Jay Melody anataka nini kupitia albamu yake mpya?

Muktasari:

  • Pia nilikuwa nalitaja jina lake kwa wanangu wote wa karibu. Utanisikia “oya, unamjua dogo mmoja anaitwa Jay Melody anaimba balaa. Ana ngoma inaitwa Goroka. Isikilize.”

Miaka fulani hapo nyuma kabla Jay Melody hajawa Jay Melody tunayemjua leo nilisikia baadhi ya ngoma zake nikajisemea mwenyewe kimoyomoyo “huyu dogo ni mtu hatari”. Na sikuishia hapo nyimbo zake ziliingia moja kwa moja kwenye ‘playlist’ yangu na nikawa shabiki wake tangu siku hiyo.

Pia nilikuwa nalitaja jina lake kwa wanangu wote wa karibu. Utanisikia “oya, unamjua dogo mmoja anaitwa Jay Melody anaimba balaa. Ana ngoma inaitwa Goroka. Isikilize.”

Baadaye alivyokuja kutoa Huba Hulu, watu wakaanza kumwelewa, nilijisikia furaha sana. Nilikuwa najiona kama mimi ndiye niliyesababisha Tanzania nzima imjue wakati usikute jina lake lenyewe nililitaja kwa watu wasiozidi hata 10.

Sasa Jay Melody hashikiki, ni bonge la msanii, anashirikishwa hadi na Simba la Masimba Dangote? Huyu ameshafika levo kubwa sana. Nyimbo zake zinapendwa mno, kule tiktok ngoma zake ‘zinafanyiwaga’ challenge kwa fujo sana. Mademu wanamkubali, harusini ngoma zake zote zinachezwa, dogo hana skendo, hana bifu na redio yoyote ile wala hayuko timu yoyote ile… kwa kifupi yuko sawa.

Wiki hii ameachia albamu yake inayoitwa Therapy yenye ngoma 14. Wakati nasikiliza albamu hiyo nilikuwa na maswali mengi sana na moja ya swali zito likiwa Jay Melody amelenga kupata nini kupitia albamu hii?

Kwa nini napata swali hili, kwa sababu kinachopatikana kwenye albamu hiyo tayari tumeshakiona sana kwa Jay Melody kwa zaidi ya miaka mitatu sasa. Nyimbo zote 14 kwenye albamu hiyo zinafanana kwa maana ya midundo inaendana, melody zinakaribiana, mada zinazoimbwa ndo zile zile na hata aina ya maneno ndo yale yale.

Nyimbo zote kwenye albamu hiyo zinafanana na nyimbo zake zilizopita. Hapa sitii chumvi, wala kunogesha stori, ninachokisema ndicho cha kweli, unaweza kwenda kusikiliza albamu na ukajionea.

Narudi kwenye swali langu, Je, Jay Melody alikuwa analenga kupata nini kupitia albamu hii? Je alitaka kuonyesha watu ana uwezo wa kutengeneza nyimbo moja na kuifanya ziwe nyimbo 14 na kuiita albamu? Kama alitaka kutuonyesha hilo, amefanikiwa.

Au pengine Jay Melody anataka kuitumia albamu hii kama daraja.

Kwamba muziki wa aina hii ndo ulifanya watu wampende zaidi. Basi ametupa mwingi wa kutosha kwa mara ya mwisho kisha avuke kwenda kwenye aina nyingine ya muziki. Kama lengo lake ndo hilo basi tunasuburi tuone.

Naamini Jay Melody ni msanii mzuri, pia amejikosesha fursa kubwa ya kutuonyesha uwezo wake kwa namna tofauti tofauti. Angeimba miondoko tofauti tofauti ya Bongo Fleva, angeimba kwenye midundo tofauti tofauti, angefanya kolabo za kutosha, angejaribu na wasanii wa nje hata wadogo… pengine angefanya hata baadhi ya niliyoyataja hapa albamu yake ingekuwa na maana zaidi.

Mwisho, muziki ni wake yeye na menejimenti yake, lakini kusema ukweli natabiri albamu hii haitakuwa na mashiko sana mtaani. Itapita na kwenda zake.