumuisha vipengele mbalimbali zinatajwa zitawanyanyua kutokana na zawadi za pesa na mchekeshaji bora wa Kike na wa kiume watapata Sh20 milioni kila mmoja, huku mchekeshaji bora wa mwaka atapata Sh30 milioni na Sh5 milioni zitatolewa kwa kila kipengele kitakachotajwa.

MSIKIE OMMY DIMPOZ
Akizungumza kwenye hafla hiyo, muasisi wa tuzo hizo, msanii wa Bongo Fleva, Omary Nyembo 'Ommy Dimpoz' alisema ameanzisha tuzo hizo ili kuinua na kukuza tasnia ya ucheshi nchini na kutambua, kuenzi michango ya wasanii wa vichekesho na kuwapa motisha kutokana na mchango wao kwenye kuburudisha na kuelimisha jamii.
“Mimi napenda sana komedi lakini sikutaka kushika 'Mic' ili nichekeshe watu, ila niliona 'gap' kwenye tasnia hii ya uchekeshaji hasa upande wa tuzo. Mara nyingi wachekeshaji wamekuwa wakiwekwa Kwenye kipengele kimoja na mara zote amekuwa akishinda mtu mmoja. Hivyo nikaona ni muda sahihi wa kuanzisha tuzo hizi ili kuendelea Kuwapa motisha wachekeshaji wetu."
Ommy alisema jukumu zima la tuzo hizo amewaachia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania na yeye ni mdau mkubwa wa sanaa hiyo zaidi hata ya muziki.
"Labda niwaambie ambacho mlikuwa hamkijui, mimi napenda sana komedi kuliko muziki. Wakati naumwa kipindi kile, komedi ilikuwa inanipa faraja nilipokuwa kitandani muda wote. Nilikuwa naingia kwenye peji za wachekeshaji tofauti tofauti, nilikuwa naangalia nacheka napata faraja, yaani nilikuwa najisahau kama nilikuwa naumwa."
"Nilikuwa nafanyiwa upasuaji kila baada ya wiki mbili, sasa kuwaza huo upasuaji kwa sababu kuna fomu nilikuwa napewa ya kujaza, unaambiwa kabisa na wazungu operesheni ikienda vibaya unaweza kufa ikienda vizuri unaweza kupona. Sasa kwangu mimi kufanya kitu kama hiki cha tuzo ni kama komedi ilikuwa inanidai na huu ndiyo nimeona muda wa kuwalipa kwa faraja waliyokuwa wakinipa."
MCHAKATO ULIVYOANZA
"Huu mchakato wa tuzo nimeuanza tangu mwaka jana mwezi wa saba, niliwaita baadhi ya wachekeshaji tukafanya nao kikao, lengo langu lilikuwa niwasikie hili suala langu la tuzo watalipokea vipi na uzuri walilifurahia. Ndipo nikaona sasa niwashirikishe wadau wengine na Basata pamoja na Bodi ya Filamu na wakanipa ushirikiano mzuri hadi nikaona hili jambo bora niwaachie wao walisimamie."

BASATA, BODI YA FILAMU WAFUNGUKA
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Dk Kedmond Mapana alieleza namna walivyopokea wazo la msanii huyo anayetamba kwenye Bongo Fleva na nyimbo kama 'Zekete', 'Tupogo', 'Nitakupa', 'Nai Nqai' na nyigine nyingi, alivyoamua kuratibu na wao watakavyoliendesha kwani wameona ni jambo zuri na wamelipokea na wanampongeza kwa hilo.
"Ommy Dimpoz alipotuletea suala hili la tuzo, tulilipokea na kujadiliana, tukasema kwa kuwa ni suala lililoletwa na wadau wenyewe na wasanii wenyewe, basi tulipokee na kulifanya kuwa endelevu sababu watakuwa na uchungu nalo na Serikali itatoa bajeti ya tuzo hizo kwani ni kitu kizuri kinafanyika."
Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dk Gervas Kasiga alisema; "Kwanza nampongeza sana Ommy Dimpozi kwa kuandaa tuzo hizi, amefanya kitu kizuri sana. Niseme tu baada ya kufanyika kwa tuzo hizo kutakuwa na muendelezo wa kutoa tuzo ya kumtambua msanii wa ucheshi atakayefanya vizuri kila mwezi. Sambamba na hilo, Bodi ya Filamu itaratibu utolewaji wa mafunzo kwa wasanii wa ucheshi kwa lengo la kuwaongezea weledi wa utendaji kazi na kufungua milango ya kimataifa."
WASANII WAFURAHIA, WAPONGEZA
Kwa upande wa wasanii wa vichekesho, walitoa maoni yao kuhusu tuzo hizo huku wakimpongeza Ommy Dimpoz kwa kuziandaa kwani zitaonyesha thamani kubwa kwa wachekeshaji kutokana na mchango wao katika kuburudisha na kuelimisha jamii na wamelipokea vizuri.
Joti alisema; "Kwanza nampongea sana Ommy Dimpoz kwa kutuletea tuzo hizi, pia niwape hongera sana wachekeshaji wanaochipukia kwa kukutana na bahati hii.
"Tuzo hizi ni moja ya kupewa heshima kubwa sana sisi wachekeshaji, kwani hapo nyuma ilikuwa ili mtu uchekeshe basi unapewa nafasi ya ulinzi kufungua geti kwenye tamthili ilimradi tu uchekeshe. Lakini kajitokeza mtu kama hivi Ommy Dimpoz na kushirikiana na serikali imezidi kutupa nguvu kuwa sasa thamani yetu imeongezeka na mimi sio kama nimetosheka, niseme tu nitakuwa mmoja wa washiriki na sitaangalia ni mkongwe hapana, bado mbichi kabisa mimi na nahitaji kupata pesa kama wengine."

Kingwendu
"Mimi kwanza nitoe shukrani zangu kwa mwandaaji wa tuzo hizi, Ommy Dimpoz akishirikiana na serikali, pili nisisitize umuhimu wa kuthamini sanaa ya uchekeshaji na mchango wake katika kuelimisha na kuburudisha jamii uzidi kuongezeka kama hivi, sababu wengine tumeanza kwenye hizi sanaa za uchekeshaji kukiwa hakuna haya mambo tunayoambiwa leo ya tuzo, ila sasa tumeonekana na katika hizo tuzo ndani yake kuna pesa, yaani kwa sasa hivi mtu ukipata pesa kati ya hizo zilizotajwa fasta unakimbilia kununua kiwanja na kujenga chumba kimoja hata kwa milioni 5. Hivyo Tuzo hizi zina faida sana na ni za kuziheshimu sana tupambane ili tuwe washindi."

Bambo
"Mimi nasema tunapokwenda ni pazuri, tulianza kuchekesha familia zetu nyumbani, tukatoka mitaani, tukafika majukwani basi ikawa vurugu mechi, nimpongeze Ommy Dimpoz kwa kufanya hiki kitu kizuri maana hatukutegemea kama siku tutaitwa na kuambiwa tutafanyiwa jambo kama hilo zuri, ni jambo la kushuru sana kwa sisi wachekeshaji."
Mzee Shayo
"Jamani kwanza niseme wajinga tumethaminika, wajinga tumeoneka, kwa Mungu hata wajinga wana thamani yao. Kwanza kabisa nimshukuru Ommy Dimpoz kwa hiki kitu alichokiandaa, kwanza hatukukitegemea, binasfi pia nimshukuru Coy Mzungu ambaye amesababisha 'comedian' wengi chipukizi kujulikana kutokana na ile 'Cheka Tu'. Hivyo ni wakati wa kuungana 'macomedian' wote hakuna haja ya kugombana, sijui hawa watu baki, hawa ni wa mitandao hapana, tuzipe heshima hizi tuzo."
Nanga
"Nimefurahishwa sana na hili jambo na hadi unaona huu muitiko mwingi wa wachekeshaji hivi, basi jua jambo hili limepokelewa vizuri, Ommy Dimpoz ameleta kitu kizuri sana na kuipa thamani kubwa sana sanaa ya uchekeshaji."
VIPENGELE TUZO ZA UCHEKESHAJI
Kasiga alivitaja vipengele vinavyowaniwa ni 17 ambavyo ni;
- Best male comedian of the year
- Best female comedian of the year
- Best Comedian of the year
- Best comic actor of the year
- Best comic actress of the year
- Best Comedy Presenter of the year
- Best female stand up comedian
- Best male stand up comedian
- Funny leader of the year
- Funny Kid of the year
- Best female social media comedian
- Best male social media comedian
- Best Chawa of the year
- Best Comedy Clip of the year,
- Best Collaboration Comedy clip
- Best Joke of the year