Hussein Jumbe (8) - Mpakanjia ampeleka kwa Sangoma

ILIPOISHIA

KATIKA mfululizo wa makala haya ya mahojiano maalumu na gwiji wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe, tuliona namna alivyopewa kesi ya ugonjwa wa ukimwi, kisha kuzushiwa kifo kilichosababisha hadi mwenyewe kuhisi huenda amekufa kweli.

Leo tunaendelea naye akieleza matukio aliyokumbana nao, ikiwamo rafiki na mfadhili wake mkubwa enzi hizo, Meddy Mpakanjia alipoamua kubeba mzigo wa kumsaidia kwa kumpeleka kwa sangoma.. Ebu endelea naye...!


MEDDY AMPElEKA KWA MGANGA

Jumbe anasema swahiba wake Mpakanjia aliamua kumchukua na kumpeleka kwa mganga wa tiba za asili, Duga Maforoni mpakani mwa Tanga, Tanzania na Mombasa, Kenya.

“Tulipofika kwa mtaalamu tulipokewa vizuri. Tuliulizwa kama tuliwahi kwenda hospitalini, tukamjibu tulishaenda. Yule mganga akasema hajajaliwa kutibu mgonjwa wa Ukimwi wala Kifua Kikuu,” anakumbuka.

Mganga yule mwanamke alimgeukia Mpakanjia na kumwambia kama mgonjwa anaumwa kati ya magonjwa hayo hana dawa ya kumtibu.

Jumbe anasema Mpakanjia alimjibu mganga yule sikuwa na magonjwa yale. Yule mganga aliinama kwa sekunde kadhaa kisha akawaomba radhi sababu muda wa swala ya Magharibi ulikuwa umefika. Akaingia sehemu maalumu kwa ajili ya kufanya ibada.

“Baada ya kumaliza ibada, alituomba tumpatie vyeti ajiridhishe lakini hatukuwa navyo, tulikuwa tumeviacha Dar es Salaam,” anasema.

Yule mganga alitoa mtu wake mmoja na kuwataka wafuatane naye hadi hospitalini kwenda kuchukua vipimo upya ili kujiridhisha kama kweli mgonjwa hana kati ya maradhi hayo aliyoyataja.

“Hospitali nilipimwa tena Ukimwi, TB, minyoo, wingi wa damu na Malaria. Majibu yalikuwa mazuri tukarudi kwa mganga na akakubali kunitibia,” anasema.


MBEGU ZA PAPAI MGUUNI

Mganga aliomba baadhi ya vifaa vinunuliwe ili kuweza kuanza kazi ya kumtibia Jumbe. Vifaa vilivyohitajika ni wembe mpya, stiki sita, dawa ya maji na bandeji.

“Nilichanjwa chini ya mguu, kwenye kifundo upande wa kulia wa mguu wangu. Zile stiki zikawa zinaingizwa ndani ya sehemu nilizochanjwa na wembe, kwa mshangao zikawa zinatoka na mbegu za papai. Maumivu ya zoezi hili yalikuwa makali sana na damu nyingi ilitoka,” anasema Jumbe na kudai baada ya dakika tatu akawa hasikii tena maumivu yoyote.

Mganga alimuomba mgonjwa aendelee kubaki pale kwa ajili ya uangalizi na katika chakula alikuwa akiwekewa mboga aina ya matembele na matunda ya zambarau ili kurudisha damu iliyopotea.

“Ijumaa ilipofika, yule mganga alitutaka tukatoe sadaka msikitini hayo ndiyo yalikuwa malipo yake. Nikiwa nimejipumzisha upenuni mwa nyumba, Meddy akiwa amekaa kwenye stuli, niliinuka na kumshika mabega na kuanza kuchechemea, Alhamisi iliyofuata tukaruhusiwa kuondoka,” anakumbuka.


KISA CHA WIMBO NACHECHEMEA

Marafiki wa Meddy Mpakanjia wanamjua vizuri jamaa alikuwa ni mtumiaji mzuri wa sigara aina ya Embassy na alikuwa akinunua pakti zima.

Jumbe anasema wakiwa wamefika Segera kwa ajili ya kurudi Dar es Salaam, Meddy alikuwa amemaliza kuvuta sigara na alikuwa akitaka kulitupa pakti la sigara, akamzuia kufanya hivyo.

Akiwa amejilaza siti ya nyuma ya gari, aliliomba pakti hilo na kulitoa jalibox (ganda la ndani la pakti la sigara) kwa ajili ya kuandikia, aliiona peni kwenye shati la Meddy pia akamuomba.

Jumbe akaanza kuandika mashairi ya Wimbo wa Nachechemea.

“Niliyaandika na kuyahakiki mara mbili tatu kisha nikaridhika na kujilaza kwenye siti ya nyuma,” anakumbuka Jumbe ambaye alidai alishtuka gari ikiwa imeshafika Ubungo.

Jumbe alitaka apelekwe nyumbani moja kwa moja lakini Meddy akamkumbusha sharti walilopewa na mganga. Waliambiwa kabla ya kufika nyumbani ni lazima wafike kazini kwake kwanza.

“Kwani huwezi kusimama kwa dakika 20? Meddy aliniuliza nikamjibu naweza ila nimekonda sana,” anasema Jumbe na kuongeza swahiba wake huyo alimwambia kwani nani asiyejua kama anaumwa.

“Hatimaye, Meddy aliniambia kwa ukali kidogo nikitaka nitaenda, na nisipotaka nitaenda,” Jumbe anasema.

Sikinde ilikuwa inapiga Buguruni katika Ukumbi wa Y2K, Jumbe aliingia ukumbini hapo na kuimba nyimbo mbili kama ushauri wa swahiba wake.

Anasema alipoingia na kuanza kuimba mmoja wa waimbaji wa bendi hiyo aliondoka jukwaani na kwenda kupanda daladala na kutimkia zake nyumbani.

Jumbe alipona na kurudi kazini na utunzi wake wa kwanza ukawa huo Nachechemea. Ndani ya wimbo huo, Jumbe anawataja watu ambao walimsaidia kwa njia moja ama nyingine.

Wanaotajwa ndani ya wimbo huo ni Mpakanjia, Mama Malifedha (alikuwa meneja wa DDC), Christina Sina, hawa ni watu wawil waliokuwa wadau wa Sikinde. Christina ni mtu mwingine na Sina sasa ni mke wa mwimbaji wa bendi hiyo, Abdallah Hemba na Mama Ima ni mke wake Jumbe.


DILI LA TOT PLUS

Jumbe anasema baada ya Nachechemea kukamata akaamua kutunga wimbo mwingine wa Nani Kaiona Kesho kwa ajili ya kuwakumbusha watu umuhimu wa kuwajali wenzetu pindi wanapopata matatizo kama ya kuumwa.

Kabla hajaurekodi wimbo huo na bendi yake ya Sikinde, alifuatwa na Bendi ya TOT Plus ili akajiunge nayo. Anasema Septemba 2001 alipokea ugeni mzito nyumbani kwake, wakiwa ni Mkurugenzi wa TOT, Kapteni John Komba (sasa ni marehemu), Gasper Tumaini (ndiye Mkurugenzi wa TOT sasa), TX Moshi William (marehemu) na mwenyeji Mpakanjia.

Komba alimwambia Jumbe walikuwa wamemfuata kwa ajili ya kujiunga na Bendi ya TOT Plus na hapo walikuwa na mkataba ambao walimpa kwa ajili ya kuusoma na kama atakubaliana nao basi ausaini na kujiunga na bendi hiyo.

“Komba alisema, awali wao walimfuata TX Moshi lakini mwimbaji huyo alinipendekeza jina langu ili wote tujiunge na TOT,” anasema Jumbe.

Mwanamuziki huyu anasema alipewa mkataba wake ambao ulikuwa na ofa tamu kwelikweli, kiwanja maeneo ya Mbezi, matofali 900, pikipiki na Sh 3 milioni taslimu na kuambiwa kama atakuwa tayari kesho aende kutambulishwa.

Jumbe anasema aliomba dakika tano za kuzungumza na mkewe wake, Mama Ima na kukubaliana baadhi ya mambo kwa sababu mshahara wa TOT Plus ulikuwa mkubwa zaidi ya ule wa Sikinde.

“Mama Ima naye alikuja na madai yake ili aniruihusu kujiunga na TOT, alitaka jokofu (freezer), mtaji (kiasi cha pesa) na sofa. Vitu ambavyo vilikubaliwa na kukamilishwa,” anakumbuka Jumbe.

Kwa mujibu wa Jumbe, TX Moshi aliahidiwa gari, pesa taslimu Sh4 milioni na mshahara mzuri pamoja na kiwanja Mbezi. Mke wake alitaka avutiwe bomba la maji ahadi ambayo pia ilitimizwa.


TX MOSHI AMCHOMOA TOT

Ndani ya Msondo Ngoma hali ilikuwa mbaya sana baada ya kusikia TX Moshi anataka kuhama bendi hiyo kwenda kujiunga na TOT Plus. Vitisho vilikuwa vingi kwake kutoka kwa mashabiki wa bendi hiyo.

Pia, maseneta wa Msondo Ngoma walikubaliana kumnunulia gari mwimbaji huyo ili asihame na kumtaka TX Moshi (au Shaban Muhoja Kishiwa) kurudisha pesa na kadi ya gari ya TOT Plus.

Jumbe anasema siku waliyopangiwa kwenda kutambulishwa kwa Makamu wa Rais Dokta Omari Ali Juma na baadaye Idara ya Habari (MAELEZO), dereva wa Kapteni Komba alianza kumpitia yeye na kwenda kwa TX Moshi.

“Tulipofika Moshi alikuwa chumbani, tulikaribishwa sebuleni na akatoka tukasalimiana na akarudi tena chumbani. Alichukua muda mrefu tukajua labda alikuwa akijiandaa. Baadaye alitoka na fuko la fedha, kadi ya gari na funguo za gari akisema tuvirudishe TOT Plus,” anasema Jumbe.


KUSHUKA DARAJA

Jumbe anasema baada ya TX Moshi kuchomoa, yeye ndiye akateuliwa kuwa kiongozi wa Bendi ya TOT Plus na laiti kama mwimbaji huyo asingechomoa yeye (Jumbe) angekuwa kiongozi msaidizi wa bendi hiyo.

Kundi zima la TOT liliweka kambi jijini Tanga na kutengeneza albamu ilikuwa na jina la Sarafina. Wakiwa kambini kuna siku Jumbe aliletewa gazeti na mmoja wa wanamuziki wa TOT Plus.

Ndani ya gazeti lile kulikuwa na habari ya kumkejeli. Mwanamuziki mmoja wa Sikinde (jina tunalo) alisema kitendo cha Jumbe kukubali kujiunga na TOT ni sawa na kushuka daraja.

“Alisema ni sawa na mchezaji aliyekuwa akicheza Ligi ya Bendesliga (ya Ujerumani) na kujiunga na Ligi ya Ufaransa (League One) ambayo ilikuwa ikiaminika ni nyepesi. Yaani nimetoka ligi ngumu na kujiunga na nyepesi,” alifafanua Jumbe.

Lakini Jumbe anasema akiwa na TOT Plus ambako alitunga nyimbo mbili za Nani Kaiona Kesho na Punching Bag alikuwa na amani sana ndani ya bendi hiyo kwa kuwa wanamuziki vijana walimkubali sana. Kipindi hicho pia mwanamuziki huyo alitoa wimbo wa Zing Zong wa Siri ya Nini.

Huku nyuma pia, Sikinde waliurekodi wimbo wa Nani Kauona Mwaka ambao maudhui yake ni yaleyale ya wimbo wa Nani Kaiona Kesho. Sikinde iliandika wimbo huo kuwa ni utunzi wa bendi na kulifuta jina la Jumbe.

Pia, baadhi ya wanamuziki wa Sikinde waligoma kumpa chochote mwanamuziki baada ya mauzo ya albamu ya wimbo huo kuuzwa pamoja na wengine kupendekeza hilo lifanyike.

“Achana na mafanikio ya kimaisha ndani ya bendi hiyo lakini nilikuwa na imani ya moyo na nilisafiri karibu katika mikoa yote ya Tanzania,” anasema.


DILI LA MSONDO NGOMA

Akiwa TOT Plus, Jumbe alikuwa akiendelea kuwasiliana na mwanamuziki Benovilla wa Sikinde na mkataba wake wa miaka miwili wa TOT Plus ulikuwa ukifikia ukingoni.