Jol Master: Kufeli elimu siyo kufeli maisha

Muktasari:

  • Kutokana na sanaa yake, Jol amejizolea mashabiki wengi hasa wanawake kwani vichekesho anavyofanya vinawahusu wao moja kwa moja.

‘From zero to hero’ ni msemo wa Kiingereza wenye kumaanisha ‘kutoka sifuri hadi shujaa’, msemo huu ndiyo unaweza kumuelezea mchekeshaji Juma Omary, maarufu kama Jol Master, ambaye licha ya kufeli kwenye mtihani wa kidato cha sita, amekuwa miongoni mwa wachekeshaji bora Tanzania ambao wanatumia kipaji chao kujipatia kipato.

Kutokana na sanaa yake, Jol amejizolea mashabiki wengi hasa wanawake kwani vichekesho anavyofanya vinawahusu wao moja kwa moja.

Akizungumza na Mwananchi, amesema vichekesho vyake huwa kwenye mtindo wa maisha halisi hasa ya wanawake kwani ndiyo mashabiki wake wakubwa.

“Mashabiki wangu wakubwa ni wadada na ndiyo watu ambao ukiwakamata utakuwa umekamata soko kubwa, kwa sababu wanawake wanapopenda kazi yangu ni rahisi kuwashawishi wapenzi wao waje kwenye shoo zangu,” alisema.

Kama ilivyo kwa wanamuziki kuandika nyimbo kabla ya kuingia studio na wengine kupata mistari baada ya kusikia biti ndivyo ilivyo kwa mchekeshaji huyu ambaye huandaa maudhui yake akiwa anatembea.

“Mimi naishi Makongo, mara nyingi huwa nachukua kofia yangu navaa inaficha sura, ili watu wasinitambue njiani, kisha naanza kutembea kutoka Makongo hadi Mlimani, huko naandaa vichekesho vyangu na nikirudi ninayafanya mazoezi mbele ya kioo ili kupata kilicho bora zaidi,” alisema.


Aeleza alivyoanza komedi

Kama ilivyo kawaida ya binadamu kukumbana na baadhi ya changamoto, ndivyo pia mchekeshaji huyu ambaye amewahi kukutana na changamoto ya kushindwa kuwachekesha watazamaji wake kipindi akiwa mwanafunzi.

“Nilivyokuwa darasa la sita au la tano nilienda kuchekesha baa na nguo za shule, nikamwambia yule dada wa pale naomba nichekeshe, nilienda nikafanya stand up comedy yangu ya kwanza, watu wameshalewa hawacheki wanasema tokaaaa! iliniuma sana lakini nikasema kuanzia hapo sitaacha kuchekesha,” alisema msanii huyo.


Kufeli shule

Mwigizaji huyu na mchekeshaji amefunguka kuwa hakufanikiwa kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu kutokana na kufeli akiwa kidato cha sita, shule ya Tambaza jijini Dar es Salaam.

“Mwaka 2020, nilikuwa nasoma HGE, nilipata sifuri Shule ya Tambaza, nilipata ziro iliyonyooka kabisa, siyo kama nilikuwa sina akili ni maisha niliyokuwa nayapitia kipindi kile nasoma, kulikuwa hakuna namna yoyote ya mimi kufaulu kilikuwa ni kipindi cha corona hakuna shoo, hakuna nini halafu geto nilipokuwa nakaa nilifukuzwa, kwa hiyo nilikuwa natafuta chakula tu na siyo shule.

“Nakumbuka mtu wa kwanza kumwambia ni mama kwa sababu ndiye kila kitu kwangu, alikuwa anaamini maisha yangu yatafanikiwa shuleni ile siku namwambia nina sifuri alimaindi sana.”

Alivyokutana na Lamata hadi kuingia Jua Kali

 Mwaka wa 2021, ni kama ulikuwa mwaka wa neema kwake baada ya kuwa mmoja kati ya waigizaji wa tamthilia ya Jua Kali ambayo anacheza kama mlinzi.

“Kwanza Lamata aliniona nikitumbuiza pale Cheka Tu akaniambia kuna namna fulani ananiona kwenye Jua Kali, tangu hapo nilianza kumsumbua kumtafuta, lakini siku moja nikiwa nyumbani alinipigia simu na kunitaka tukutane Mbezi.

“Nilipofika pale aliniambia kuwa naweza kuigiza baadhi ya matukio na angenilipa Sh 1 milioni, kwa wakati huo sikuwahi kupokea pesa nyingi kiasi hicho huko nyuma, hivyo niliipokea na kuanza kufanya kazi, thamani yangu ilianza kupanda,” alisema.

Mchekeshaji huyo ana shoo yake ya vichekesho inayotarajiwa kufanyika Kwenye Ukumbi wa Mlimani City kesho Jumamosi. Shoo hiyo imepewa jina la ‘Jol Master Comedy Special’.