Hivi ndivyo Mzee Matata alivyowaaga wasanii wenzake Mizengwe

Wakati tasnia ya uigizaji ikiwa katika wingu zito baada ya kumpoteza msanii mwenzao, Jumanne Alela ’Matata’, aliyekuwa akiigiza kipindi cha luninga cha Mizengwe, kiongozi wao ameeleza namna alivyowaaga siku chache kabla ya kufikwa na umauti.
Akizungumza na Mwanspoti leo Jumatano Juni 16, 2021, kiongozi wa kundi la Kash Kash ambalo ndilo linaigiza maigizo ya Mizengwe, Mkwere Original, amesema aliwaambia kuwa mara hii hatoboi.
Mkwere amesema hii ni baada ya kwenda kumsalimia wiki moja iliyopita nyumbani kwake maeneo ya kwa Ali Mboa alipokuwa akijiuguza.
“Huyu mtu ameanza kuwa serious kuumwa kama mwezi mmoja uliopita ambapo alikuwa hata kuigiza hawezi na sisi tukawatunaenda kumsalimia nyumbani kwake na hata harakati za kumpeleka hospitali na kumrudisha tulikuwa tunashiriki pia.
“Hata hivyo moja ya neno ninalolikumbuka alilotumbia wakati tulipoenda kumsalimia ni kuwa ‘Wanangu eeeh mara hii sitoboi’ neno ambalo hata hivyo hatukulichukulia kwa uzito,” amesema  Mkwere.
Akielezea dakika zake za mwisho zilivyokuwa kwa msanii huyu,  amesema Matata siku mbili hizi alikuwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo mara ya mwisho kwenda kumuona ilikuwa juzi, kwani walikuwa wakiruhusiwa kuingia wachache huku akitaja ugonjwa uliokuwa ukimsumbua zaidi kuwa ni sukari.
Kuhusu ratiba za mazishi, amesema mwili wa matata utazikwa kesho katika makaburi ya Buguruni na msiba kwa sasa upo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Enzi za uhai wake Mzee Matata alitesa na maigizo katika kikundi cha Mizengwe kilichokuwa na wasanii, Mkwere, Safina, Sumaku na Maringo Saba.