Huyu ndiye mmiliki wa wimbo ‘Halal’

Muktasari:
- Wimbo huo sio mpya kwani umetoka miaka 12 nyuma, lakini umekuwa maarufu hivi karibuni na baadhi ya wasanii hapa nchini kama Hamisa Mobetto wamekuwa wakiutumia kwenye kipindi hiki cha Ramadhani.
HALAL ni kati ya nyimbo zinazofanya vizuri nchini hasa kwenye kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kutokana na kuwa katika mahadhi fulani ya Kiarabu.
Wimbo huo sio mpya kwani umetoka miaka 12 nyuma, lakini umekuwa maarufu hivi karibuni na baadhi ya wasanii hapa nchini kama Hamisa Mobetto wamekuwa wakiutumia kwenye kipindi hiki cha Ramadhani.
Biti za wimbo huo zinaendana na muziki wa asili ya Kiarabu, lakini hauna maana yoyote na Ramadhani kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakiutumia.
’Halal’ ni neno lenye asili ya Kiarabu likimaanisha kitu kinachoruhusiwa au kilicho sambamba na sheria, mfano chakula na matendo ya maisha.

“Mpenzi wangu, moyo wangu unakuhitaji/ Bado mimi ndiye ninayekuita, umeongeza mateso yangu kwa kutokuwepo kwako, Je, huu utengano utaisha?/” hayo ni baadhi ya maneno yanayopatikana kwenye wimbo huo.
Msanii Elissa, raia wa Lebanon ndiye aliyeimba wimbo huo ambao ulitolewa miaka 12 iliyopita.
ALIPOZALIWA
Jina lake kamili ni Elissar Zakaria Khoury maarufu Elissa. Alizaliwa Oktoba 27, 1972 Deir Al-Ahmar nchini Lebanon na amekuwa maarufu kwa kutunga na kuimba nyimbo za mapenzi zenye hisia.
Kazi yake ya muziki ilianza mwaka 1992 aliposhiriki kwenye shindano la vipaji la Kilebanoni Studio El Fan, alishinda medali ya fedha. Mwaka 1998, alitoa albamu yake ya kwanza ‘Baddy Doub’ kupitia EMI Music Arabia.
Elissa alipata mafanikio makubwa kupitia wimbo wake wa kwanza “Ayshalak” alioutoa mwaka 2002 kutoka kwenye albamu yake ya tatu yenye jina hilohilo ukipokewa vyema.

ELIMU
Elissa alihitimu shahada ya Sayansi na Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Lebanon aliyoitumia kuchanganya kwenye muziki wake.
Hakuishia kwenye kusomea Sheria bali ni mfuasi wa chama cha Lebanese Forces na kiongozi wake, Samir Geagea, na aliunga mkono juhudi za kuwania urais kwa kiongozi huyo.

SARATANI YA MATITI
Mwishoni mwaka 2018 mkali huyo alipata ugonjwa wa saratani ya matiti ingawa hakuweka wazi hadi alipopona na mwaka 2018 alitoa wimbo ‘Ila Kol Elli Bihebbouni’ ukiwa na maana ya ‘Kwa Wote Wanaonipenda’.
Ndani ya wimbo huo kuna maneno yanayosema “Nimepona, nimeushinda ugonjwa huu na nimeshinda, utambuzi wa mapema wa saratani ya matiti unaweza kuokoa maisha yako, usipuuzie likabili fanya hivyo si kwa ajili yako tu, bali pia kwa ajili ya wapendwa wako.”
Akimaanisha kwamba yuko sawa kiafya na kuwahamasisha wanawake kufuatilia kwa ukaribu afya zao, kampeni iliyoungwa mkono na wananchi wengi nchini humo na mwaka huo huo akachaguliwa kuwa balozi wa kampeni ya uhamasishaji wa saratani ya matiti.

ALBAMU TISA
Hadi sasa mwanadada huyo ana albamu tisa alizotoa tangu mwaka 2004 zilizouzwa zaidi Mashariki ya Kati ikikadiriwa zaidi ya nakala milioni 30.
Albamu ya kwanza, Baddy Doub (1998), W’akherta Maak (2000), Ayshalak (2002)Ahla Dounya (2004), Bastanak (2006), Ayami Bik (2007), Tesada’a Bemeen (2009), Asaad Wahda (2012), Halet Hob (2014), Saharna Ya Leil (2016), Ila Kol Elli Bihebbouni (2018), na Sahbit Raey (2020).

TUZO
Alichaguliwa kwenye tuzo mbalimbali za kimataifa ikiwamo MTV Europe Music Awards 2007 kwenye kipengele cha Best Arabian, World Music Awards akishinda tuzo nne kwenye kipengele Best Selling Middle Eastern Artist.
Mwaka huo pia alishinda tuzo za ‘Billboard Music Awards’ zinazotolewa nchini Marekani akishinda kwenye kipengele cha Lifetime Achievement Awards.
Hizo ni baadhi ya tuzo za kimataifa ambazo nyota huyo alifanikiwa kuchukua na kumpa umaarufu mkubwa akiwa miongoni mwa wasanii wakongwe nchini humo.
Tuzo hizo zilimpa kolabo na wasanii mbalimbali akifanya wimbo na Saad Lamjarred msanii kutoka Morocco ‘Min Awel Dekika’ uliotoka mwaka 2022 na piaia Muingereza Chris de Burgh wakitoa wimbo wa Lebanese Night uliotoka mwaka 2002.