Prime
Khadija Kopa aanika ukweli ndoa ya Diamond na Zuchu

Muktasari:
- Khadija Kopa, ambaye ni mama mzazi wa Zuchu, amezungumza na Mwanaspoti akianza kupokea hongera aliyopewa kwa kuozesha, na baada ya hapo amesema ni kweli wawili hao wamefunga ndoa.
HUKU wasanii wa muziki wa bongofleva, Diamond Platnumz na Zuchu wakiendelea kugonga vichwa vya habari kwamba wamefunga ndoa na wengine wakihisi ni katika zile kiki zao za kimuziki, gwiji wa taarab nchini, Khadija Kopa, ameweka wazi ishu nzima.
Khadija Kopa, ambaye ni mama mzazi wa Zuchu, amezungumza na Mwanaspoti akianza kupokea hongera aliyopewa kwa kuozesha, na baada ya hapo amesema ni kweli wawili hao wamefunga ndoa.
"Ni kweli wamefunga ndoa, ila sio ya mkeka kama mitandao inavyosema, wale ni watu wazima wamekubaliana na kufunga ndoa ya halali," amesema Khadija Kopa.
Mwanaspoti lilimuuliza mkongwe huyo kama alipokea posa, mahari na kisha kuhudhiria ndoa hiyo ambapo amesema:
"Mimi sijawahi kupokea posa wala mahari ya Zuchu, na kwenye suala la ndoa mbona wanandoa wanaweza kuoana wenyewe na wakapeana mahari yao wao wenyewe, maana mahari anaweza hata kuchukua mwanamke mwenyewe, na kuhusu uwepo wa ndugu, ndoa haikutaka ndugu."
TUJIKUMBUSHE
Miezi mitatu iliyopita kulikuwa na fununu ya Zuchu kutolewa posa na Diamond ambapo madai yalizuka kwamba posa hiyo ilikataliwa na Khadija Kopa. Mwanaspoti lilimtafuta Khadija Kopa na kuzungumza naye juu ya madai hayo ambapo alisema:
"Kwanza niwaambie watu mambo ya ndoa huwa mpangaji ni Mungu na kuhusu habari za wazazi tumekataa barua ya posa hizo siyo taarifa za ukweli, sisi hatujaona barua yoyote kutoka kwa Diamond, zaidi ya kusikia tu huko mitandaoni.
"Halafu watu wanatakiwa waelewe hili, furaha ya Zuchu ndiyo furaha yangu na familia yake, sasa sisi tukatae posa kwa ajili ya nini? Maana hadi mipango ya posa hiyo inapangwa ni lazima mwanamke husika ajue, sasa kama wamekubaliana watoto, kwa nini wazazi wapinge?
"Tena sio tu barua ya posa kwa Diamond, sisi tunapokea barua ya mtu yeyote atakayehitaji kumposa Zuchu, kwa nini waseme Diamond tu? Kikubwa Zuhura (Zuchu) akikubali sisi hatuna pingamizi, ndoa ni heshima bana na ni jambo la kheri. Hivyo achana na wapiga midomo ya mitandaoni hao wanaongea tu."
Zuchu na Diamond inadaiwa ni wapenzi wa muda mrefu mbali na kufanya kazi ya muziki pamoja katika lebo ya WCB, huku kila mara wakidaiwa kutibuana na hata wiki iliyoisha Zuchu katika akaunti yake ya Instagram alifuta utambulisho wa kuwa ni mmoja wa wanamuziki wa lebo hiyo, swali ni kwamba ni kweli wawili hao wamefunga ndoa? Au kuna kitu kingine kinaendelea?