Kolabo kali zilizomfikisha Diamond kwa Alicia Keys

Sunday October 04 2020
mondii pic

HISTORIA inasema Diamond Platnumz ndiye msanii wa kwanza Tanzania kushirikishwa kwenye kolabo binafsi na msanii wa Marekani aliyewahi kuwa A LIST. Historia hiyo iliandikwa Septemba 18 baada ya mwanamuziki Alicia Keys kuachia albamu yake ambayo ndani ina wimbo aliomshirikisha Mondi.

Wimbo huo uliopewa jina la Wasted Energy ni wimbo namba 4 kati ya nyimbo 15 zinazopatikana kwenye albamu hiyo.

Hata hivyo, licha ya kwamba tukio hilo ni dalili nzuri kwa maendeleo ya muziki wetu, bado pia liliibua kasheshe kwenye mitandao ya kijamii baada ya mashabiki wa Diamond kulalamika kwenye ukurasa wa Alicia kwamba alimpotezea muda msanii wao kwa kumuimbisha kwa sekunde 20 tu kwenye wimbo huo.

Na baada ya kasi ya matusi na lugha kali kuongezeka, ilibidi Swizz Beatz, prodyuza wa muziki kutoka Marekani na mume wa Alicia Keys amtumie ujumbe Diamond akimuomba awatulize mashabiki wake kwa kuwaelezea kuwa kile kinachosikika kwenye wimbo alikichagua Diamond na kwamba kuna vitu vizuri zaidi vinakuja kutoka kwao.

Lakini sasa tuzungumze hatua ambazo Diamond alizipitia kwa miaka mingi ya muziki wake mpaka kufikia kwa Alicia na kuombwa kolabo. Kwa sababu ishu kubwa hapa sio tu Diamond kufanya kolabo na Alicia, bali ni Alicia kutaka kumshirikisha Diamond.

Moja ya mbinu kubwa iliyomsukuma Diamond mbali kimafanikio katika muziki ni collabo za nje ya Tanzania. Diamond amekuwa akifanya nyimbo na wasanii kutoka Nigeria, Afrika ya Kusini, Ufaransa na mpaka Marekani na kwa namna hiyo ndivyo ameweza kukuza jina lake nje ya mipaka.

Advertisement

Sasa katika makala haya tunaangazia kolabo zilizomletea matokeo makubwa na kumpandisha levo.

Number One Remix ft Davido

Mpaka 2013 Diamond alikuwa ni msanii mkubwa Tanzania, ilikuwa ni kama haiwezekani kukwepa stori zake. Ukienda huku anaongelewa penzi lake na Wema, ukirudi huku linazungumziwa bifu lake na prodyuza aliyemuibua Bob Junior. Lakini licha ya yote hayo, ustaa wake ulikuwa unaishia ndani ya nchi tu, bado alikuwa hajafanya kitu kikubwa nje ya mipaka.

Milango ya kimataifa ilifunguka mwanzoni mwa mwaka 2014 ambapo aliachia wimbo wa My Number One Remix akiwa amemshirikisha Davido kutoka nchini Nigeria, na baada ya hapo vitu vimekuwa bampa to bampa kwake.

Kwenye muziki wa Diamond, wimbo wa My Number One remix unabaki kuwa kama funguo iliyomfungilia mafanikio na kuliandika jina lake kwa ukubwa kwenye historia ya muziki wa Tanzania.

Nana ft Mr. Flavour

Ukitaka kuingia kwenye list ya wasanii wakubwa wa muziki Afrika, unatakiwa ulipeleke jina lako Afrika ya Magharibi hususan Nigeria, kisha jina lako lipambanishwe na list ndefu ya wasanii maarufu, kina Davido, Wizkid, Tiwa Savage na wengine.

Diamond alipogundua hilo akajaribu kutoa nyimbo kadhaa akishirikisha wasanii wa Nigeria. Wimbo kama Bum Bum aliomshirikisha Iyanya ni miongoni mwa ngoma hizo — hata hivyo zote hazikumpa ukubwa.

Mwaka 2015 akaachia wimbo wake wa Nana akiwa amemshirikisha Mr. Flavour kutoka Nigeria. Wimbo ambao kwanza ulimuingiza rasmi kwenye list ya wasanii wakubwa wa muziki Afrika na baada ya hapo Wanigeria wakaanza kumgombania kumshirikisha kwenye kazi zao. Ngoma kama Love Boat ya KCEE na Nakupenda ya Iyanya zimekuja baada ya kolabo hiyo.

Make Me Sing ft A.K.A

Muziki wa kiafrika uko sehemu tatu, Afrika Mashariki, Magharibi na Kusini — upande wa Kaskazini wenyewe wana aina yao ya muziki ambayo ina utofauti sana na huku kwingine.

Sasa mpaka kufika mwaka 2015 Diamond alikuwa ni mwenyeji Afrika ya Magharibi, wakati kwa hapa Afrika ya Mashariki ilikuwa ni nyumbani kwake kabisa, na kwa Afrika ya Kusini ilikuwa jina lake limepenya kidogo tu.

Sasa ili kujijenga zaidi, Diamond alitengeneza ngoma na rapa kutoka Afrika Kusini A.K.A, wimbo ambao waliuachia mwezi Februari mwaka 2016 na likawa bonge la hit lililomsambaza Diamond karibu Afrika yote — wimbo unaitwa Make Me Sing.

Marry You ft Ne-Yo

Baada ya kutosheka na Afrika, Diamond akaingia anga za kimataifa kwa maana ya kwamba kufanya muziki nje ya bara hili. Na ili kufanya hivyo, mwaka 2017 alifanya ngoma na msanii mkubwa kutoka Marekani Ne-Yo, wimbo unaitwa Marry You na tangu hapo milango ya kimataifa ikafunguka.

Baada ya Marry You, Diamond amefanya kolabo nyingine kibao na wasanii wakubwa wa Marakeni kabla ya kupewa dili na Alicia, wimbo kama Waka alioufanya na Rick Ross mwaka 2017 na African Beuaty aliomshirikisha Omarion ni baadhi ya ngoma hizo.

Kwa Alicia sasa

Kuna uwezekano mkubwa kwamba baada ya Wasted Energy, Diamond simu nyingi zaidi kutoka kwa wasanii Marekani wakimtaka aingize sauti kwenye ngoma zao. Au pia inawezekana akaitumia fursa aliyoipata kwa Alicia kuwaingia wasanii wengine kwa urahisi zaidi na kufanya nao kazi. Kwahiyo ni kama tukae mkao wa kula, tunaweza kusikia dude la Diamond Platnumz ft Chris Brown siku yoyote. Pengine. Usiondoke karata yako kwa ‘The Boy From Tandale’ kwa sababu kwa Simba lolote linaweza kutokea.

Advertisement