Wivu tu ndiyo ulimfanya Madee kutoa ngoma, Hip Hop Haiuzi

Muktasari:
- Madee amefanya mengi katika huu muziki akitoa nyimbo zenye miondoko mbalimbali na baadaye kuanza kuwasimamia wasanii kupitia lebo yake, Manzee Music Baby (MMB). Fahamu zaidi.
KWA miaka zaidi ya 20 Madee amekuwa maarufu katika Bongo Fleva kutokana na muziki wake pamoja wasanii wenzake alioshirikiana nao katika kundi la Tip Top Connection lililoundwa na mastaa kibao waliovuma wakati huo.
Madee amefanya mengi katika huu muziki akitoa nyimbo zenye miondoko mbalimbali na baadaye kuanza kuwasimamia wasanii kupitia lebo yake, Manzee Music Baby (MMB). Fahamu zaidi.
1. Baada ya Madee kumweleza Abdul Bonge, MB Dogg ni msanii mzuri na anafanya vizuri mtaani kwenye zile shoo za uzinduzi wa Camp, ndipo Bonge akatoa ruhusa ajiunge Tip Top Connection baada ya kuridhika pia na uwezo wake.
Marehemu Abdul Bonge alimkubali sana MB Dogg kwa wakati huo na ndiye aliyelipia fedha ya kurekodi wimbo wake wa kwanza Bongo Records, pia alimfanya Bonge kujihusisha zaidi na muziki.
2. Wimbo wa Madee ‘Kazi Yake Mola’ aliutunga baada ya kifo cha kaka yake na Babu Tale, Ally Zungu, wimbo huo ndiyo uliobeba jina la albamu ya kwanza ya Madee na albamu hiyo ndiyo iliyompatia fedha za kununua kiwanja chake cha kwanza kwa Sh500,000.
3. Hadi sasa Madee anaamini vesi yake bora kwa muda wote ni ile aliyochana katika wimbo wa MB Dogg ‘Latifah’ unaopatikana kwenye albamu yake ya kwanza, Si Uliniambia (2005) yenye nyimbo 10.
Na Latifah ndiyo wimbo wa kwanza kwa MB Dogg kuachia chini ya Tip Top lakini tayari ulikuwa umesharekodi kitambo kabla ya kujiunga na kundi hilo, viongozi Tip Top walipousikia wakapendekeza ukarudiwe Bongo Records kwa P Funk Majani.
4. Siku ya kwanza ambayo Madee anampeleka MB Dogg Bongo Records kwa P Funk Majani, Kajala Masanja ndiye aliyewafungulia geti la kuingia ndani, studio iliyokuja kumtoa kimuziki na mengine sasa ni historia.
5. Marehemu Ngwea ndiye alitakiwa kuwepo kwenye wimbo wa MB Dogg ‘Latifah’ ila Majani ambaye ndiye mtayarishaji wa wimbo huo akamchugua Madee ambaye wakati huo alikuwa amefanya vizuri na nyimbo zake, Kazi Yake Mola na Yote Maisha.
6. Albamu nne kali kwa Madee ndani ya Bongo Fleva kwa muda wote ni Machozi Jasho na Damu (2001) ya Professor Jay, Ulimwengu Ndio Mama (2002) ya Jay Moe, A.K.A Mimi (2004) ya Ngwea na Love Sounds Different (2022) ya Barnaba.
7. Madee aliamua kumshirikisha Marehemu Godzilla katika wimbo wake ‘Game’ baada ya kumsikia Zilla ametaja sehemu anapotokea, yaani Manzese katika wimbo wake ‘Get off My Way’ uliyotayarishwa na Marco Chali.
8. Sio kwenye muziki bifu la Madee na Nay wa Mitego lilipoanzia, bali mtaani kwao, Manzese na wote walikuwa na kambi zao, Madee akiongoza kambi yake, World Camp Nakoz, huku Nay akiongoza Small Tiger.
9. Mtayarishaji muziki kutoka studio za Kama Kawa Records, Yudi alimgomea Madee kuhusu wimbo wake ‘Hip Hop Haiuzi ‘ kwa kuhofia utaleta shida na kumtaka asiutoe ila alipoupeleka Tip Top wakaamua kuuachia bila kumpa taarifa.
Baada ya wimbo huo kusikika, kundi la Manzese Crew walifika nyumbani kwa kina Madee kueleza kuchukizwa na wimbo huo kiasi cha kutaka kufanya fujo.
10. Na sababu ya Madee kuandika ngoma ‘Hip Hop Haiuzi’, ni kutokana na kuona kina MB Dogg wanapata fedha nyingi kwa mauzo ya albamu zao, ila yeye anapata kidogo, kila walipoenda kuchukua fedha za mauzo katika duka la kanda, wenzake wanabeba kibunda, yeye fedha ya mboga tu.