JB, Gabo 'vitani' tuzo za filamu

Wasanii wanaotamba kwenye Bongo muvi, Salum Ahmed (Gabo) na Jacob Steven (JB) ni miongoni mwa nyota watano walioingia kwenye fainali ya kuwania tuzo ya muigizaji bora katika tamasha la tuzo litakalofanyika nchini Desemba 18.

Wengine ni John Kokolo, Sadam Nawanda na Isarito Mwakalindilie ambao watawania tuzo hiyo kwa wanaume.

Upande wa wanawake, watakaochuana ni Riyama Ali, Godliver Godian, Tishi Abdallah, Johari Thabiti na Christina Mroni.

Mjumbe wa kamati ya tuzo hizo, profesa Martin Mhando amesema, hiyo ni moja ya vipengere 28 vitakavyotoa washindi kwenye tamasha hilo lililopewa jina la Tanzania Festival Film Award.

Amesema baada ya mchujo, kila kipengere kilisalia na washiriki wasiozidi watano ambao wameingia fainali na kuanzia kesho Jumatano wataanza kupigiwa kura.

Meneja programu wa tuzo hizo kutoka Azam Media, Fatma Mohammed amesema filamu zote zilizopingia kwenye fainali zitaanza kuonyeshwa laivu kuanzia sasa kwenye chaneli ya Sinema zetu ili kuwapa fursa watazamaji kuzipigia kura kwa ubora na uhakika zaidi.

"Zitaonyeshwa kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 jioni na marudiao itakuwa ni kuanzia saa 4 usiku,' amesema.

"Ni muhimu watazamaji kuangalia filamu hizo ili wanapopiga kura iwe ni kura halali kabla ya fainali," alisema.

Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Eliya Mjatta alisema tuzo hizo ambazo msimu huu zimeandaliwa na Serikali ni hatua kubwa katika tasnia ya filamu nchini.

"Tumeridhika na kila hatua ya mchakato huu hadi sasa tumepata washiriki walioingia fainali, hakuna shaka fainali hii itakuwa ni moto," alisema.

Hata hivyo kipengere cha tuzo ya filamu ambayo inatangaza utamaduni wa Tanzania hakijapata washindani kufuatia filamu nyingi kutoigizwa kwa mahudhui hayo huku Profesa Martin akisisitiza kwamba katika kipengere hicho wamewaachia waandaaji wa filamu kama chalenji kwenye tuzo za mwakani.

"Pia kuna kipengere cha tuzo heshima kubwa katika filamu, hii bado haijapata mtu wa kuingia kwenye kipengere hicho," alisema.