Hussein Jumbe alala kwenye shamba la mihogo

ILIPOISHIA

Anasema kila alipokuwa akimuomba msamaha Mzee Mnenge ni kama alikuwa akimzidisha hasira kwani aliendelea kuzungumza kuhusu suala hilo la kukanyaga kiti chake kwa bahati mbaya wakati akijaribu kuvuka upande wa pili.

Kama haitoshi, hata walipomaliza kupiga na kuingia ndani ya gari ili warudishwe makwao, Mzee Mnenge aliendelea kusema kuhusu suala lile. Baadhi ya wanamuziki walimsihi Jumbe asimjibu.

Jumbe anasema gari lilipofika Ilala sokoni alishindwa kuvumilia akashuka ili kuepusha shari.

ENDELEA...


WAKATI ule Jumbe alikuwa akiishi Magomeni Mapipa na Mnenge alikuwa akiishi Magomeni Mwembe Chai na gari ilikuwa ikianza kuwarudisha wanamuziki wa Ilala na Keko na baadaye warudishwe wao.

“Ilishafika saa tisa za usiku, kipindi kile usafiri ulikuwa mgumu sana, nililazimika kulala pale sokoni Ilala na asubuhi ya kesho yake kutafuta usafiri wa kwenda nyumbani.”


Mwanamke ampa msala

Jumbe anadai, Jumapili iliyofuata bendi ilipiga katika Ukumbi wa Amana na wakati akiimba alitokea mwanamke mmoja ambaye yeye hakuwa akimfahamu. Yule mwanamke alipanda jukwaani na kumtunza wakati akiimba kipande cha Wimbo wa CCM kipande cha Hassan Rehani Bitchuka na kama haitoshi yule mwanamke akamsindikiza Jumbe na busu la shavuni ambalo hakuwa amejiandaa kulipokea.

“Kilikuwa kitendo cha ghafla mno. Nilishangaa sana lakini sikuweza kufanya jambo lolote,” anasema mwanamuziki huyo.

Siku ya Jumanne wakiwa kwenye Ukumbi wa Amana, wakifanya mazoezi na wenzake mara Jumbe aliitwa chemba na Mzee Mnenge.

Alipoenda akakabidhwa barua ya kuachishwa kazi bila ya kujua au kuambiwa kosa lake. Baadaye ilifahamika yule msichana aliyemtunza na kumpiga busu ndiye aliyemponza kwani alikuwa ameongeza chumvi kwenye kidonda.


Atua Urafiki Jazz

Jumbe anasema uzuri wa maisha ya zamani kulikuwa hakuna mitandao ya kijamii. Lakini kama ingekuwepo taarifa za yeye kufukuzwa kazi Msondo Ngoma zingesambaa.

Anasema siku moja alienda Jumba la Maendeleo la Urafiki, pale Bendi ya Urafiki Jazz ilipokuwa ikitumbuiza na akakutana na wanamuziki ambao alikuwa nao Tabora Jazz.

“Wale wanamuziki wakanitaka nijiunge na bendi yao, lakini walifahamu nilikuwa Msondo, ila hawakuwa na taarifa za kutimuliwa kwangu. Niliwaambia kama maslahi yatakuwa mazuri nitaacha Msondo na kujiunga na bendi yao. Nikakubaliwa na utaratibu ulikuwa kama ule wa Msondo nilifanyiwa usaili.”

Anakumbuka alifanyiwa usaili mbele ya Wanamuziki Gidion Banda na Juma Mrisho Ngulimba wa Ngulimba na baadaye kujadiliwa na wanamuziki wengine hivyo nikatolewa nje.

“Wakati najiandaa kutoka nje, baadhi ya wanamuziki wakahoji tunamjadili nini? Kauli hiyo iliungwa mkono na kiongozi wa bendi Juma Mrisho, nikapewa fomu ya kujiunga na bendi.”

Wakati mwanamuziki huyo anajiunga na Urafiki alikuta wanajiandaa kwenda RTD kurekodi. Hapo hapo Jumbe akaibuka na nyimbo tatu, Elimu Makazini, Ndugu zangu wamenitenga na Asha wa Chande.

“Baada ya miezi mitatu nikapewa uongozi, nikawa katibu wa bendi na mshahara ukaongezeka. Kitu cha ajabu chuki nazo zikaongezeka.”



Ishu ya shamba la mihogo

Akiwa katika ajira yake mpya na Urafiki Jazz, Bendi ya DDC Mlimani Park ilikimbiwa na wanamuziki takribani saba. Hii ilikuwa ni awamu ya pili kwa wanamuziki wa bendi hiyo kukimbilia Ochestra Safari Sound (OSS- Ndekule) baada ile ya mwaka 1985.

Wanamuziki waliondoka Sikinde ni Cosmas Chidumule, Maxmillian Bushoke na Fresh Jumbe Mkuu. Wengine ni Said Chipembele, Ally Jamwaka, Shaban Lendi na Huruka Uvuruge.

Ndipo mwanamuki aliyerudi Sikinde kutoka Ndekule, Bitchuka alipofika katika Jumba la Maendeleo la Urafiki na kumuulizia Jumbe.

“Alikuwa hanijui, isipokuwa alikuwa amesikia nyimbo zangu za Tabora Jazz na Urafiki Jazz. Wiki moja baadaye nikaenda Sikinde kwa ajili ya kujaribiwa, nikapewa nafasi ya kuchagua wimbo mmoja wa Sikinde, nikaimba Christina Bundala,” anasema Jumbe ambaye alipewa wiki moja kupewa majibu yake.

Akiwa amekubaliwa kujiunga na Sikinde mwaka 1987, Jumbe aliamua kuaga katika bendi yake ya Urafiki ambako alikuwa mwimbaji, mpiga drums, mtunzi na katibu mipango wa bendi.

Siku hiyo Urafiki ilikuwa ikipiga nje ya Jiji la Dar es Salaam maeneo ya Chanika, akaamua kumwambia mwimbaji mwenzake hilo litakuwa dansi lake la mwisho kwani ameitwa kujiunga na Sikinde. Jumbe alimtaka mwimbaji huyo awape taarifa ya kuwaaga wanamuziki wengine.

“Hilo lilikuwa kosa la kwanza, baada ya salamu zangu kufika mmoja wao akasema tuone kama leo atapanda basi la bendi, sijui atarudi vipi mjini,” anakumbuka.

Anasema mwanzo alidhani ni utani lakini alipochunguza akagundua wamedhamiria kweli. Walipomaliza kupiga muziki, akaenda kwa kiongozi mwingine wa bendi ili amweleze kinachoendelea na kutaka kujua kosa lake.

“Lilikuwa kosa la pili, kwani kiongozi yule alinikosakosa ngumi, nikajua wamedhamiria, nikatoka mbio kukimbia nisipopajua na giza lilishatanda,” Jumbe anasema

Anasema ulikuwa ni usiku mnene wanamuziki wote wakaungana kumfukuza ili wampige lakini bahati nzuri kwake hakufika mbali sana na kujiingiza kwenye shamba la mihogo na kujificha.

“Walipita bila ya kuniona, nililazimika kulala kwenye shamba lile la mihogo hadi asubuhi. Chanika ya kipindi kile siyo kama ya sasa zamani usafiri ulikuwa shida sana,” anasema. Jumbe anafafanua kiongozi aliyemkosa ngumi katika Bendi ya Urafiki Jazz mpaka leo hii yupo. Na yeye amehamia Sikinde (jina tunalo).

Oktoba 10, 1987, basi la DDC Mlimani Park lilisimama katika maghorofa ya Urafiki Bloki G na kubeba vyombo vya Jumbe na kumhamishia Mwenge, Mlalakuwa. Jumbe anasema alijiunga bendi hiyo pamoja na mwanamuziki mwingine, Mohammed Mwinyikondo aliyekuwa ametokea Dar International na aliambiwa angekuwa ndani ya majaribio ya wiki moja ila mwenzake aliajiriwa kabisa. Jumbe alipiga moyo konde na kujiongeza katika kufanya kazi kwa bidii. Mlalakuwa alikuwa akiishi na wanamuziki wengine kina Michael Enock ‘King’, Michael Bilali, Abdallah Gama, Mwinyikondo na Abdallah Dogodogo.


Zengwe la kuzomewa

Mikasa bado ilikuwa ikiendelea kumwandama Jumbe. Akiwa na Sikinde alisukiwa zengwe la kuzomewa jukwaani, mpango ulioandaliwa na baadhi ya wanamuziki. Anasema baadhi yao waliamua kutengenezea zengwe hilo ili asiajiriwe katika bendi hiyo.

Nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kesho katika gazeti hili.