Hussein Jumbe 9 - Amtoa machozi TX Moshi, mazoezi yavunjika

ILIPOISHIA

JANA katika mfululizo wa makala haya ya mahojiano maalumu na gwiji wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe, tuliona namna alivyopelekwa kwa sangoma na swahiba wake, Meddy Mpakanjia na kutolewa mbegu za papai mguuni.

Pia, tuliona alivyoletewa dili la kwenda TOT Plus na kupondwa, kabla ya TX Moshi William kumchomoa na kumpa dili la Msondo Ngoma ambapo hata hivyo lilimtumbukia nyongo. Kivipi? Tiririka naye...!


DILI LA MSONDO NGOMA

Akiwa TOT Plus, Jumbe alikuwa akiendelea kuwasiliana na mwanamuziki Benovilla wa Sikinde na mkataba wake wa miaka miwili wa TOT Plus ulikuwa ukifikia ukingoni.

Mkataba huo ulipoisha, Sikinde ilikuwa imesafiri kwenda Mtwara, huku nyuma DDC ilikuwa imeleta meneja mpya, Mhando Muya ambaye alilipitia faili na Jumbe na kuona ni mwanamuziki mkubwa anayefaa kurudi katika bendi yao.

“Nilishanza mazoezi na Benovilla, lakini Muya alikuwa akinisifia tu kwa kazi nilizowahi kuzifanya Sikinde hadi kufikia kuwa mfanyakazi bora, hakutoa pesa, basi nikaamua kukaa zangu nyumbani mara mkataba wangu na TOT ulipoisha,” anasema.

Jumbe anaongeza akiwa nyumbani siku moja alifuatwa na aliyekuwa Meneja wa Serengeti Breweries, Kagusa na kumtaka kesho yake afike ofisini kwake kwa mazungumzo zaidi.

“Nilipoenda kumuona Kagusa, nikakutana na viongozi wa Msondo Ngoma kina Said Mabera (marehemu) na Said Kibiriti mazungumzo yakafanyika na nikamkumbusha Mabera kilichotokea mwaka 1986, akaniambia nimesoma dini na kunitaka nisamehe yaliyopita, anasema Jumbe.

Jumbe anasema kesho yake alienda kwenye Ukumbi wa Klabu ya Amana na kukutana na maseneta wa Msondo chini ya Masoud Limira na kukubaliana kusaini dili la miaka miwili.

Hata hivyo, inadaiwa Jumbe kujiunga kwake na Msondo kulitokana na shinikizo la TX Moshi ambaye alitishia hata kujiweka pembeni iwapo baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo wangeendelea kumkatalia kwa sababu za kudaiwa ni mkorofi.

Katika mazungumzo haya, Jumbe alikiri hilo na kudai hata TX Moshi alipata tabu sana kukubaliwa na baadhi ya wanamuziki wa Juwata Jazz wakati akijiunga na bendi hiyo mwaka 1982.


AMLIZA MOSHI MAZOEZINI

Ilikuwa ni katika mazoezi ya Bendi ya Msondo Ngoma, achana na suala la kumliza tu mwimbaji huyo, bali mazoezi yalivunjika hapohapo huku TX Moshi na wanamuziki wengine wakiangua vilio kutokana na hisia za Jumbe.

Ilikuwa ni wakati wa mazoezi ya Wimbo wa Ajali uliotungwa na TX Moshi, awali Jumbe aliachwa pembeni wakati wimbo huo ukifanyiwa mazoezi. Mwanamuziki mmoja alimtaka asogee jirani ya wenzake.

“Nilipofika pale niliwasikiliza kisha nikaingiza hisia zangu. Niliingiza kipande hiki ...Ndio maana nilipopatwa na maradhi miyeee nililialia ooooh. Ndio maana nilipopatwa na ajali nilijua familia yangu itaadhirika iyooleleee.”

Jumbe anasema alipoingiza kipande hicho kila mtu alilia, TX Moshi alilia na kufanya mazoezi kuvunjika hapohapo hadi kesho yake huku wanamuziki wengine wakimwambia Jumbe asikisahau kipande hicho.

Mwanamuziki huyo alifafanua kipande hicho kilikuwa kinagusa sehemu mbili, kwanza ni maradhi yake hadi akatunga Wimbo wa Nachechemea na pili ni ajali aliyoipata TX Moshi.

Katika albamu ya Ajali, Jumbe alitunga nyimbo mbili, Tranfer na Ndugu zangu Wamenitenga.


ARUDI SIKINDE NA KUULA

Jumbe anatumia fursa hii kukanusha madai yaliyozagaa kwamba hakumuaga TX Moshi wakati alipotoka Msondo kurudi Sikinde.

Pia, anakanusha mwimbaji huyo kugeuka ukutani alipoenda kumwangalia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa lengo la kukataa kuzungumza naye.

“Sio kweli, kwanza nilimuaga. Nilipoenda Muhimbili sikuwa peke yangu. Nilikuwa na Hemba (Abdallah) na Sauda Mwilima wa Star TV na majina yetu yalipelekwa ndani kisha tukaruhusiwa, ndani tulimkuta Hassan Moshi,” anasema.

Mwanamuziki huyo anasema alirudi Sikinde kwa msaada wa mwanamuziki Ally Yahya na Sikinde Family, ambao walimpa pesa alizotaka na kwa upande wa DDC aliwapa sharti mkataba wake uanze mwaka 2006.

Mwaka 2007, Sikinde ilifanya uchaguzi na baadhi ya wanamuziki wakapendekeza jina lake akawa meneja wa bendi baada ya kumshinda Dede.

Kabla ya kushinda uchaguzi, Jumbe alitoa ahadi za kufanya uzinduzi wa albamu ya Full Squad iliyokuwa imerekodiwa siku nyingi, kurudisha uhusiano na Sikinde Family, kuipeleka bendi mikoani na Ulaya.


AKOSA MSAADA

Mwanamuziki huyo anasema akiwa kiongozi wa bendi alijikuta akipitia wakati mgumu baada ya Shirika la DDC kushindwa kumpa kiasi cha Shilingi laki 9 kwa ajili ya bendi kurekodi nyimbo zake katika Studio za Sound Crafter.

Meneja Muya alimwambia shirika halikuwa na pesa na wahasibu wakamwambia cheki yake imefeli.

Akiwa anatafakari hilo, Jumbe alijikuta akifutiwa posho zake kama meneja wa bendi alitakiwa kulipiwa chakula, kinywaji na vocha.

Hata hivyo, Jumbe alizungumza na Enrico Figueiro wa studio ya Sound Crafter na kufanikiwa kurekodi albumu yao na kupatiwa kiasi cha pesa kwa ajili ya posho ya wanamuziki.

Wakiwa studio, mwanamuziki Hassan Kunyata na Dede walikuwa wakihangaika kubadilisha maneno ya wimbo wa ‘Kiranga cha Kujitakia’ utunzi wa Kunyata ambao ulikuwa ukimnanga Jumbe alipohamia TOT.

“Niliwafuata na kuwataka waimbe kama walivyokuwa wakiimba na nikawaambia na miye nitashiriki kuitikia wimbo huo, Dede alikataa,”ù Jumbe anakumbuka.

Katika hali ya kushangaza, mwanamuziki huyo alianza kufanya maandalizi ya uzinduzi wa Albamu ya Full Squad huku akijua shirika lishamwambia halikua na pesa.

Alimwambia katibu wake Hemba awaambie wanamuziki wa bendi hiyo waende kupimwa suti na achukue namba zao za viatu kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi wa albamu.

Pia, Jumbe alichukua namba za viatu vya Meneja Muya na Afisa Utumishi wa kipindi hicho, Shaban Mafumbi.

Jumbe alimfuata fundi wa suti na kumwambia aachane na mambo ya advance na kumwahidi kumlipa pesa yake yote.

Wakati Jumbe akifanya mambo yote hayo, katibu wake, Hemba alikuwa akishangaa pesa ilikuwa nyingi sana ingepatikana wapi?

Pia, wanakamati wote wa bendi walikaa pembeni na kuangalia nini kitatokea. Hawakushirikiana kabisa na Jumbe pamoja na katibu wake.

“Nilienda kwa katibu muktasi wa DDC, nikamuomba barua yenye muhuri wa ofisi, akanipatia na kuandika barua ya udhamini kwenda Tanzania Bweries,” anasema Jumbe.

Jumbe anasema alipata udhamini na kupewa cheki ambayo aliipeleka ofisini na kufanikiwa kulipa suti za wanamuziki na viatu. Pia, mwanamuziki huyo anasema pesa hizo zilisaidia kuwalipa wanamuziki madai yao na vilevile walilipa studio.

Katika uzinduzi huo, Sikinde ilisindikizwa na TOT Bendi na Twanga Chopolopolo, ulifana na kufanikisha ahadi yake ya kwanza aliyoahidi wakati akichaguliwa kuwa meneja wa bendi.

Mwanamuziki huyo anasema uzoefu huo aliupata katika Bendi ya Msondo Ngoma kutokana na ukaribu wake na meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti.


Nini kiliendelea? Usikose kufuatilia mikasa ya mwanamuziki huyu kesho.