Kizimkazi Festival ni zaidi ya Tamasha

Muktasari:
- Tamasha hilo litafunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Agosti 18 likifanyika kwa siku saba huko Kizimkazi, visiwani Zanzibar.
Ni zaidi ya tamasha! Ndivyo unaweza kutamka wakati tamasha la nne la Kizimkazi likifunguliwa Jumapili ijayo mjini hapa, linatajwa kufungua fursa mbalimbali za kijamii, kimichezo na kiuchumi.
Tamasha hilo litafunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Agosti 18 likifanyika kwa siku saba huko Kizimkazi, visiwani Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Mahfoudh Said Omar, amesema mapema leo Jumapili kuwa, maandalizi yamekamilika na kwa siku saba litakuwa na matukio mbalimbali yaliyoandaliwa na wadhamini.
Mahfoudh amesema tamasha hilo lenye kauli mbiu ya 'Kizimkazi imeitika' litakuwa na programu mbalimbali zikitanguliwa na jogging itakayoanzia kwenye Uwanja wa Kizimkazi Dimbani hadi viwanja vya Kizimkazi Mkunguni kabla ya ufunguzi itakayoongozwa na Dk Mwinyi siku ya Agosti 18.
Siku hiyo inayodhaminiwa na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) itahusisha pia tukio la upimaji afya bure na badae usiku kutakuwa na shindano la taarabu asilia kabla ya kuendelea siku inayofuata kwa matukio mbalimbali.
Agosti 20, kutakuwa na tukio maalumu la uzinduzi wa skuli ya Dk Samia Suluhu Hassan na badae jioni ni bonanza maalumu litakalohusisha michezo ya bao, karata na soka ya ukufukweni ambayo ni michezo ya asili ya Kizimkazi.
Siku inayofuata ambayo ambayo imedhaminiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZTC) pamoja na mambo mengine kutafanyika mbio za baiskeli ambazo zitaanzia kwenye uwanja wa Maisara hadi Makunduchi zikiusisha wapiga pedeli wa ushindani, wazee na walemavu.
Kwa mujibu wa wadhamini siku hiyo, pia kutachezwa kabadi mchezo ambao Zanzibar imekuwa ikifanya vizuri kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na usiku kutakuwa na taarabu asilia.
Agosti 22 na 23 kutakuwa na mbio za ngalawa ambazo zitawapa fursa washindi kupewa boti za kisasa na pesa ili kuwafungulia fursa za kiuchumi sanjari na kuwekwa jiwe la msingi kwenye akademia ya Suluhu na itahitimishwa kwa mdahalo wa nishati safi.
Funga kazi ni Agosti 24 ambayo kutakuwa na fainali ya mechi ya soka inayoendelea hivi sasa kwa timu 16 za Visiwani Zanzibar kuchuana kusaka tiketi ya fainali.
"Pia kutakuwa na uzinduzi wa Cafe ya Casa na burudani ya Bongo Flava," amesema Meneja Masoko wa TTCL, Janet Maega ambao ni moja ya wadhamini wa siku hiyo sanjari na Benki ya NBC.
Akizungumzia maandalizi ya tamasha, Mahfoudh amesema yapo katika hatua za mwisho ikiwamo kumtambulisha Balozi wao, Dotto 'Magari' Abdallah.
"Msimu huu tunatarajia kuwa na viongozi mbalimbali wa SMZ na wenzetu kutoka Bara wamehamasika kushiriki litakuwa ni kubwa zaidi ya misimu iliyopita," amesema.
Tamasha hilo lilianza mwaka 2016 likijulikana kama Siku ya Samia (Samia Day) kabla ya kubadilishwa na kuwa Kizimkazi Day na miaka minne iliyopita lilibadilishwa jina na kuitwa Tamasha la Kizimkazi.