Kisa derby Bifu la mastaa Bongo laanza upya

Saturday May 08 2021
siimba bifu pic

Leo Jumamosi, Simba na Yanga watakutana katika dimba la Mkapa, Dar es Salaam kwenye mchezo wa raundi ya pili ya Ligi Kuu baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa sare ya 1-1.

Mchezo huu unaibua tena vita vya kiburudani kwa baadhi ya mastaa Bongo ambao awali walikuwa na ‘bifu’ na pengine hadi sasa. Mmoja yupo Simba, mwingine Yanga, bila shaka tambo, majivuno, vijembe na mengineyo lazima viibuke kisa mtanange huu. Je, ni kina nani hao?


Diamond vs Harmonize

Hakuna ubishi Diamond Platnumz ni shabiki wa kutupwa wa Simba na ukizingatia anatumia pia jina hilo katika kazi yake ya muziki, anarudi tena katika ubishani na Harmonize ambaye ni shabiki wa Yanga.

konde bifu
Advertisement

Wawili hawa waliowahi kutoka na nyimbo za kuzisifu timu zao, wamekuwa katika vita vya maneno mtandaoni na hata kwenye nyimbo zao tangu pale Harmonize alipojitoa WCB Wasafi yake Diamond na kwenda kuanzisha lebo yake, Konde Music Worldwide.


Hamisa vs Kajala

Mwanamitindo Hamisa Mobeto ni shabiki wa Simba na ndiye aliyemtoa mwali (kombe) ndani na kumleta uwanjani katika fainali ya Simba Super Cup, bila shaka atatamani timu yake ishinde ili kumwacha mdomo wazi Kajala Masanja ambaye humwambii kitu kuhusu Yanga aisee.

Ikumbukwe wasanii hawa wa filamu pia waliingia katika bifu kali baada ya Kajala kumshutumu Hamisa ndiye aliyemchukua mtoto wake, Paula na kwenda kumkutanisha na Rayvanny hadi kusambaa mitandaoni video zisizo na maadili.


Idris Sultan vs

Billnass

Mchekeshaji Idris ambaye hivi karibuni aligonga vichwa vya habari baada ya kuonekana Netflix, atazidi kutamba endapo Simba itaifunga Yanga ambayo Billnass anaishabikia.

Chanzo cha bifu lao hakijawahi kujulikana ni kipi hasa, hivi karibuni Billnass kaponda muonekano wa Idris kwenye filamu ya Slay, huku Idris akijibu mapigo kwa kueleza Billnass kaachwa vibaya na mchumba wake, Nandy.


Baba Levo vs Mwijaku

Tayari Baba Levo ambaye ni shabiki wa Yanga amesema endapo timu yake itafungwa na Simba anayoishabikia Mwijaku ataacha kazi kwenye kituo cha redio cha Wasafi FM.

Wawili hao wanaofanya sanaa na utangazaji wa redio, wamekuwa katika vita vya maneno na Baba Levo anapambana na yeyote anayemshambulia Diamond, huku Mwijaku akifanya hivyo kwa Alikiba. Ikumbukwe Diamond na Alikiba ni mahasimu wa kimuziki.


Wema vs Zari

Miss Tanzania huyu kwa mwaka 2006 Wema Sepetu moyo wake umetekwa na Yanga, hapo hasikii wala haoni, ni zaidi ya mahaba niuwe. Je, lakini amani ya moyo wake itabaki salama ikiwa Simba inayoshabikiwa na Zari The Bosslady itashinda?

Jibu ni hapana, kutokana Zari ndiye aliyempokonya Diamond wake kipindi cha nyuma na kwenda kumzalia kabisa na watoto. Hilo lilileta bifu kubwa kati yao kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili hadi pale Hamisa alipoingia kati kabla ya Zari kuondoka kwenye maisha ya Diamond.

Ikumbukwe mastaa wengine wa kike Bongo wanaoishabiki Yanga ni Riyama Ally, Irene Uwoya, Malaika, Zamaradi Mketema, Jacqueline Wolper, huku Simba ikiwa na Flaviana Matata, Salama Jabir, Monalisa, Mboni Masimba, Zuchu na wengineo.

Imeandikwa na Peter Akaro

Advertisement