Hussein Jumbe, visa mikasa yamwandama miaka 42

Tuesday August 02 2022
jumbe pic
By Mohammed Kuyunga

MMOJA kati ya wanamuziki wenye sauti nzuri katika muziki wa dansi hapa nchini ni Hussein Suleimani Jumbe. Ukipenda mwite Mzee wa Dodo au jina analolitumia sasa la Mtumishi.

Mwanamuziki huyu mwenye tunzi za kusikitisha kama sio kulalamika, hupenda sana kutunga nyimbo zinazotokana na matukio ya kweli. Jumbe ambaye anatesa jukwaani kwa takribani miaka 42 sasa amefanya mahojiano na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi aliyokutana nayo katika maisha yake ya muziki kwa ujumla.

Baada ya kumaliza elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko jijini Dar es Salaam, Jumbe alijiunga na Sekondari ya Kinondoni Muslim, baba yake alimtafutia kazi katika Kiwanda cha NCG cha kuzalisha vifaa vya plastiki ambayo aliifanya huku akiwa na mipango yake ya kushiriki kwenye muziki.


Safari Trippers Yamkosha

Wakati baba yake mzazi akitaka Jumbe asome Qur’an, akili ya Jumbe ilishaingia kwenye muziki tangu alipokuwa akisoma shule ya Msingi.

Advertisement

Siku za wikiendi alikuwa akienda katika muziki na bendi aliyokuwa akihudhuria ni Safari Trippers iliyokuwa ikipiga kwenye Ukumbi wa Princes, Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

“Ilifika hatua wanamuziki wote wa bendi hiyo walikuwa wakinifahamu. Nilikuwa nafika mapema nanunua soda yangu, raha yangu ilikuwa ni kuwaona wanamuziki wa bendi hiyo walipokuwa wakiingia ukumbini,” anasema Jumbe.


Aenda kusomea muziki

Mishahara ya miezi mitatu ilimtosha kuacha kazi aliyotafutiwa na baba yake Mzee Suleimani Jumbe, kipato hicho kilimfanya kwenda kusomea muziki katika Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo.

“Niliacha kazi na kwenda kusomea muziki. Baba alikasirika sana, tangu utotoni alinitaka nisomee dini. Nikitoka shule alitaka nienda madrasa. Muda huo ndio ulikuwa wa kwenda kufanya mazoezi ya muziki na wakati mwingine nikiutumia kucheza mpira.

“Dada yangu Mwanakombo ndiye aliyekuwa akinitetea na kunipangia ratiba ya kwenda madrasa na kufanya mazoezi ya muziki,” anasema.

Jumbe anasema kazi ilikuwa ngumu sana na ilikuwa ikimnyima ratiba zake za kufanya mazoezi ya muziki na hata kucheza soka vitu ambavyo alikuwa akivipenda sana.

“Kazi zikiwa nyingi nilikuwa naunganishwa kwenye shifti ya saa nne usiku hadi asubuhi. Kwenye mazoezi ya muziki nilikuwa naenda kwa nadra sana. Baada ya miezi mitatu nikaacha kazi.”

Baada ya kuacha kazi, Jumbe anasema alikiona cha moto kwani baba yake alimpiga marufuku kula nyumbani na alizichukua nguo zote alizomnunulia na kwenda kuzigawa kwa ndugu yake mwingine.

“Maisha yalikuwa magumu sana. Nilianza kufunga kandambili kwa waya na kuweka viraka kwenye nguo, ndipo nilipoamua kutoroka.”


Atorokea Tabora

Mwaka 1983, baada ya kupata mafunzo ya awali ya muziki, Jumbe alitoroka na kwenda mkoani Tabora kujiunga na bendi ya Tabora Jazz. Aliingia mkoani humo Desemba 28.

“Nilipofika Tabora moja kwa moja nilienda nyumbani kwa mmiliki wa bendi Mzee Mlekwa. Nilijitambulisha kuwa ni mwanamuziki, nilipokewa vizuri na kupewa chakula na sehemu ya kulala na kesho yake nikaanza kufanya shughuli za muziki,” anasema.


Kalenga amtoa kwenye drums

Alipofika Tabora Jazz, Jumbe alikuwa akishiriki muziki kama mpiga drums lakini kiongozi wa bendi hiyo, Shem Kalenga akamtoa kwenye chombo hicho.

Ilikuwa ni Desemba 23, 1984 Tabora Jazz ilikuwa safarini kwenda Mpanda, Sumbawanga kutumbuiza kwa ajili ya Sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya.

Wakiwa ndani ya treni saa saba usiku wanamuziki na abiria wengine wakiwa wameshapiga usingizi, Jumbe alikuwa akiimba wimbo wa Safari Trippers wa Matilda hasa vipande vilivyoimbwa na mwamuziki nguli, Marijani Rajabu.

Kumbe Kalenga hakuwa amelala, alimsikia Jumbe akiimba. Waliporudi Tabora, kiongozi huyo akamwambia kuanzia wakati huo atakuwa mwimbaji na sio mpiga drums tena.

“Nilimwambia mbona miye sio mwimbaji, akaniambia nilikusikia ukiimba wakati tulipokuwa safarini,” anasema Jumbe ambaye tangu siku hiyo akaanza kuimba na kupiga drums mara moja moja. Shem Kalenga alimkabidhi nyimbo sita azifanyie mazoezi ya kuziimba kwa kuwa ilikuwa imebaki wiki moja kwenda kurekodi Redio Tanzania (RTD).

“Kipindi kile RTD walikuwa na kipindi cha Misakato kwa ajili ya kuzitambulisha nyimbo mpya, wakati nyimbo zetu zilipokuwa zikipigwa, dada yangu Mwanakombo ndiye aliyesikia na kumwambia mama na watu wengine.” Jumbe anakumbuka wakati Tabora Jazz ilipofika RTD kurekodi.

“Huzuni iliyokuwa imetanda kwa ajili yangu ikapotea. Nyumba ikalipuka kwa furaha wakajua miye ni mzima,” anasema.

Jumbe anaongeza baada ya kufanikiwa kurekodi alienda nyumbani kwao na kumaliza tofauti zake na wazazi wake ambao nao walifurahi kumuona akiwa mzima wa afya njema. Akiwa Tabora Jazz, Jumbe alishiriki kurekodi nyimba nane. Kati ya hizo sita aliimba na mbili akapiga drums.


Maisha yasonga mbele

Februari 5, 1985 mwanamuziki huyo aliihama Tabora Jazz na kujiunga na Bendi ya Mara Jazz iliyokuwa na masikani yake mjini Musoma Mjini.

Jumbe anasema wakati wakiwa Dar es Salaam na Bendi ya Tabora Jazz walifanya onyesho kwenye Ukumbi wa DDC Keko pamoja na Mlimani Park ‘Sikinde’, alituzwa pesa sana.

“Nikiwa nimekaa pembeni nikiwaangalia Sikinde, alikuja bwana mmoja na kunitaka tuonane kesho yake Manyai Guest House, maeneo ya Karikoo.

“Kumbe yule alikuwa ni mmiliki wa Mara Jazz. Basi kesho yake tukazungumza na akaniachia pesa za kutosha. Niliporudi Tabora nikaunganisha hadi Mwanza na baadaye Musoma.”


Lifti ya ndege hadi Dar

Akafika mkoani Mara na kujiunga na Mara Jazz. Baada ya kukaa kwa muda bendi hiyo ilienda katika ziara katika miji ya Mugumu, Serengeti na katika Kambi ya Jeshi ya Fety Ikoma na jina la Jumbe likipewa kipaumbele kwenye matangazo, kumbe baba yake alikuwa ameshafariki dunia jijini Dar es Salaam.

“Mkuu wa Kambi ya Fety Ikoma alipotaka tuongeze shoo nyingine mbili, ndipo mmiliki wa bendi, Bwana Msomi alipomwambia alikuwa ametumiwa teregramu ya kufariki kwa baba yangu mzazi ila sikuwa nimeambiwa.

“Mkuu wa kambi akamwambia bosi wangu aniambie nijiandae na nikapewa lifti ya ndege hadi Dar.”


Atua Msondo Ngoma

Jumbe anasema alipofika Dar es Salaam alikuta baba yake mzazi ameshazikwa siku moja nyuma. Katika matembezi yake katika Jiji la Dar es Salaa, Jumbe alijikuta ametokea Keko Mwanga katika Ukumbi wa Jitulize Bar, ambako Bendi ya Juwata Jazz ilipokuwa ikitumbuiza.

“Nilimkuta Said Mabera (kiongozi wa bendi ambaye sasa ni marehemu) nje ya ukumbi akivuta sigara. Nikamsalimia na kumwambia miye ni mwanamuziki na kumwonyesha kitambulisho changu.

“Mabera alinishika mkono hadi mlangoni na kuwambia nikija kuingia wasinizuie,” anasema.

Muziki ulipoisha Jumbe alimfuata Mabera na kumshukuru kisha akamuomba ratiba ya bendi na kujua wanapofanya mazoezi na utaratibu wa kujiunga na bendi.

“Jumanne moja nikaenda Klabu ya Sigara, Ilala Shariff Shamba walipokuwa wakifanya mazoezi. Nilipeleka barua ya kuomba kujiunga, nikafanyiwa usaili nikaambiwa nitoke nje ili wanamuziki wanijadili.”

Miaka ya nyuma Msondo ilikuwa ikifanya mazoezi Klabu ya Sigara iliyopo Shariff Shamba kabla ya kuhamia kwenye Ukumbi wa Amana.

Baada ya dakika 10, Jumbe aliitwa ndani na kuambiwa amekubaliwa kujiunga na bendi. Ila alitakiwa kuongeza juhudi na kuondoa hofu huku akisubiri ajira yake.

Kesho yake viongozi kutoka ofisini Juwata walifika na kumwona na kumkubali kutokana na uwezo wake.

Jumbe anakumbuka wakati akijiunga na Juwata Jazz aliwakuta waimbaji kina Suleiman Mbwembwe, Tx Moshi William, Hamis Kitambi, Theofil Mvambe na Tino Masinge.

Kwenye magitaa walikuwapo kina Mabera, Abdul Ridhiwani Pangamawe, Hagai Kauzeni, Mustafa Pishuu ‘Baba Isaya’, Bakari Semhando ‘Difsa’, Haji Seseme na Kassim Mponda ‘De la Chance’.

“Nilianza mazoezi na kushiriki katika wimbo wa Asha Mwanaseif utunzi wa Tx Moshi. Kile kipande alichorekodi Nico Zengekala nilikuwa nakiimba miye ndiye niliyekichomekea, Nico alivaa viatu vyangu,” anasema Jumbe.

Kipande hicho kinaimbwa hivi: ‘Natubu mbele yako hasa kwa hao Malaika unisamehe duniani hata mbinguni’.


Kiti chamuondoa Msondo Ngoma

Jumbe anasema bahati haikuwa upande wake hakuweza kupata ajira wala kurekodi na Juwata Jazz. Ilikuwaje?

Anasema siku hiyo walikuwa wakitumbuiza katika Ukumbi wa DDC Kariakoo. Yeye alikuwa akiimba wimbo mmoja wa zamani wa mwimbaji Shabani Dede uitwao ‘Christopher’, wakati anashuka jukwaani hakupita kwenye ngazi, bali alipita njia ya mkato kwa kushukia pembeni.

Lakini wakati akishukia upande huo alikanyaga kiti cha mwanamuziki mkongwe wa bendi hiyo, Ramadhani Mnenge (sasa ni marehemu) katika kutafuta balansi ya kushuka.

“Mzee aliniita, nilipogundua kosa langu nilimuomba msamaha lakini hakunielewa. Nikakifuta kile kiti kwa mikono yangu, bado hakunielewa. Nikatoa kitambaa changu na kukifuta, bado hakunielewa. Nikaenda kumletea kiti kingine bado mzee hakunielewa,” anakumbuka Jumbe.

Anasema kila alipokuwa akimuomba msamaha Mzee Mnenge ni kama alikuwa akimzidisha hasira kwani aliendelea kuzungumza kuhusu suala hilo.

Kama haitoshi, hata walipomaliza kupiga na kuingia ndani ya gari ili warudishwe makwao, Mzee Mnenge aliendelea kusema kuhusu suala lile. Baadhi ya wanamuziki walimsihi Jumbe asimjibu.

Jumbe anasema gari lilipofika Ilala sokoni alishindwa kuvumilia akashuka ili kuepusha shari.

Advertisement