Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kisa cha Yamoto kinachowaanika wachepukaji kweupee

YA MOTO BAND

Muktasari:

Wimbo huo unasikika ukichezwa na kufurahiwa na wapenzi wa muziki katika maeneo mengi ukiwavutia watu wa rika na kada tofauti. Hii ni kuanzia jijini Dar es Salaam na kwingineko nchini.

MIONGONI mwa nyimbo zilizopata umaarufu mkubwa katika siku za hivi karibuni na kusambaa kama moto nyikani ni ‘Niseme Nisiseme’ wa Kundi la Ya Moto Band la jijini Dar es Salaam.

Wimbo huo unasikika ukichezwa na kufurahiwa na wapenzi wa muziki katika maeneo mengi ukiwavutia watu wa rika na kada tofauti. Hii ni kuanzia jijini Dar es Salaam na kwingineko nchini.

Maudhui yaliyomo ndani ya wimbo huo yamekuwa burudani tosha hasa kwenye vyombo vya usafiri kama vile daladala, bodaboda, mabasi ya mikoani na hata kwenye usafiri binafsi. Kwenye kumbi za burudani nako usiseme, hata majumbani pia unapigwa kama ilivyo kwenye vituo kadhaa vya redio na vile vya televisheni.

‘Hasara baba yule, Sadiki baba yule, Shukuru baba yule, baba huyo katoka kazini zawadi mkononi, kaleta na ungo usipate tabu ya kupeta mchele...Baba umerudi nipe soda nikaringishe huko nje...., ila babaa, mama na mjomba Jitu, leo wamepigana, wamemwaga maji kitandani kwako na shuka wamechana, wanachofanya kwenye mabano, nililia sana...”

Haya ni baadhi tu ya maneno yanayoimbwa katika wimbo huo wa aina yake unaoelezea jinsi gani jamii yetu ilivyokumbwa na jinamizi la mmomonyoko wa maadili na usaliti katika ndoa, tena mambo hayo yakifanyika mchana kweupe mbuzi wanakula majani.

Ya Moto Band, kundi lililokuja juu kwa kasi ya ajabu, katika wimbo huo wamebainisha na kutufumbua macho wakionyesha ni kwa jinsi gani baadhi ya wanandoa wasivyo waaminifu katika ndoa zao.

Pamoja na kwamba katika wimbo huo mhusika mkuu ni mke, anayewapanga, kuwaleta na kuwaingiza wanaume wa kila aina na kufanya nao tendo la ndoa chumbani kwake wakati mumewe akiwa kazini.

Bila shaka yoyote Ya Moto Band chini ya Mkubwa, Said Fella wamefanikiwa kutuonyesha ni namna gani wanandoa wengi (mke na mume) walivyokosa uadilifu.

Tena mbaya zaidi vitendo hivyo vinafanywa huku vikishuhudiwa na watoto wao wa kuwazaa, majirani na hata ndugu kwani wanavitumia vyumba, nyumba za kupanga na hata za familia kutenda na kutekeleza ushetani huo ambao siku hizi ni maarufu kwa jina la ‘Mchepuko’.

Kwa bahati nzuri katika hali inayoonyesha mabadiliko makubwa na ujasiri, Ya Moto si tu wameliona hilo bali pia wamejitoa katika ‘utumwa’ wa tungo za mapenzi ambazo zimekuwa zikisifia tu uzuri wa uhusiano, utumwa huu kwa kiasi kikubwa umewaelemea wasanii wa sasa wa muziki wa kizazi kipya.

Badala yake Ya Moto Band wameonyesha njia, wamewaanika wachepukaji kweupe kwani licha ya kuzungumzia mapenzi, pia wamejikita katika ukatili na tabia mbaya za ndani ya ndoa, mmoja wa wanandoa anasaliti kiapo.

Vikundi au wasanii mmoja mmoja kama kioo cha jamii wana wajibu wa kutunga nyimbo zinazokemea au kuzungumzia maeneo yanayoathiri ustawi na maendeleo ya taifa letu. Tabia ya ‘michepuko’ au ukahaba ni tatizo kubwa na madhara yake ni makubwa katika jamii kwani linaweza kusababisha ndoa kuvunjika na familia kuparaganyika, chanzo cha watoto wa mitaani.

Wasanii pia wanatakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya lugha, misemo, nahau katika kuwasilisha visa na mikasa. Hapa ni muhimu kuzingatia mwiko wa kutumia maneno yanayobughudhi na kuumiza masikioni ili kuzingatia maadili na tamaduni zetu.

Lakini wimbo huo licha ya kukubalika na kutamba, bado umepokewa kwa hisia tofauti na makundi mbalimbali ya kijamii.

Baadhi ya wasikilizaji wanahoji kama maudhui ya wimbo huo yanakidhi malengo ya kazi ya sanaa. Je, matumizi ya mtoto kama mhusika mmojawapo anayelia na kukerwa kwa yale anayoyaona kutendwa na mama yake pale baba yake anapokuwa kazini, yanakubalika katika fasihi simulizi hasa ukitilia maanani mila na desturi za Kiafrika?

Wapo wanaodai kwamba ingekuwa vizuri au ingeleta maana kubwa zaidi kama malalamiko hayo yangetolewa na shemeji au wifi kuliko ilivyo katika wimbo huo ambapo watoto ndiyo wamebeba uhusika katika malalamiko.

“Watoto wanahusika vipi katika uhusiano wa mapenzi ya baba na mama? Na je, ni sahihi kwa watoto wa Kiafrika kuyasema kwa mama au baba yale yanayotendwa na mmoja wao hasa yanayohusu uhusiano wa kimapenzi?” Anauliza Mayola Mayola wa Charambe, Mbagala, jijini Dar es Salaam.

“Je, watoto wakiachiwa wawataje hawara wa baba na mama zao, hali ya amani na utulivu katika familia itakuwaje?’”anaendelea kuuliza Mayola.

Bila shaka, sote tujiulize hili na tuone namna ya kukabiliana na changamoto hizo, lakini hakuna shaka yoyote kuwa kutingisha na kukubalika kwa wimbo huo, kunatokana na ubainishaji ulio wazi wa vitendo vichafu vinavyofanywa ndani ya jamii, mpaka watoto wanakuwa mashahidi. Ni ushahidi wa wazi kabisa jinsi maadili yalivyoporomoka katika jamiii.

Kisa cha ‘Niseme Nisiseme’ ni ushahidi tosha wa yale yanayotendeka katika baadhi ya nyumba zetu usiku na hata mchana.

Pamoja na kukubalika huko bado Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na wadau wengine, wana wajibu wa kupitia na kuzikagua nyimbo kama hizo ili kuyabaini mapungufu yanayoweza kuathiri imani, mila, desturi na tamaduni zetu.

Heko wana Ya moto Band, tunasubiri mengi kutoka kwenu katika kutuburudisha na kutuelimisha zaidi. Wito wangu punguzeni ukali wa maneno mnayoyatumia katika kufikisha ujumbe.

Mwisho rejea wimbo ‘Barua Kwa Mama’ (namba moja na mbili) wa Cosmas Thobia Chidumule wakati ule akiwa na Orchestra Mlimani Park ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ au ule wa ‘Edita’ uliotungwa na Hassan Rehani Bitchuka. Siku zijazo nitazichambua nyimbo hizo kwa undani.

0716 801987, [email protected]