Prime
Ishu ya msosi yazua mambo sherehe ya Aziz KI, Hamisa Mobetto

Muktasari:
- Wawili hao waliooana Jumapili iliyopita Mbweni, ikiwa ni siku moja tangu kufanyika kwa tukio la utolewaji wa mahari, walipongezwa katika sherehe kubwa iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Super Dom Masaki na kuhudhuriwa na mastaa mbalimbali.
ILIKUWA bab'kubwa. Ndivyo ilivyokuwa katika sherehe ya kupongezwa kwa maharusi, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI na mwanamitindo, Hamisa Mobetto iliyofanyika juzi usiku, jijini Dar es Salaam.
Wawili hao waliooana Jumapili iliyopita Mbweni, ikiwa ni siku moja tangu kufanyika kwa tukio la utolewaji wa mahari, walipongezwa katika sherehe kubwa iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Super Dom Masaki na kuhudhuriwa na mastaa mbalimbali.
Miongoni mwa waliohudhuria sherehe hiyo iliyopambwa na burudani ya muziki wa Bongo Fleva na taarabu ni pamoja na wachezaji wa soka, wanamitindo, wabunifu wa mavazi na watu wengine mashuhuri na licha ya kuwa na idadi ya watu wanaoweza kuhesabika kwa urahhisi, lakini sherehe ilifana na Mwanaspoti inakuletea baadhi ya yaliyojiri ukumbini.
WEMA, WOLPER NDANI
Kati ya mastaa wa Bongo Movie waliotoa sapraizi kwenye harusi hiyo ni Wema Sepetu na Faustina Charles Mfinanga 'Nandy' huku wasanii wengine pia wakijitokeza ukumbini hapo.
Wasanii hao ni pamoja na Marioo na mchumba wake Paula, Lulu Diva, Jackline Wolper, Masha Love, Gigy Money, Christian Bella, Gabo ze Gamba, Mzee Yusuf na mkewe Leila Rashid, Husna Sajenti, wabunifu wa mavazi Khadija Mwanamboka na Martin Kadinda.
Katika usiku huo, Wema aliyeingia na Wolper alionekana kupendeza na akivalia gauni la rangi ya bluu bahari la mtindo wa nguva, huku Wolper akiwa amevalia vazi la kawaida lililokuwa limetobolewa shingo tu na mkoba wake mkubwa.
AMPA NENO HAMISA
Wema ambaye anasema alichelewa kujua uhusiano wa wawili hao anamshauri Hamisa aondoke kwenye ndoa akiona mambo siyo na kukosa furaha.
"Nilipoanza kuona uhusiano wa karibu sana wake na Aziz ki, nilimuuliza Hamisa kama ni wapenzi ila alinificha, lakini baada ya muda kupita ilibidi aniambie ukweli huku akiniambia anaolewa naye," amesema Wema Sepetu.
"Mimi namtakiwa kila la Kheri Hamisa Mobetto kwenye ndoa yake, nampenda sana ila kuna kipindi alitaka kuingia kwenye mfumo wa watu wagombanishi ili tugombane, huyu ni mdogo wangu nilimuita na kumwambia aachane na habari za mitandaoni kwani zinampotezea watu wake wa karibu wengi."
NANDY ASHTUA
Kwa upande wa Nandy, aliibua mshangao kwa baadhi ya waalikwa baada ya kutajwa na MC Gara B kutumbuiza maharusi na wageni na aliimba wimbo wa 'Dah' aliomshirikisha Ali Kiba.
Mshangao na minong'ono iliibuka kwani wengi wanajua Nandy na Hamisa wana bifu bila kujua kama tofauti zao zilikwisha.
Mmoja alisikika akisema "Hee...jamani kumbe Nandy kweli, afadhali kama bifu lao limeisha hii ni nzuri sana, wamefanya jambo la maana sana kupatana."
Mwingine akasikika; "Haya ndiyo mambo tuliyokuwa tunataka, ndiyo maana tuliambiwa leo kwnenye hii sherehe kutakuwa na sapraiz kumbe ni Nandy kuja kwa Hamisa Mobetto ambaye watu wengi wanajua hawana maelewano."
ikumbukwe bifu la wawili hao lilitokana na ukaribu wa Nandy kwa Diamond Platnumz mara tu baada ya Hamisa kuachana na mkali huyo wa Bongo Fleva, na kuishia kutupiana vijembe mitandaoni tangu mwaka 2019.

NYOTA YANGA WAMPAMBA AZIZ KI
Wachezaji wa Yanga wa kigeni wakiongozwa na Khalid Aucho, Kennedy Musonda, Yao Kouassi, Pacome Zouzoua pamoja na wazawa kama Clement Mzize, Kibwana Shomary, Denis Nkane, Bakari Mwamnyeto walionyesha sapoti ya hali ya juu kwa nyota mwenzao na walimsindikiza kuingia ukumbini huku wakiimba na kucheza naye.
Katika tukio lingine, Ali Kamwe, Priva Abiudi 'Privaldinho' pamoja na Haji Manara na mke wake Zaylissa na wafanyakazi wengine wa klabu hiyo wakiongozwa na Rais Injinia Hersi Said waliipamba sherehe, huku pia Mzee Yusuph akifungua kwa dua huku pia akiwatakia mema maharusi na waalikwa.
"Leo ni jambo la furaha kwa maharusi wetu Aziz Ki na Hamisa Mobetto, wamefanya jambo la kheri kufunga ndoa hivyo tunawajibu kuwapongeza siku ya leo na sio kuwabeza."
"Sio kukaa kuwazungumzia tofauti ikiwa wamefanya jambo la maana, nasema na wale walioshindwa kuingia ukumbini waombe heri waache roho za kwa nini," alisema Mzee Yusufu.
NGUO ZA MAHARUSI MARA MBILI
Moja ya mambo yaliyovutia waalikwa ukumbini ni mavazi ya bwana na bibi harusi na awali waliingia ukumbini wakiwa wamevalia meupe kabla ya baadaye kubadilisha na kuvalia ya rangi ya bluu bahari.
Jambo hilo lilifanyika licha ya kuwa muda haukutosha kwa sababu ya muda kuwa mchache, hata hivyo MC alijaribu kupeleka mambo haraka ili kutokuchosha watu ambao pamoja na kucumilia kusubiri maharusi walioingia ukumbini saa 6 usiku, lakini walifurahia shughuli hiyo iliyofana.
MAMA HAMISA AFUNGUKA AFYA YAKE, NG'OMBE WA MAHARI
Baada ya kuonekana kwenye ndoa ya mwanae kulizuka zogo juu ya mwili wa mama hamisa, Shufaa Lutenga na mwenyewe amesema wala watu wasishtuke, hiyo ni 'surgery' kupunguza mwili.
"Naona watu wengi wananishangaa mwili wangu kupungua, kila mtu anasema lake ila hawajui kama mimi nimepunguza mwili 'surgery' na hapa hata kidonda hakijapona vizuri," alisema na kuongeza kwa sasa mwili alionao ndiyo anaoupenda kwani wa awali ulikuwa ukimsababishia presha, miguu kuuma na uvivu wa kufanya jambo.
Kuhusu mahari ya ng'ombe waliotolewa amesema wengi wanapotosha kwenye mitandao ya kijamii wakidai ni 30 na wamekodishwa lakini ukweli ni ng'ombe 150 pamoja na pesa na mkwe wake Aziz KI ametoa vyote.
“Nadhani ilikuwa mubashara jamani kila mtu ameona ng’ombe wale wamesimama. Ng’ombe walikuwa nadhani malori mawili na walienda kwa mamangu.”
“Sijawahesabu kwa sababu unajua nilikuwa kwenye furaha na mihemko lakini ng’ombe tuliokubaliana nao ni 100. Unajua ng’ombe mmoja mzima ni Sh3.5 milioni, lakini wao walileta ng’ombe kama 150, wengine walipelekwa kwa mama, wale walioonekana pale ni wachache," alisema mama Hamisa.

MSIKIE GIGY MONEY KUHUSU NDOA YAKE
Gift Stanford 'Gigy Money' baada ya kushuhudia ndoa na harusi hiyo iliyofana, alisema licha ya kwamba kwa sasa hayuko tayari kuolewa ila anataka mahari ya Msahafu tu.
Amesema mahari ya ng'ombe sawa ila atawatafuna wote na asiwe na kumbukumbuku, ila msahafu utabaki kama kumbukumbu.
"Mie kuolewa bado sana, ila muda ukifika, nikipata bwana wa Kiislamu nitaolewa na Msahafu tu, mie sitaki mambo mengi maisha yenyewe haya.
"Nikwambie kitu kimoja, kwenye mapenzi kikubwa ni kupendana na kuheshimiana, zaidi ya hapo vitu vingine ni mbwembwe tu za Dunia," amesema Gigy.

CHAKULA DAH!
Katika hali isiyokuwa ya kawaida kuna baadhi ya waalikwa walikosa chakula na hata muda wenyewe wa kula ulishangaza na ilikuwa saa 9 usiku.
Baadhi ya wageni waalikwa na wachezaji wa Yanga waliinuka kwenda nje kutafuta chakula, hata hivyo muda ulikuwa umeenda hadi saa 8 usiku na ilibidi waalikwa waamue k8ujitafutia wenyewe kabla ya kuinuliwa kwenda kula na wengine walikosa baada ya chakula kuisha.

UKIKOSA KITI UNASIMAMA
Jambo lingine lililoibua mshangao ni kwa baadhi ya waalikwa kujiukuta wakisimama kutokana na kukosa viti kitendo ambacho kiliwaboa waalikwa.
Kilichoonekana, sababu ya wengi kukosa viti ni kutokana na upangaji na hawakuzingatia idadi ya wageni na watu kujikuta wakisimama mwanzo hadi mwisho wa sherehe, licha ya kuwa ukumbi ulirembwa vizuri na kuvutia.