Hussein Jumbe - Baada ya kuzomewa ageuka shujaa Sikinde

Thursday August 04 2022
jumbe pic

ILIPOISHIA

Mikasa bado ilikuwa ikimwandama Jumbe. Akiwa na Sikinde alisukiwa zengwe la kuzomewa jukwaani, mpango ulioandaliwa na baadhi ya wanamuziki.

ENDELEA...


ANASEMA baadhi ya wanamuziki waliamua kumtengenezea zengwe hilo ili asiajiriwe katika bendi hiyo. Anasema ilitokea chuki tu, hata hajui ilitokana na nini.

Mpango mzima ulisukwa ili Jumbe aimbe wimbo ambao haujui vizuri na mashabiki wa kumzomea walishaandaliwa. Ilikuwa ni Alhamisi katika Ukumbi wa Vijana, Kinondoni akiwa amejituliza kimya nyuma ya jukwaa, mwanamuziki mmoja wa bendi hiyo alimfuata na kumwambia akaimbe wimbo wa Zuwena.

Advertisement

Jumbe anasema jana yake alishamwambia mwanamuziki huyo wimbo huo alikuwa haujui vizuri. Lakini siku hiyo akamfuata tena na kumwambia akaimbe jukwaani.

“Nilimwambia wimbo huo siujui vizuri, akasisitiza lazima nikaimbe,” alisema Jumbe. Anasema alimwomba Mungu na akapanda jukwaani, akashika kipaza sauti na kuanza kuimba wimbo huo.

“Ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe na mashabiki wakajaa kunitunza pesa za kutosha na wengine wakanibeba juu juu. Nilikuwa kama naota, sikuamini kilichotokea, muziki ulizimwa, nilibaki natweta na machozi yakinichuruzika, acheni Mungu aitwe Mungu,” anakumbuka Jumbe

Gazeti moja lililokuwa likitoka mara mbili kwa wiki lilimpamba Jumbe kwa picha kubwa akiwa amebebwa jukwaani.

Kesho yake akiwa Mlalakuwa alifuatwa na kijana mmoja mwenye asili ya Kiarabu, Bakary Omary ambaye naye alikuwepo kati ya wale waliombeba pale Ukumbi wa Vijana.

“Yule kijana nilikuwa nimesoma naye Shule ya Sekondari ya Kinondoni Muslim na alikuwa rafiki yangu mkubwa sana, ndiye aliyekuja kunipa mkasa mzima ulivyokuwa.”

Jumbe anasema kijana yule alienda Ukumbi wa Vijana kumwona yeye baada ya kusikia yuko Sikinde, akiwa pale ndipo aliposikia mpango ulioandaliwa ili kumzomea. Baada ya kuusikia mpango ule rafiki yake akapindua meza na kuwafanya mashabiki wamshangilie na akamtajia wanamuziki waliopanga mpango mzima.


Shule ya Benovilla na King Enock

Mwanamuki huyo anasema baada ya kuona hali ile alimfuata Michael Enock ‘Teacher’ na kumwomba amwambie udhaifu wake.

“King Enock aliniambia, nilisikia wenzio wakisema wewe ni jeuri wa chinichini, ukikaa na wenzio huongei na unapenda kukaa peke yako,” Jumbe anayakumbuka maneno hayo.

“Palepale nikajua usia wa bibi yangu unanitesa, maana yeye ndiye aliyeniambia nikiwa mbele ya watu niwe nazungumza kidogo na kusikiliza sana.”

Jumbe anasema King Enock alimpa msaada mkubwa wa mazoezi na akawa anajifunza pia kwa mwanamuziki mwingine wa bendi hiyo, Benovilla Antony Magari.

“Pamoja na kupata kozi pale Bagamoyo, niliona kuna haja ya kujifunza zaidi, hivyo kila Jumamosi nilikuwa namfuata Beno Magomeni na kufanya naye mazoezi,” anasema na kuongeza kipaji chake kilipanda na uwezo uliongezeka hadi akapewa ajira ya kudumu DDC Mlimani Park.


Panga safari ya Nairobi

Mwaka 1990 Sikinde ilifanya ziara jijini Nairobi, Kenya kwa nia ya kwenda kufanya maonyesho na kurekodi nyimbo.

Katibu wa bendi enzi hizo, Herny Mkanyia alitoa taarifa kwa wanamuziki wote kuhusu safari hiyo ya wiki moja na itakuwa na wanamuziki 17.

Jumbe anasema katika majina hayo jina lake halikuwemo. Lakini yalipotajwa majina ya wanamuziki watakaobaki jina la Jumbe lilikuwa la kwanza.

“Wenzangu wengine waliobaki walionyesha chuki, miye wala sikujali na ndio kwanza nilinyoosha kidole na nilipopewa nafasi niliwaombea dua waliokuwa wanasafiri.”

Anasema safari ilikuwa Jumapili baada ya onyesho lao katika Ukumbi wa DDC Kariakioo na baada kumaliza kazi aliondoka lakini akiwa kituoni alimwona mwanamuziki wa Sikinde, Habib Abbas Mgalusi ‘Jeff’ akimfuata. “Jumbe, viongozi wanakuita umo kwenye safari. Nilishangaa nikamshuru Mungu.”

Mwaka 1990, Benovilla alihama Sikinde na kujiunga na OSS na baadaye, Vijana Jazz. Gurumo akarudi Sikinde. Hata hivyo Gurumo hakukaa sana aliondoka na Bitchuka wakajiunga na Msondo Ngoma. Uongozi wa Sikinde ukamrudisha Shaban Dede kundini.


Kifo cha Meneja Mwampulo

Jumbe anakumbuka Sikinde ilipata mwaliko wa kwenda kutumbuiza Ujerumani lakini ghafla kilitokea kifo cha Meneja wa bendi, Henzron Mwampulo na safari ikafa. Dede akachaguliwa kuwa kiongozi wa bendi.

Mwaka 1995, Jumbe aliandika barua ya kuomba likizo bila malipo kwa miezi mitatu ili aende Nairobi kwa ajili ya matibabu ya kutosikia vizuri. Akiwa Nairobi alifikia kwa rafiki yake, Mfanyabiashara Onyii Kadori ambaye awali yeye alimpokea rafiki yake huyo alipokuja Dar es Salaam.

Baada ya kukaa Nairobi kwa miezi mitatu na kumaliza tatizo lake, Jumbe alitaka kurudi Tanzania lakini Kadori akamzuia. Rafiki yake huyo alimpeleka Jumbe hadi mpakani Namanga na kugonga tena muhuri wa kuendelea kuishi Kenya kwa miezi mingine sita.

Kisha Kadori akataka Jumbe awe mfanyabiashara kwa kumfungulia duka kubwa jijini Nairobi lakini mwanamuziki huyo alikataa kwa kumwambia hakuwa na uzoefu na biashara.

“Ndipo Kadori ambaye dada yake ameolewa na raia wa Denmark aliponiambia nitafanya kazi niliyoizoea,” anasema Jumbe.

Kadori na dada yake wakatafuta hoteli na Jumbe akanunuliwa vyombo vya muziki, akapewa Bendi ya Five Matata kuingoza.

“Maisha ya Nairobi yalikuwa mazuri sana, mkurugenzi wetu Pamela Onyii na mume wake Mr. Hans walitujali sana. Wanamuziki tulipangiwa nyumba nzima eneo la Westland, yaani ushuwani kama Masaki vile kwa hapa Dar es Salaam,” anakumbuka Jumbe ambaye anasema alimchukua Abdallah Gama aliyekuwa Nairobi wakati huo kwa sababu watu wengi walikuwa wakiomba kupigiwa nyimbo za Sikinde.

Mbali na nyumba, lakini waliwekewa wafanyakazi wa usafi na upishi na walikuwa wanaishi maisha mazuri sana.


Safari ya Denmark

Jumbe anasema Kadori alizungumza na shemeji yake, Hans na mpango wa kuipeleka Denmark Bendi ya Five Matata. Tatizo wanamuziki walikuwa wakipenda sana pombe, hata Jumbe alipojaribu kuwakataza au kuwataka wapunguze ilishindikana.

“Wakati wa maandalizi ya kwenda Denmark tuliandaa onyesho ambalo tulikuwa tunachukuliwa na video ili itumwe kwa wenyeji wetu kabla hatujaenda, kilichotokea hakisimuliki,” anakumbuka Jumbe.

Anasema wanamuziki walikuwa wamelewa sana na ilifika hatua wengine walitaka taa za kwenye onyesho zizimwe.

Hatimaye wanamuziki walipigana jukwaani na bendi ikaishia hapo hapo.


Advertisement