Jumbe kutoa wimbo ajali yake ya kujeruhiwa na kuku

Thursday November 19 2020
jumbe pic

ZIKIWA zimepita wiki mbili tangu mwanamuziki wa dansi, Hussein Jumbe, kupata ajali ya kuvunjika vidole baada ya kuota ndoto  anampiga mateke kuku, anatarajia kuachia nyimbo inayoelezea tukio hilo.

Katika ajali hiyo iliyotokea nyumbani kwake Temeke Vetenari jijini Dar es Salaam, Jumbe alivunjika vidole vinne vya miguu na kwenye maungio yanayounganisha  nyayo na mguu.

Akizungumza hayo katika mahojiano maalum na Mwanaspoti Online, iliyomtembelea kumjulia hali, amesema kutokana na ajali hiyo tayari ameingia studio kurekodi wimbo unaohusu tukio hilo.

Amesema wimbo huo wa kisa cha kuku anatarajia kuuachia wiki ijayo na ameupa jina la ‘Mazongizongi Ndotoni’.

“Katika nyimbo zote ninazoimba huwa ni matukio ya kweli yanayonitokea  mwenyewe au watu ninawafahamu hivyo ni utamaduni wangu na ndio maana hata katika hili nimeona nilitungie wimbo,”amesema Jumbe aliyewahi kutikisa na kibao cha ‘Siri’.

Akitolea mfano mwaka 1999 alipozushiwa kuwa amefariki, alitoa wimbo wa ‘Nachechemea’, kama haitoshi akiwa kwenye bendi ya Msondo, alitunga wimbo wa ‘Ajali’ ambao ulihusisha ajali aliyoipata aliyekuwa msanii wa bendi hiyo marehemu TX Moshi.

Advertisement

Mkasa wa ajali ulivyokuwa
Akielezea mkasa mzima ulivyokuwa wa ajali hiyo, amesema ilikuwa siku ya Jumamosi, akiwa amelala, aliota akiwa anaendesha baiskeli katika moja ya mtaa kijijini kwao.

Hata hivyo akiwa njiani alikutana na wasichana watatu na alipowakaribia aliwasikia wakisema mtu mwenyewe si ndio huyu na kuamua kupita kushoto ili kuwakwepa.

Wakati akiwa anafanya hivyo alikutana na mtoto akiwa ameshika manati na kumtishia kama kutaka kumpiga nayo na mara baada ya kumpita alipiga jiwe kwenye tairi la nyuma la baiskeli yake.

"Kitendo cha mtoto yule kupiga baiskeli yangu, kilinifanya nimrudie mtoto yule na kumuuliza kulikoni kabla sijamaliza,, akageuka kuku ambaye alikuja kuanza kupambana na mimi na ndipo hapa nikawa napambana naye kwa kumpiga mateke.

“Kumbe wakati najiona napigana na kuku, nilikuwa naupiga ukuta mateke jambo lililomshutua mke wangu kwa kuniona nikiwa katika hali ile ambapo aliniamsha na wakati huo nilikuwa nimetota mwili mzima na ndipo nikamuahadithia kuhusu ndoto hiyo,”amesema.

Anasema kulipokucha aliendelea na shughuli zake ikiwemo kwenda kwenye mazoezi, lakini siku iliyofuata maumivu yalizidi na hapo ndipo mke wake alimlazimisha aende hospitali kwa ajili ya matibabu na alipopigwa x-ray ndio akakutwa amevunjika vidole vinne.

___________________________________________________________

BY NASRA ABDALLAHAdvertisement